Mume Mzinifu, Haswali, Hapendi Kusikiliza Mawaidha, Mshirikina – Nifanyeje Kuhifadhi Dini Yangu?

 

 

Mume Mzinifu, Haswali, Hapendi Kusikiliza Mawaidha, Mshirikina  

Nifanyeje Kuhifadhi Dini Yangu?

 

 

 

SWALI:

 

Assalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh.

 

Hongereni kwa kazi kubwa ya kutuelimisha waislam. Allah atakulipeni Inshaallah, Amin. Nimeishi na mume wangu kwa miaka 12. Tangu aliponioa nikagundua kuwa ni mzinzi, lakini nilifanya subra ya kumueleza hajajirekebisha. Hivi sasa anazini na watoto wa shule kuanzia miaka 16 hadi 21. Yeye ana miaka 56. Hana ibada yoyote anayofanya hafungi ingawa haonyeshi nyumbani, wala haswali, akisikia mawaidha anatoka, pia ni mshirikina kupindukia. Je nifanyeje ili nisiharibu Uislam wangu?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hakika ni kuwa hali hii katika jamii yetu itaendelea kwa muda mrefu sana kwani tumekataa kufuata maagizo ya Uislamu. Tumekuwa tukikariri sana mas-ala ya ndoa katika Uislamu pamoja na masharti yake lakini inaonekana hasa kwa wanawake suala hilo halijazingatiwa hivyo kuwatumbukiza katika matatizo kama hayo na mengine mengi.

 

Tatizo hilo huwa linajitokeza kwa kuwa ima mume au mke hakumchagua wapili wake katika misingi ya kidini. Lau kama mwanamke angekuwa na uangalifu pamoja na kufuata agizo la Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) la kutafuta mume mwenye Dini janga lote hili lingekuwa limemuondokea kabisa shingoni mwake kuanzia hapo awali. Tatizo hilo linawafikia wengi kwa kukosa kufuata maagizo yaliyo mepesi na sahali.

 

Kulingana na maelezo yako ni kuwa mumeo haswali, mzinzi na mshirikina. Mambo yote haya yanamtoa mtu katika Uislamu. Umefanya vyema kuzungumza naye lakini inaonyesha kuwa hasikii kabisa. Sasa unaweza kufanya yafuatayo:

 

 

1-Itisha kikao ambacho utakuwa wewe, yeye, wazazi wako na wake mzungumzie suala hilo kwa uwazi kabisa. Hapo unataka uelezeee wazi yanayokusibu kwa ukaidi wake wa kufanya maovu. Ikiwa atakubali kujirekebisha sawa, lau hataki basi itabidi muachane.

 

 

2-Ikiwa njia hiyo imeshindikana, basi tumia Mashaykh wa hapo na watu anaoelewana nao wazungumze naye kuhusu hilo.

 

 

3-Ikiwa hatajirekebisha basi itabidi uende kwa Qaadhi na uombe muachane.

Hivyo unatakiwa ufanye haraka kuhusu hilo kabla Dini yako pia haijaharibika.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share