Mume Wangu Ananiadhiri Na Kunitisha Kunidhuru, Nifanyeje?

 

 

SWALI:

salam aleikum.nilikua nataka kuliza maswali yangu.mimi nimschana mdogo ambae sijafika miaka thalathini nina plomlem sana na mume wangu mambo mengi hata kusema siwezi na nimambo mengi mume wangu yuwanitendea kwaubaya nakunifikiria kwaubaya na matusi yandani nakuniazirisha kwawatu najaribu kustahamili kwa mda mrefusana kama miaka 7lakini kwasasa nimechoka namimi simtendei lolote analonifikiria niko nyumbani kama watu nimekaa.sasa mimi nauliza naweza kuomba talaka kwasababu ashaniambia aweza hata kunidhuru mda wowote na mimi naogopa nasijui nifanye nini.nimejaribu kuongea nae kumweleza lakini hasikii,sasa mimi naomba maoni kwenu nifanye nini.hata wazazi weke wanajua hata family yake mzima wamjua na mimi nimechoka hadi yamwisho nakaa nae lakini roho yangu iko mkononi najua any time aweza kunidhuru kwa njia ya kifo na wala hanijali wala hanioni kama mimi nimkewe nanimemzalia watoto.tafadhili mukipata barua yangu naomaba munijibu nipate kuyatatua.maasalam



 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu aliyeuliza swali hili la matatizo yanayopatikana katika unyumba. Matatizo ambayo yanapelekea kusambaratika kwa familia, hivyo watoto kupata shida. Tunakuombea kwa Allaah Aliyetukuka Akutoe na Akupatie njia muafaka ya kutoka katika janga hilo.

Mwanzo kabisa ningependa kukuelewesha kuwa katika Uislamu wewe si msichana mdogo kwani unapobaleghe tu huwa tayari umetoka katika utoto na kuingia katika utu uzima. Unapozungumzia kuhusu udogo na ukubwa katika sheria yetu tukufu ni kutobaleghe au kubaleghe. Msichana au mvulana anapobaleghe tu huwa amekuwa ni mukallaf (mwenye kuhitajia kutekelezea mambo yote ya Uislamu). Anapotekeleza hayo huwa anaandikiwa thawabu, na akikengeuka na kutenda mambo maovu basi huwa anaandikiwa dhambi. Kwa sasa wewe ni mama uliyepewa taklifu na wajibu mwingi wa Dini. Hivyo, ni juu yako kuyatekeleza hayo ili usiingie katika shimo hapa duniani na Kesho Akhera.

Hakika makosa mengi hutokea na kufanyika wakati wa posa na uchaguzi baina ya wanandoa. Mara nyingi huwa hatuchukulii uzito vigezo na nasiha akizopatia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hivyo kuja kujuta baadaye. Mazingira na malezi hucheza dauru muhimu katika ufanisi wa ndoa zetu. Hapa yaonyesha binti muuliza swali na wazazi walikosa katika uchaguzi.

Misingi aliotupatia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) haikufuatwa vilivyo mpaka imekufikisha katika janga kama hilo. Kwa hali nyingi mwanadamu anakosea na tunapokosa inafaa tujirudi na tujirekebishe ili tusiingie katika matatizo mengine. Msingi kemkemu tuliopewa wa kuchagua mume au mke ni:

Dini na Maadili: Huu ni ule ufahamu wa uhakika na wa kweli wa Uislamu na utekelezaji wake. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) anatueleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allaah Hatazami sura zenu na mali yenu lakini Anatazama mioyo yenu na amali zenu” (Muslim).

Hivyo, ikiwa msingi wa uchaguzi ni sura au mali huwa tunajiingiza katika balaa. Amesema tena Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mwanamke huolewa kwa mambo manne: Kwa mali yake, nasaba yake, uzuri wake na Dini yake. Chagua mwenye Dini …” (al-Bukhaariy na Muslim). 

 

Na mwanamme naye pia huchaguliwa au kukubaliwa kwa moja ya mambo haya manne. Ikiwa Dini haipo katika msingi wa uchaguzi basi ni hasara. Amesema tena Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Anapokujieni mnayemridhia Dini na maadili yake muozeni, kwani msipofanya hivyo kutakuwa na Fitna katika ardhi na uharibifu mkubwa” (at-Tirmidhiy).

