Mkwe Wangu Hataki Mtoto Wetu Aende Kwetu, Anamdhibiti Mume Wangu Kwa Kila Jambo

 

SWALI:

mimi ni msichana nilieoleowa mwaka tu uliopita.kinachonichangaza nikuwa ninapomuomba mumu wangu ruhusa ya kwenda pahali kama kwetu hanipi kama mamake amekataa.tumejaliwa kupata mtoto mmoja mamake mume hataki nende na mtoto kwetu kwa mamangu mzazi na anasema wazi sitaki mjukuu wangu aende huko na mume hanipi ruhusa ukiuliza sababu asema mamake hapendi nende na mtoto kwetu.Mume yuko safari akileta pesa mpaka zije kwa kakake zipite kwa mamake ndio nipewe ukimwambie akulete kivyako asema mama atakasirika.Je kijana wa kiume atakosa radhi kwa haya?je haya ndio mafundisho ya dini. shukran

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Haya ni katika matatizo mengi ambayo wanandoa wanakabiliwa katika ndoa zetu. Wakati mwingine mume anakabiliwa na tatizo kama hilo na wakati mwingine inakuwa ni mke mwenyewe kama ulivyotuelezea.

Hata hivyo, tumekuwa tukikariri mara nyingi kuwa matatizo kama haya yanatokea kwa sababu ya kutofuata maagizo ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika uchaguzi kabla ya ndoa. Inapokuja posa huwa hatutazami huyu mume yu hali gani na familia yake vipi? Je, unaingia katika familia ya Dini au la? Je, mume mwenyewe ameshika Dini na ana maadili mema au vipi? Kwa kutoangalia hayo ndio huwa tunaingia katika majanga na mitihani kama haya. Pia wanawake huwa hawaweki masharti yoyote yanayokubalika kisheria kabla ya ndoa ili kuidumisha ndoa hiyo.

Haya ni mafunzo ambayo wasichana na wazazi wanafaa wayatilie maanani kabla ya ndoa ili wasikabiliwe na matatizo kama hayo baadaye. Hakika ni kinyume na sheria ya Kiislamu kwa mume kumfuata mamake katika kumkataza mkewe kumzuru mamake pamoja na mtoto wake kwani hiyo ni haki ya mke na mume anafaa amkubalie mkewe kuwazuru wazazi wake. Mbali na kuwa mume mwenyewe anaweza kumkataza mkewe kwenda sehemu akihisi kuwa kwa kumruhusu huko kunaweza kuleta natija mbaya na ufisadi. Wakati kama huo ili kuondoa tatizo hilo mume mwenyewe anaweza kuwa anakwenda na mkewe katika nyumba ya mama mkwewe na kufanya hivyo kutaongeza mahusiano mema na mapenzi baina ya wanandoa.

Tatizo kama hilo linaweza kuondoka tu pale utakapozungumza na mumeo ana kwa ana kuhusu suala hilo kinaganaga ili mpate suluhisho la kudumu. Suluhisho moja ni kuweza kumshawishi mumeo muweze kuishi kando ki-vyenu kwani katika kuishi kama mnavyoishi inaweza kuleta matatizo zaidi kuliko kupata ufumbuzi. Hata hivyo, tumia hekima na maneno mazuri na matamu kumkinaisha mumeo kuhusu hilo. Ikiwa itashindikana kupata hilo basi watumie watu wengine kama mashaykh na watu wake wakaribu ambao anaweza kuwasikiliza kwa hali nzuri.

Haifai kumuudhi mama bali inafaa atiiwe katika mambo ambayo hayaendi kinyume na maagizo pamoja na maamrisho ya Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake. Kwa hiyo, mumeo anafaa azungumze na mamake na kumuelewesha wajibu wake kama mume kwa mkewe katika kufuata mafundisho ya Dini yaliyo mema na mazuri.

Tunakutakia kila la kheri na fanaka katika maisha yako ya ndoa. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akupatie ufumbuzi katika tatizo lako hilo ulilo nalo.

Na Allaah Anajua zaidi

Share