Mume Katoa Maneno Kwa Mkewe Kuhusu Kitendo Cha Ndoa, Maneno Hayo Yanamtia Mashaka Mkewe

SWALI:

 

Assalamu Alaykum.

Naomba jina lihifadhiwe. Tumeingiwa na "shubha" juu ya "Mwanamke alitakiwa kufanya tendo la ndoa na mumewe, kwa bahati mbaya mwanamke huyo kwa wakati huo hakumfanikishia mumewe. Mwenyewe anasema kulingana na mazingira ya wakati huo lakini si kwa sababu ya ugonjwa. Na haikua kawaida kumkatalia kwa sababu ni mtu mwenye uelewa juu ya haki za mume kwake kwa kiasi. Lakini mumewe alikasirika na kusema, basi UCHI wako mwenyewe si lazima. Akamuuliza unanambia hivyo? Akamwambia ndio kwani wangu si wako mwenyewe, wako mwenyewe.

 

Sasa anauliza wakati, "Mimi ni wake, inakuaje aseme vile? Si itakua kama kaniepuka?" Kwa hiyo anaomba kutolewa wasi juu ya usemi huu kwani unamkosesha raha. Kwa vile ni suala zito. Au haukuleta athari. Kwani kwa unde wao wanaendelea vizuri na hakuna tofauti yoyote (yeye na mumewe). Isipokua yeye ndie mwenye wasiwasi. Tunategemea kupata jibu zuri na kwa haraka. Allah atuwafikishe.

 


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu hasira ya mume kwa mkewe. Hakika ni kuwa kama tunavyokariri mara kwa mara katika masuala ya kijamii ni kuwa matatizo haya yanatokea kwa sababu ya ukosefu wa maadili mema. Inafaa mwanamke afanye juhudi ya kumridhisha mumewe kwa hali zote na vile vile mwanamme mwema na mzuri ni yule ambaye ataweza kumfikiria mkewe hasa anapomtaka akaona kuwa labda kuna tatizo fulani. Hawa ni wanandoa ambao wanatakiwa watazame hali ya kila mmoja na kuvulimiana na kusameheana kwa kiasi kikubwa panapotokea tatizo.

 

Huenda mume akamtaka mke lakini kukawa na shida, hivyo, mume ampatie maneno matamu, ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameyaita: “Ni sadaka” (al-Bukhaariy na Muslim). Kwani pia huenda mke akamtaka mume na mume akawa ana tatizo wakati huo hivyo hakuweza kumtosheleza, hapo pia mke afahamu. Kwani bila kuafikiana kila mmoja kwa mwengine mambo hayatakuwa mazuri baina yao.

 

Kwa vile tayari limetokea hilo ambalo limetokea inatakiwa mwanamke akae na mumewe wazungumze suala na mke aombe msamaha kwa vile hakuweza kumfurahisha siku aliyotakwa.

 

Usemi huo aliosema huenda ni ile hasira aliyokuwa nayo mbali na kwamba Muislamu anatakiwa aimiliki hasira yake na asiwe ni mwenye kusema lolote lililo baya. Hata kama mume hakudhamiria chochote kibaya lakini neno kama hilo si zuri kutoka kwake kumwambia mkewe kwa hali yoyote na kinyume chake pia.

 

InshaAllaah halina neno na inahitajika kutoa wasiwasi kwani wasiwasi unatoka kwa shetani ambaye dhamira yake si nzuri kwa wanadamu. Wasiwasi pia huleta magonjwa na mambo mengine mabaya, na hakuna madhara makubwa kama shetani kufanikisha shughuli yake hiyo kwa kuwafanya wanandoa kuachana. Ukiona na kusikia wasiwasi tafuta kinga kutoka kwa Allaah Aliyetukuka kwa kusema A‘udhu Billaahi minash-Shaytwaanir Rajiym. Pia soma Qur-aan kwa wingi na pia isikilize ikisomwa mara nyingine.

 

Tunawaombea muweze kusahau yaliyopita na kuganga yajao na tawfiki inatoka kwa Allaah. Tunamuomba Mola Muumba Awape tawfiki na Awape masikilizano mema na jambo hilo lisirudie tena.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share