Fisadi Gani Mbili Za Mayahudi Zilizotajwa Katika Suwrah Bani Israaiyl?
Fisadi Gani Mbili Za Mayahudi Zilizotajwa Katika Suwrat Bani Israaiyl?
SWALI:
Assalam alaykum
Natumai mnaendelea vizuri na afya njema na shughuli zenu za Dawa. Ningependa kuuliza: Katika kitabu kitukufu Qur'an, Allaah ameelezea katika Suwrah Al-Israa au Bani Israel katika aayah ya 4 - 5.
Napenda kujua hizo fisadi mbili zilizoandikwa kuwa Wana wa Israel watazifanya, haswa hiyo ya kwanza ilitokea wakati gani na wakati wa Nabiy gani. Na ni watu gani katika waja wake Allaah ambao aliwapeleka kuwatia adabu. Kisha napenda kujua hiyo fisadi ya pili ni ipi au lini itatokea. Na kama kuna mengine ya ziada tuchambulini kwa hawa watu ambao Allaah amewalaani kwa jeuri yao.
Shukran
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakika hili ni swali nyeti ambalo inatakiwa kila Muislamu awe na ufahamu nalo. Swala la Mayahudi ambao Qur-aan, Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hata historia imetubainishia uovu wao usio kifani. Lakini hapa si mahali pake kuelezea hayo kwani swali mbele yetu ni jengine japokuwa linahusiana.
Hakika ufisadi wa Bani Israaiyl umetokea mara nyingi katika historia yao, idadi zake haziwezi kuhesabika. Na makusudio ya Aayah ni kuwa mara mbili hizi ufisadi ni dhahiri kabisa. Na kuwa Aayah inayofuata ni dalili kuwa kusalitishwa juu yao waja wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kutaendelea mpaka Siku ya Qiyaamah kwa sababu ya ukafiri na uasi wao. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
..وَإِنْ عُدتُّمْ عُدْنَا ۘ
Na mkirudia (ufisadi na dhulma), Nasi Tutarudia (kukuadhibuni).” [Al-Israa: 8]
Kabla hatujazifafanua Aayah hizo ni vyema tuandike tafsiri zake ili tuwe katika ufahamu kwa tunayoyaeleza. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
وَقَضَيْنَا إِلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ فِي الْكِتَابِ لَتُفْسِدُنَّ فِي الْأَرْضِ مَرَّتَيْنِ وَلَتَعْلُنَّ عُلُوًّا كَبِيرًا ﴿٤﴾فَإِذَا جَاءَ وَعْدُ أُولَاهُمَا بَعَثْنَا عَلَيْكُمْ عِبَادًا لَّنَا أُولِي بَأْسٍ شَدِيدٍ فَجَاسُوا خِلَالَ الدِّيَارِ ۚ وَكَانَ وَعْدًا مَّفْعُولًا ﴿٥﴾
Na Tukawahukumia wana wa Israaiyl katika Kitabu kwamba: Bila shaka mtafanya ufisadi katika ardhi mara mbili, na bila shaka mtapanda kiburi kuasi kwa dhulma na kutakabari kukubwa. Basi ilipokuja ahadi ya kwanza kati ya fisadi mbili; Tulikutumieni waja Wetu wenye nguvu kali za kupigana vita, wakaingia kusaka (na kuwaua) ndani ya majumba na ikawa ahadi ni ya kutekelezwa. [Al-Israa: 4-5]
Wametofautiana Mufassiriyna kuhusu maana ya kufanya ufisadi mara mbili katika ardhi. Nasi tutaangalia baadhi ya tafsiri na kutaja mwishowe rai ambayo ina nguvu zaidi.
Ash-Shawkaaniy katika Fat-hul-Qadiyr amesema:
"Mara mbili inasemwa kuwa, mara ya kwanza ni baada ya kuuliwa Ash‘iyaa’ au kufungwa kwa Nehemia au kukhalifu amri za Tawraat. Na mara ya pili ni kuuliwa kwa Yahyaa bin Zakariyyaa (‘Alayhimas-Salaam) na azma ya kumuua ‘Iysaa ('Alayhis-Salaam). Na panasemwa kuwa ufisadi wa kwanza umetokea lakini wa pili bado. Nao walitumilizwa watu wetu wenye mapigano makali yaani wenye nguvu katika vita na ukali wanapopambana na adui. Panasemwa kuwa huyu alikuwa ni Nebukadneza na jeshi lake kutoka Babeli".
Hapa upo mgongano wa maelezo kwani mfalme Nebukadneza alikuja takriban miaka 580 kabla ya kuja kwa Yahyaa na ‘Iysaa (‘Alayhimas Salaam).
