Mume Na Watoto Hawaswali Na Hawataki Kunisikiliza
Mume Na Watoto Hawaswali Na Hawataki Kunisikiliza
SWALI:
Assalam alaykum.
Swala langu ni: mimi ni mwanamke nilio olewa na nna watoto swala langu liko hapa huyu mume wangu na watoto hawataki kuswali na kila siku nawambie na hawataki kunisikia, mimi nnaswali, Je, sala yangu inakubaliwa wakati wao hawaswali, halafu nimeshachoka kuwambia kila siku kwahiyo nnaomba msaada wenu mnitumie hikma gani? Naomba nijibiwe swala langu maasalam
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Hili ni tatizo sugu ambalo limezagaa katika jamii yetu. Tatizo hili linatokea kwa sisi kutotilia maanani agizo la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika mke kuchagua mume au kinyume chake. Wakati ambapo tutakiuka agizo la kuchagua mwenye Dini, maadili, muruwa, mwenye ‘Ibaadah, basi isipokuwa wale wanaorehemewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) lakini ndoa inatukua na misukosuko mingi.
Mara nyingi mtoto huwa anafuata ada na desturi za wazazi wao. Ikiwa mtoto ni wa kiume akawa anamuona baba hashughuliki na ‘Ibaadah basi naye atafuata mtindo huo huo na inamwia vigumu kumuelekeza mtoto huyo.
Allaah ('Azza wa Jalla) Akubarikie juhudi zako za kutaka watu wako waongoke kama ulivyo wewe. Jambo hilo ndilo lilihimizwa katika Qur-aan Anaposema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ﴿٦﴾
Enyi walioamini! Jikingeni nafsi zenu na ahli zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe; juu yake wako Malaika washupavu hawana huruma, shadidi, hawamuasi Allaah kwa yale Anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa. [At-Tahriym: 6]
Kwa mujibu wa Aayah hiyo, wewe unawajibika katika kugeuza familia yako ili wasiingie katika ghadhabu ya Allaah ('Azza wa Jalla).
Hakika ni kuwa ‘Ibaadah zako zote unazofanya utapata ujira kamili bila kupunguziwa chochote na Allaah ('Azza wa Jalla) Ambaye Sifa Yake ni Uadilifu. Swalaah zako zote utalipwa kamili pamoja na juhudi unazofanya katika kuwavuta watu wako waje waingie katika njia nyoofu inayomridhisha Allaah ('Azza wa Jalla).
Dada yetu, usiseme nimechoka katika jambo hili, kwani Muislamu hana nafasi ya kusema hivyo. Hiyo si sifa ya Muislamu wa kihakika. Kuhusu hili Allaah ('Azza wa Jalla) Anasema kuelezea namna Nabiy Ya'quwb ('Alayhis Salaam) alipokuwa akiwasisitiza wanawe kutokuwa na tabia ya kukata tamaa:
يَا بَنِيَّ اذْهَبُوا فَتَحَسَّسُوا مِن يُوسُفَ وَأَخِيهِ وَلَا تَيْأَسُوا مِن رَّوْحِ اللَّـهِ ۖ إِنَّهُ لَا يَيْأَسُ مِن رَّوْحِ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْكَافِرُونَ ﴿٨٧﴾
Ee wanangu! Nendeni mkauulizie kuhusu Yuwsuf na ndugu yake; na wala msikate tamaa na faraja ya Allaah; hakika hawakati tamaa na faraja ya Allaah isipokuwa watu makafiri. [Yuwsuf: 87]
Jambo la kuamrisha Swalaah ni jambo lipasalo kuendelezwa na wazazi na kila mchungaji, na hakika ni jambo gumu linalohitaji azma na subira, ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametuhimiza nalo Anaposema:
وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا ۖ لَا نَسْأَلُكَ رِزْقًا ۖ نَّحْنُ نَرْزُقُكَ ۗ وَالْعَاقِبَةُ لِلتَّقْوَىٰ ﴿١٣٢﴾
