Mume Mzinifu, Haswali, Nilipokasirika Naye Kanitenga Nifanyeje?

SWALI:

 

Assalam Alaykum.

Mimi nina mume lakini ni mzinifu sana na nimeshamkuta na vidhibiti vingi vya kunijulisha kuwa anazini. Hasali wala si mcha Mungu. Kuna siku nimemjibu kwa hasira kuwa hata akiniingilia sisikii raha. Tangu siku hiyo hadi leo hajanigusa sasa ni mwezi mmoja na nusu. Nifanyeje nisitoke nje ya maadili?


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mume mzinifu. Hakika hili la waume kutochukua majukumu ni katika matatizo sugu katika jamii yetu. Tatizo linalopatikana ni kuwa wazazi na wanawake huwa hawajali sana kutazama na kumjua mume anayeoa. Lau kama tungekuwa tumefuata muongozo wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tatizo hilo halingepatikana kwani huyu mume haswali hivyo hata hiyo ndoa kukatika.

 

Jambo ambalo unaweza kufanya ni kumuuliza huyo mume kama bado anakutaka au kujitenga nawe ndio tayari amekupatia talaka. Ikiwa amekupatia talaka basi hiyo ni kheri kwako kwani utakuwa umejiepusha na shari kubwa ya kukaa na mzinzi na Taarikus Swalah. Ikiwa anasema kuwa wewe bado ni mkewe inatakiwa uende kwa Qaadhi umuelezee kuhusu hilo ili uachishwe kwani huyo si mume wa kukaa naye, kwa sababu kutokana na Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zinaonyesha wazi ukafiri wa mtu mwenye kuacha Swalah kwa makusudi na Ma'ulamaa wengi wameona kwamba kuishi na mtu asiyeswali japo kwa uvivu na hataki kujirekebisha haipasi na bora kujiepusha naye asije kuharibu Dini yako na ya watoto wako. Na mke anayo haki kudai talaka ikiwa mumewe hataki kuswali baada ya kupewa mawaidha na bado akashikilia ukaidi wa kutokuswali.

 

Ni vyema umtafute mwenye elimu na amfahamishe umuhimu wa kuswali na madhara yake, na atambue kwamba kutokutimiza nguzo hiyo kuu ya Kiislamu ni kukanusha amri za Allaah zilizo fardhi kwa kila Muislamu. Pia mpatie makala zilizomo katika kiungo kifuatacho zenye kuelezea umuhimu wa kufaridhishwa Swalah, fadhila zake na hukmu ya mwenye kuacha Swalah:

 

 

Swalah, Umuhimu Wake, Fadhila Na Hukmu Ya Mwenye Kuacha 

 

 

Ikiwa hatorudi kuswali na huku bado anakutaka basi huna budi kwenda kwa Qaadhi umtake akuachishe naye kwani huyo atakuwa sio mume mwenye kheri na wewe. 

 

Tunakuombea kila la kheri na mafanikio ya kujiepusha naye. Usiwe ni mwenye kutia wasiwasi kwani Allaah Aliyetukuka hatakuacha mkono na usaidizi Wake uko pamoja nawe.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share