Na amesema Abul Fidaa’ Ismaa‘iyl bin Kathiyr katika tafsiri yake Tafsiyrul Qur-aanil ‘Adhwiym, mjalada wa 3, uk. 28 – 29:
"Hakika Mufassiriyna wa zamani na sasa wametofautiana ni kina nani hawa waliosalitishwa juu yao? Ibn ‘Abbaas na Qataadah wanasema kuwa ni Jaaluwt na jeshi lake ambao waliwasumbua lakini baadae wakawa ni wenye kupata nguvu na Daawuwd (‘Alayhis-Salaam) kumuua Jaaluwt". Na kwa hiyo Akasema (Ta’aalaa):
ثُمَّ رَدَدْنَا لَكُمُ الْكَرَّةَ عَلَيْهِمْ
Kisha Tukakurudishieni nguvu zenu dhidi yao... [Al-Israa: 6]
"Amesema Sa‘iyd bin Jubayr kuwa huyo alikuwa na mfalme wa Muswul, Senharib na jeshi lake. Na kutoka kwake na wengineo kuwa huyo alikuwa ni mfalme wa Babeli, Nebukadneza".
Wamesema baadhi ya Mufassiriyna kuwa maadui waliowatoa katika majumba yao walikuwa ni qaumu ya Jaaluwt ambao walikuwa wamewashinda Bani Israaiyl na kuwaua idadi kubwa. Hii ilikuwa ni kabla ya kurudishiwa nguvu zao chini ya uongozi wa Twaaluwt.
Na kauli ya Allaah Aliyetukuka:
ثُمَّ رَدَدْنَا لَكُمُ الْكَرَّةَ عَلَيْهِمْ
Kisha Tukakurudishieni nguvu zenu dhidi yao...[Al-Israa: 6]
Hii ni wazi kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aliwanusuru baada ya kujuta na kutubia, nao wakawa ni wenye kulishinda jeshi la Jaaluwt na Nabiy Daawuwd (‘Alayhis-Salaam) akamuua Jaaluwt.
Na kauli Yake:
وَأَمْدَدْنَاكُم بِأَمْوَالٍ وَبَنِينَ وَجَعَلْنَاكُمْ أَكْثَرَ نَفِيرًا ﴿٦﴾
...na Tukakuongezeeni mali na wana, na Tukakufanyeni wengi zaidi kwa idadi na nguvu. [Al-Israa: 6]
Hii ilipatikana katika kipindi cha dhahabu chini ya utawala wa Manabii Daawuwd na Sulaymaan (‘Alayhimas-Salaam) cha miaka 80. Ama baada ya kipindi hiki cha dhahabu dola hiyo iligawanywa sehemu mbili: Dola ya Yahudha na Dola ya Israaiyl. Ufisadi uliingia kati yao, mzozano na mapambano mpaka Dola ya Israaiyl ilipopigwa na kutawaliwa na Assyria mwaka wa 721 (kabla ya kuzaliwa kwa ‘Iysaa) na ufalme wa Yahudha kusambaratishwa katika mwaka 588 (kabla ya kuzaliwa 'Iysaa) na mfalme wa Babeli, Nebukadneza. Historia ya bani Israaiyl baada ya hapo haikuwa ila ni silsila ya maasi, adhabu, balaa na maafa ambayo yaliwapitia wakiwa na watu tofauti” [Banu Israaiyl Fiyl Qur-aan was Sunnah, Mj. 2, uk. 366].
Na wengine wamesema: "Ufisadi wao wa mara ya pili ulikuwa wakati wa utawala wa Warumi ambapo jemedari jeshi wake, Titus aliwaua wengi na wengine kushikwa mateka na wengine kukimbia. Tukio hili lilitokea baada ya kuuliwa Nabiy Yahyaa (‘Alayhis Salaam) kwa miaka kadhaa" [Al-Khatwarul Yahuwd, uk. 23-25].
Kwa ufupi tunaweza kusema kuwa ufisadi wa Wana wa Israaiyl ulikuwa mwingi kuanzia wakati wa Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) na kila mara walisalitishwa watu wengine. Kwa mfano Fir-awn, Jaaluwt, Waasuri, Wababeli, Wayunani, Wamakdoni, Warumi, na mwisho kabisa watakuwa ni Waislamu. Waislamu ambao watasimama imara kwa kufuata maagizo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Wakati huo mpaka mawe na miti itazungumza kumuashiria Muislamu pale alipojificha Myahudi. Hapo watauliwa na kushindwa na ardhi tukufu hiyo kurudi mikononi mwa Waislamu.
Na Allaah Anajua zaidi