Na amrisha ahli zako Swalaah, na dumisha kusubiri kwayo. Hatukuombi riziki. Sisi Ndio Tunaokuruzuku. Na khatima njema ni kwa wenye taqwa. [Twaahaa: 132]
Nasaha ambazo tunaweza kukupa sasa ni kama zifuatazo:
1-Jaribu kuwa laini kwa mumeo na uwe mpole katika kumrekebisha tatizo lake hilo la kutoswali. Allaah ('Azza wa Jalla) Anasema:
اذْهَبَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ إِنَّهُ طَغَىٰ ﴿٤٣﴾ فَقُولَا لَهُ قَوْلًا لَّيِّنًا لَّعَلَّهُ يَتَذَكَّرُ أَوْ يَخْشَىٰ ﴿٤٤﴾
Nendeni wawili nyie kwa Fir’awn, hakika yeye amepindukia mipaka ya kuasi. Mwambieni maneno laini, huenda akawaidhika au akakhofu. [Twaahaa: 43 – 44]
Tazama hapa Allaah ('Azza wa Jalla) Anawatuma Manabii wake wawili watukufu kwa mtu aliyejidai kuwa ni Rabb na mwenye kustahiki kuabudiwa, lakini wakaamriwa waseme naye maneno laini na kwa upole. Na ndio Allaah ('Azza wa Jalla) Anatuelezea sifa ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kusema:
فَبِمَا رَحْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ لِنتَ لَهُمْ ۖ وَلَوْ كُنتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ ۖ
Basi ni kwa rahmah kutoka kwa Allaah umekuwa mpole kwao (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Na lau ungelikuwa mjeuri mwenye moyo mgumu wangelitawanyika mbali nawe. Aal-‘Imraan: 159]
2-Jaribu kukaa naye faragha mukiwa yeye na wewe tu ili umpatie nasaha kama mume na mke. Huenda kwa njia hii akawa ni mwenye kukusikiliza katika hilo. Zungumza naye mara moja, mbili na kadhaa. Kwa kukariri kuzungumza naye huenda akabadilika na ikiwa hakubadilika basi fahamu kuwa Allaah ('Azza wa Jalla) Anasema:
إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ ۚ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ ﴿٥٦﴾
Hakika wewe huwezi kumhidi umpendaye; lakini Allaah Humhidi Amtakaye, Naye Anawajua zaidi wenye kuongoka.” [Al-Qaswasw (28: 56)].
3-Je, kutoswali kwake anaamini kuwa Swalaah si waajib? Ikiwa anaamini hivyo basi huyo ametoka Dini hii ya Uislamu na kukaa na mtu kama huyo haifai kwa Muumini wa kihakika. Lakini kabla ya kuacha naye kabisa unaweza kumpatia fursa ajirekebishe, kwa kumuitia Mashaykh wazungumze naye na asimamishiwe hoja. Hilo likishindikana basi itabidi uitishe kikao ambamo wataitwa wazazi wake na wako pia watakuwepo. Ikiwa katika kikao hicho atashikilia ya kwake basi itakuwa bora uachane naye. Kwa sababu ya kufanya hilo kwa ajili ya Allaah ('Azza wa Jalla) basi Atakutolea lenye kheri nawe kwa kiasi kikubwa zaidi.
4-Ikiwa kutoswali kwake ni kwa ajili ya uvivu, goi goi na sababu nyenginezo na anatambua kuwa Swalaah ni waajib, basi huyo ni asi. Kwa minajili hiyo itabidi uzungumze naye mwanzo. Kukiwa hapana mabadiliko yoyote yale itabidi uitishe mkutano wa wazazi wake na wako ili mujadili suala hilo. Ikiwa ameshikilia ya kwake basi ni bora kabisa kuachana naye.
Kwa kutumia maelekezo hayo tuna yakini kuwa mambo yatabadilika kwa njia nzuri. Nasi hapa tunakuombea kila la kheri na fanaka katika shughuli hiyo na Allaah ('Azza wa Jalla) Akupatie tawfiki.
Na Allaah Anajua zaidi