Kampeleka Nchi Za Kigeni Kisha Ameoa Mke Mwengine, Je, Nini Hukmu Yake?
SWALI:
Asalaam Alaykum warahmatu llah taala wabarakaatu. mimi napenda kuuliza swali hili:mwanamme kumpeleka Ulaya mkewe akamuacha kule na watoto halafu yeye akarudi Afrika na baada ya mwaka yeye akaoa mke mwengine, na wakati anampeleka ulaya, mkewe alikua hataki kwenda lakini kenda kwa kumsikiliza mumewe na mkewe alipojua kama mumewe kaoa, akamuuliza mumewe kwa nini umeoa? Mume akamwambia mkewe nimeoa nataka stara kwa sababu siwezi kujizuia, mkewe akamwambia umenileta huku mwaka tu na mimi nilikua sitaki kuja huku. Swali langu lipo hapa huyu mume alikua anamtaka kweli mkewe au alikua anamuondoa apate kuoa na vipi sheria inasema nini kuhusu stori hii.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mke kupelekwa Ulaya na mumewe kuoa mwengine.
Hakika ni kuwa mume amepatiwa haki na Uislamu kuoa mke wa pili, wa tatu na hadi wa nne. Hata hivyo, Uislamu umekataa dhuluma kwa wake wakati mume anaoa zaidi ya mke mmoja. Ikiwa mume hawezi kufanya uadilifu basi Uislamu umeamua kuwa mwanamme huyo aoe mke mmoja tu.
Mke ambaye amepelekwa Ulaya pia ana haki kutoka kwa mumewe kwa kupatiwa chakula, makazi na kustareheshwa. Na pia haifai kwa mume kukaa zaidi ya miezi minne mbali na mkewe. Mume amefanya makosa kumpeleka mkewe mbali naye, baadaye yeye akaoa kwa kuwa anahitaji stara, ilhali mke pia anataka stara. Ingekuwa ni busara zaidi kwa mume kuoa mke wa pili, mke wake wa kwanza akiwa huko huko Afrika na akampatia kila mmoja wao haki yake.
Kile ambacho tungeweza kumshauri mke huyo ni kutafuta njia bora ya kuweza kutatua tatizo
1. Kuzungumza na mumewe kwa njia ya upole na uzuri ili kutatua tatizo
2. Kuwashirikisha wazazi wa pande zote mbili ili kupata ufumbuzi wa tatizo
Twawatakia kila la kheri na fanaka na maahusiano mema baina yenu.
Na Allaah Anajua zaidi