Familia Yampiga Vita Mume Wangu Nifanyeje?

 

SWALI:

 

Familia yangu yampiga vita mume wangu, nimechanganyikiwa sijuwi ni fanye nini shukran



 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Swali lako hili halijakamilika kabisa kama tunavyoliona. Ni jambo lililo muhali sana kuona familia yote inampiga vita mtu fulani na hasa akiwa anahusiana na familia kwa njia ya kuoa binti yao kama ilivyo katika kesi yako.

Ni wazi kwetu kuwa yapo mambo ambayo hujatufahamisha kutuwezesha kukusaidia kwa njia iliyo nzuri kabisa. Tutahitaji maelezo zaidi ili kuweza kukupatia nasaha muafaka katika suala hilo.

Je, nikaha yenu haikukubaliwa na familia yako? Ikiwa jawabu ni la, ni sababu gani zilizowafanya wazazi na familia yako kumpiga vita mumeo. Je, maadili yake si mazuri kama yanavyotarajiwa kwa Muislamu? Je, mumeo ni Muislamu asiyefuata Dini yake?

Lau majibu ya haya maswali yatakuwa ni ndio basi familia itakuwa ina haki ya kumpiga vita mumeo. Wewe unafaa kwa wakati huu uwe mpatanishaji baina ya familia na mumeo kwa njia inayolingana na vile Uislamu unavyotaka.

 Ikiwa mlitumia njia mbaya ya kuoana ambayo haijamridhisha Allaah Aliyetukuka wala wazazi basi inabidi mrekebishe hilo kwanza kabla ya kuweza kupata suluhu za kudumu. Na ikiwa mlitumia njia ya sawasawa kwa kuchaguana lakini familia kwa sababu moja au nyingine wakakataa nyinyi muwe pamoja inafaa utumie mbinu za kuweza kuwakinaisha familia yako kuwa uchaguzi wako ni wa sawa na inahitajika wao wawasaidie ili muwe na utulivu katika ndoa pamoja na masikilizano.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share