Anaweza Kuchukua Pesa Za Mume Bila Ya Mume Kujua Kwa Mahitaji Yake?

 

 

SWALI:

Asalam alykum samahani nauliza suali mimi nna watoto baba yao kuna baadhi ya vitu anawapa sasa pengine kuna vitu vyengine watoto wanahitaji na baba yao hataki kuwanunulia au mimi pia nahitaji kitu cha ndani na najua nikimwambia atakua mkali, sasa naweza kumchukulia pesa nikaenda kununua yale mahitaji bila yeye kujua inafaaaaaa au napata dhambi nikifanya hivo? Naomba jibu

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 


Kwa hakika nyumba zetu zina matatizo na hili ni tatizo moja la baba kutotekeleza mahitaji ya mkewe na watoto wake ambalo ni jukumu lake la msingi. Pia kuna tatizo kuwa mke mara nyingi au mara nyingine hutaka mahitaji yanayopita kipimo, hivyo mume kutoweza kumudu kutekeleza hayo.

Hivyo, nasaha zetu kwa wanandoa wawe na masikilizano na waweze kuelewana na kujua majukumu yao bila ya mmoja kumkalifisha mwenziwe kwa kiasi ambacho mmoja wao hataweza kumudu.

Mume asiwe bakhili katika kutekeleza mahitaji ya walio chini yake na wala mke asitake mahitaji juu ya uwezo wa mumewe. Na ndio hapa tunapata mifano kwa Maswahaba (Radhiya-Allaahu 'anhum) – wanaume kwa wanawake ambao walikuwa wanasaidiana katika majukumu na ikiwa mke ni muweza anaweza pia kumsaidia mumewe kama walivyokuwa wakifanya Maswahaba wa kike.

Sasa tukirudi kwa swali letu inafaa mke ajiulize: Je, hivi vitu ambavyo watoto wanataka ni muhimu kwao na vya msingi? Je, vile vitu ambavyo anasema ni vya ndani pia ni vya msingi katika maisha au si muhimu? Ikiwa vitu vinavyotakiwa na watoto au yeye mwenye ni vya msingi basi anaweza kuchukua fedha kutoka kwa mumewe bila ya yeye kujua lakini asichukue zaidi ya mahitaji yake.

 

Akichukua zaidi ya mahitaji hayo basi atakuwa anapata dhambi kwa kitendo chake hicho. Hii inatokana na Hadiyth ya Mtume wa Allah  (Swalla-Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  inayosema: ‘Aishah (Radhiya-Allaahu 'anhaa) anahadithia: “Hind bint Utbah (mke wa Abu Sufyaan (Radhiya-Allaahu 'anhu) alikuja na kuuliza: ‘Ee Mtume wa Allah! Mume wangu ni bakhili, je, kuna ubaya wowote nikichukua kutoka katika mali yake na kutumia kwa ajili ya watoto wetu?” Akamjibu  “Hapana ubaya ikiwa utatumia katika kuwalisha kwa uadilifu, kiasi na wema (usiwe ni mwenye kufuja)” (al-Bukhariy).

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share