Mke Mjeuri Sana - Anamwambia Mtoto Wangu Kuwa Nimeshakufa, Nifanye Nini?

 

 

SWALI LA KWANZA:

 

Baada ya kumshukuru Allaah na kumtakia rehma mtume wake (s.a.w)na washukuru sana na ndugu zangu kwa website hii Allaah aendeleze na awape ujra kwa kazi hii. Suali langu,mimi nina mke lakini mke wangu huyu hanihishimu wala hanitwi.Tunapo kosana yeye hutoa maneno yasio stahiki na yuko tayari kunizulia mambo au katika niliyo sema kuyabadilisha.Kwake yeye yuko tayari kuapa kwa uzushi anao nisingizia na yeye huaminiwa.Tuko na mtoto mmoja pamoja, mtoto mwenyewe bado ananyonya.Juu hii ashamtamkia mtoto kua yeye hana baba babake ameshakufa.ameshasema huyu mtoto mimi sitamuona wala familia yangu.hofu yangu nikwamba nikimuacha huyu mke nitamkosa mwanangu naatapata mafunzo mabaya.sasa nifanye nini?kwani sishaswali istighara sikupata majibu.shukran

 

SWALI LA PILI

AAWW

Nnajambo ambalo linanitatiza sana yaani nimefikia sehemu ambayo sina hata lazaidi.kusema nimeshindwa inanibitu nibaki nnaayapa macho. kifipi ni hivi, mke wangu ni mjeuri sana kiasi ambacho nimejaribu kutowa ushauri mawaidha kama mume ndani ya nyumba ila bado tu mjeuri nimejitenga naye kimalazi kutaka aelewe ilabadutu.hakunajambo analolifanya kwa idhni yangu.nnacho mkataza hicho ndio anacho fanya.Naomba ushauri. InshaAllaah

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza kabla hatujajibu maswali yenu, tunawakumbusha kuwa mnapoandika jina la Allaah au Mtume, msifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali muandike kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andikeni (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andikeni Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu.

Pia Salaam hazifai kufupishwa kwa kuandikwa (A.A) au (A.A.W.W.) kwani haijafundishwa hivyo na pia ni kujikosesha fadhila za Salaam kama tulivyoelezwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo nayo tujizoeshe kuandika (Assalaamu ‘alaykum) au (Assalaamu ‘alaykum wa rahmatullaah) au (Assalaamu ‘alaykum wa Rahmatullaah wa Barakaatuh) kwa ukamilifu na tutakuwa tumeiga mafunzo ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia tutakuwa tumezoa thawabu zote za Salaam kama tulivyofundishwa.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muuliza maswali hayo mawili. Maswali haya mawili yanafanana, hivyo tutajaribu kwa mpigo mmoja kuyajibu yote mawili.

Matatizo ya kifamilia katika jamii yetu ni mengi na yanakariri kariri kila mara. Tatizo kubwa tulilonayo ni katika uchaguzi na malezi yetu tunayopata kutoka kwa wazazi. Malezi ya watoto ni muhimu na pia uchaguzi wa mke kwa mume na kinyume chake kwani kukosa kufanya hivyo ndiyo maana tunapata shida chungu nzima baina ya wanandoa. Kwa umuhimu mkubwa wa uchaguzi huo ndiyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuambia:

Mwanamke huolewa kwa sababu nne: Mali yake, nasaba yake, uzuri wake na Dini yake. Chagua mwenye Dini utasalimika” (al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Abu Hurayrah [Radhiya Allaahu ‘anhu]).

Mara nyingi tunapotaka kuoa huwa hatutaki kutafiti na kujua hali ya mwanamke na familia yake. Lau kama tungekuwa tunafanya hivyo basi hatungeingia katika matatizo hayo kwani ungekuwa umejua yale katika sifa na tabia za atakayekuwa mkeo. Hata hivyo, hayo yashapita tuangalie uliyo nayo wakati huu. Kwa mujibu wa swali lako inaonyesha mkeo hana akili timamu kwani si akili ya mtu au mwanamke kuzungumza na mtoto anayenyonya.

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Ametueleza kuhusu kumrekebisha mke aliyekengeuka na kutoka katika twaa. Anatuambia (Subhaanahu wa Ta‘ala):

Basi wanawake wema ni wale wenye kutii na wanaojilinda hata katika siri kwa kuwa Allaah Ameamrisha wajilinde. Na ambao mnachelea kutoka katika utiifu wanasihini, muwahame katika malazi na wapigeni. Wakikutiini msiwatafutie njia ya kuwaudhi bure. Hakika Allaah ndiye Aliye juu na Mkuu. Na mkichelea kutakuwapo mfarakano baina ya mke na mume basi pelekeni muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za mke. Wakitaka mapatano Allaah Atawawezesha. Hakika Allaah ni Mjuzi, Mwenye khabari” (4: 34 – 35).

Inaonyesha tayari umeshaanza kuchukua hatua kwa mambo yaliyoelezwa hapo juu katika Aayah – kumpatia nasiha na kujitenga naye kimalazi. Jambo lililobaki ni kujaribu kumtia adabu lakini sio kumpiga mpaka kumuumiza. Adabu hiyo hutiwa kwa kitambara au nguo kwa taratibu bila kuacha alama. Ikiwa hilo limeshindikana basi iatabidi uitishe kikao baina yako, yeye (mkeo), wazazi wako na wazazi wake (wawakilishi kutoka pande zote mbili). Ikiwa kikao kitafanyika kwa njia ya ikhlasi basi suluhisho litapatikana baina yenu. Ikiwa hakuna suluhu yoyote baina yenu basi hakuna kheri kuishi pamoja kama mume na mke.

Fahamu kuwa mtoto akiwa mchanga mama ndiyo anakuwa haki zaidi ya kumlea kisheria nawe utahitajika kumtunza kwa pesa za kuweza kumkimu kimaisha. Lakini kama ulivyosema unahofia malezi yake hayatakuwa mazuri kwani mkeo hana maadili muruwa ya Kiislamu itabidi uende ukashitaki kwa Qaadhi kuhusu hilo. Ikiwa unapoishi hakuna Qaadhi itabidi utafute Shaykh, mcha Mungu na muadilifu ili awasikilize na kutoa uamuzi kwa mujibu wa Uislamu.

Twakuombea kila la kheri, fanaka na tawfiki.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share