Mume Anakesha Katika Internet Hampi Mke Haki Yake - Mke Afanyeje?

 

SWALI:

baada  ya  salam ningependa   kutanguliza shukrani za dhati kwa wale wanao shughulikia site hii na  ningependa   kujuwa je ni haki  hii...ikiwa mume wangu anakaa online usiku bila  ya kunijali  kama mimi ndo mke wake wa ndoa na ninapo mwambia yeye  anakuwa mkali  na  pia ananambia ninawasiwasi wa nini wakati yeye  yumo ndani hatoki nje? lakini mimi ni mkewe wa ndoa  na pia  ninahitaji  kupewa haki yangu na  pia   nahitaji heshima ya ndoa yangu na pia nahitaji  kuenziwa  sio mke tu ndani ya nyumba  bila  mapenzi  wala  imani wala huruma.kwani anapo fanya hivo mimi  nahisi kama hanitaki  tena au  kapata mwengine...aAllaahu a'lam. na pia inanifanya hata nifikirie  mambo mabaya kutokana bwana  huyu hanipi  haki yangu.

ustadh  naomba  uniwekee wazi  juu ya  hilo   kutoka  kwenye  quran  na  hadith na pia ni nini nifanye na nimeshajaribu kusema  nae mara  nyingi tu na bila  ya  kunisikiliza? JazakAllaah khair..



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu muuliza swali. Baina ya wanandoa kila mmoja ana haki na wajibu juu ya mwenziwe. Na katika haki ya mke kutoka kwa mume sio kupewa chakula, malazi na nguo tu bali pia kupatiwa haki ya unyumba. Kukosa kupewa haki hiyo ni sababu moja anayoruhusiwa mke kuomba talaka kwa mumewe.

Ni jambo la busara ulilofanya kwa kuzungumza na mumeo lakini bila ya mafanikio. Tunaomba ujaribu tena kuzungumza naye wakati unapoona ana makini na hali ya kuwa anaweza kukusikiliza. Usife moyo kwani kufa moyo si katika sifa ya Muislamu. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

"Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yuusuf na nduguye, wala msikate tamaa na faraji ya Allaah. Hakika hawakati tamaa na faraji ya Allaah isipokuwa watu makafiri" (12: 87).

Weka muda wa kujaribu kuokoa ndoa hiyo kwa mfano mwezi au na vikao vitatu naye.

Ikiwa hukufanikiwa, basi waeleze wazazi wake na wazazi wako au wawakilishi wenu muwe na kikao cha kujadili suala hilo kwa njia nzuri ya kutaka suluhu. Lau mtataka suluhu basi Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atawafanikishia na kuwaondolea tatizo hilo.

Ikiwa hukufanikiwa kwa njia hiyo ya pili pia, itabidi upeleke kesi yako kwa Qaadhi au Shaykh aliye karibu nanyi ili aingilie kati na kusuluhisha baina yenu. Kukiwa hapatopatikana ufumbuzi itabidi akuache au uombe talaka.

Twaomba msifike kote huko bali mpate suluhisho muafaka. Twawaombea kila la kheri.

Na Allaah Anajua zaidi

Share