 

Inaonyesha vipengele vya Dini na maadili havikutazamwa wala mwenye kuposa (mume) hakuchunguzwa na familia ya mke kwani kama hilo lingefanyika basi yangebainika hayo uliyoyasema. Pindi uhakika wake ungejulikana kuwa yeye ni mtu wa aina fulani asiyekuwa na maadili mazuri, uamuzi muafaka ungefanywa kwa urahisi kabisa. Inafaa kabla ya kujibu posa watu wa mume waulizie kuhusu Dini na tabia ya mke na vile vile watu wa mke. Na zipo njia nyingi za kutekeleza hilo kwa usahali. 

 

Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wameusia sana kuwatendea wema wake zetu na yule mume ambaye hatatekekeza hilo si mbora kati yetu. Amesema Akiyetukuka: “Tangamaneni nao kwa wema” (). 

 

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Nawausieni kheri juu ya wanawake” (al-Bukhaariy na Muslim). 

 

Amesema tena mtukufu wa daraja (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Waumini waliokuwa na Imani ni walio bora wa maadili, na mbora kati yenu ni aliye bora kwa wake zake” (at-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh). 

 

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema wale wanaowapiga wake zao si bora kati yetu: “Hakika wamezunguka wanawake wengi kwa nyumba za familia ya Muhammad wakishtakia waume zao, hao sio bora miongoni mwenu” (Abu Daawuud kwa Isnadi iliyo sahihi).

 

Uislamu una msingi unaosema hapana kudhulumu wala kukubali kudhulumiwa. Pia haifai kudhuru wala kulipana madhara. Muislamu anafaa atetee haki yake kwa njia na hali zote za halali, asikubali kudhulumiwa wala kudhuriwa naye asiwe ni mwenye kudhuru wala kudhulumu. Allaah Aliyetukuka Anasema katika Hadiyth al-Qudsiy: “Enyi waja wangu! Mimi Nimejiharamishia dhulma juu ya nafsi Yangu na Nikaifanya ni haramu baina yenu, basi msidhulumiane” (Muslim). 

 

Pia amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hakika damu zenu, mali na heshima yenu ni haramu baina yenu” (al-Bukhaariy, Muslim na Abu Daawuud).

 

Baada ya kutufahamisha kuhusu madhara ambayo yanaweza kukufikia ni vyema uchukue hatua ya haraka. Kwa sababu, familia ya mumeo wanajua tabia halisi ya mumeo, itisha kikao cha haraka baina yako, mumeo, wazazi wake (au wawakilishi wa upande) na wazazi wako kama Alivyotuamrisha Aliyetukuka. Anasema Aliyetukuka: “Mkihofia uhaini na utovu wa usalama baina ya wanandoa, basi chagua wasuluhishaji (mahakimu) wa upande wa mume na mke. Mkitaka mapatano na suluhuhisho Allaah Atawapatia tawfiki. Hakika Allaah ni Mjuzi na Mwenye hekima” (). 

Ikiwa ipo kheri ya nyinyi kubaki pamoja kwa amani, usalama na utulivu kutapatikana suluhisho kamili kabisa, la sivyo basi itakuwa kheri akupatie talaka kwa hiyari yake. Sababu ni kuwa Allaah Aliyetukuka Ameijaalia ndoa kuwa na mambo yafuatayo: “Na katika Ishara Zake ni kuwa Amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye Amejaalia mapenzi na huruma baina yenu” (30: 21).

Allaah Amejaalia mapenzi na huruma lakini unapokuwa usalama na uhai wako uko hatarini vitu hivyo viwili vinaondoka. Ikiwa imeshindana kupatikana natija yoyote kwa sababu moja au nyengine au mume hataki kutoa talaka itabidi uende kwa Qaadhi au Shaykh mwenye ikhlaasw au hata yule aliyewafungisha ndoa ikiwa ni muadilifu ili mumuelezee matatizo yenu.

 

Ikiwa sehemu unayoishi yupo Qaadhi, unaweza kwenda kwake ukamwelezea matatizo baina yako na mumeo. Yeye ana uwezo wa kutoa talaka ikiwa mume ni mkaidi na hataki kufanya na kutekeleza jambo hilo. Lakini tunatumai mtapata suluhisho katika kikao chenu hivyo hakutokuwa na haja ya kwenda mbele zaidi.

 

Sisi hapa tunakuombea na tunawaombea kila kheri na fanaka katika kusuluhisha tatizo lako hilo kubwa. Na tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akupatie na Akusahilishie lile la kheri … Aamiyn.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share