Mume Anaishi Na rafiki Zake Huja Kwangu kulala Kwangu Anapopenda tu? Ndoa Inasihi?

 

SWALI:

assalam alaykum

Sifa njema zote in za Allaah. Allaah awajaze kila la kheri wahusika wote wanaojitahidi kuelemisha jamii ya kiislam kupitia mtandao huu. Nilinataka kuliza kuhusu wakati wa kuvunjika kwa ndoa. Jee ndoa bado ina sihi Ikiwa mume hakai nyumba mmoja na mke bali kakodi sehemu pamoja na rafiki zake na huwenda tu siku chache kulala nyumba ya mkewe? Bila shaka mume huyu atakuwa hajatimiza wajibu wake lakini je patakuwa pana ndoa tena wakati huyo mume hamhudumii mkewe kama ipasavyo ila huwenda kwa mkewe hususan kwa sababu za malazi siku apendazo. Ikiwa hali ndo kama hiyo je ndoa bado ipo au talaka pekee ndo inavunja ndoa?

Jazaka Allaah kheir.



 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu kwako ewe ndugu yetu kwa swali lako. Hakika ni kuwa matatizo ya ndoa katika jamii yetu ni mengi na hatuna ila kumshukuru Allaah. Tunaomba taufiki kutoka kwa Allaah Aliyetukuka kuhusu mas-ala haya.

Tatizo linalojitokeza ni watoto kutopatiwa malezi mazuri na kuweza kuchukua na kutekeleza majukumu. Maandalizi kuhusu ndoa hayako katika maadili ya Kiislamu kama kuhakikisha udini wa kila mmoja. Pia kutofundishwa majukumu na ya kila mmoja katika wanandoa kabla ya kuingia katika Nikaah yenyewe. Hili limekuwa tatizo sugu kati yetu mpaka limeenda kuvunja nyumba nyingi.

Suala lako hili linatoa maswali mengine mengi yakuulizwa wewe. Kwa mfano, je wewe umeridhia hali hiyo? Je, mume anakutambua kuwa wewe ni mkeo? Je, ushawahi kumkalisha chini mumeo na kuzungumzia kuhusu suala hilo? Ikiwa ushawahi, je alisema nini? Ikiwa hukufanikiwa je, ulijaribu kuwaita wazazi wako na wake ili mzungumzie kuhusu jambo hilo?

Huu ni mpangilio ambao lau ungeufuata basi ungepata ufumbuzi wa suala lako hilo hata bila ya kuuliza hili swali lako. Hata hivyo ndoa ina masharti na majukumu ambayo kila mmoja anawajibika katika hilo. Ni wajibu wa mume kumlisha, kumvisha, kulipa kodi ya nyumba na mke anapokuwa mgonjwa basi ahudumiwe matibabu yake n.k.. Ikiwa mke hatimiziwi haya ana haki kwenda kwa Qaadhi kumshitaki. Qaadhi atasikiliza pande zote mbili na ikiwa hayo uyasemayo ni kweli basi atalazimishwa ima akutizame au aachishwe.

Umetueleza kuwa mume wako anakuja mara nyingine kulala nyumbani kwako, lakini hukutueleza kama anafanya nawe tendo la ndoa.

Juu ya yote hayo maadamu mume hajatoa talaka ima kwa maneno au kwa maandishi basi wewe bado ni mke wake. Jambo tu ambalo unaweza kufanya ni:

  1. Kuzungumza naye na kumnasihi.

  2. Kutumia wazazi wako na wake.

  3. Kutumia marafiki zake wa karibu.

  4. Kwenda kumshitaki kwa Qaadhi au kiongozi wa Dini yetu ya Kiislamu katika mji unaoishi ili upate ufumbuzi.

Tunakutakia kila la kheri na kuondokewa na tatizo hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share