Mume Kuchelewa Kurudi Nyumbani Kwa Ajili Ya Marafiki
Mume Kuchelewa Kurudi Nyumbani Kwa Ajili Ya Marafiki
SWALI:
ASALAM ALYKUM.NINA SUALA KUHUSU MUME WANGU,YEYE HUENDA KWA MARAFIKI SIKU YA WEEKEND NA HURUDI USIKU SANA NA MIMI SIPENDELEI JAMBO HILI, NIMEJARIBU KUMWELEZA LAKINI HUKASIRIKA SANA NA HUENDA ASIZUNGUMZE NA MIMI KWA SIKU TATU AU PIA KUNIGURA KITANDA NA MIMI SIPENDELEI KUTETA NAE NA TUNA WATOTO WATATU, JE UTANIPA NASAHA GANI?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Katika mambo muhimu katika Dini yetu ni uanandoa na jinsi kukaa pamoja baina ya wanandoa. Mara nyingi huwa tunakosea katika hilo na hivyo ndoa kuharibika na malezi ya watoto kuathirika. Na ndio katika hili Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akahimiza sana kuchaguana katika misingi ya Dini. Mume na mke ni kuvumiliana katika ile misukosuko ya maisha na hivyo inawabidi wawe na maadili ya Kiislamu kabambe ili waweze kushinda nguvu za shetani na wasaidizi wake. Wanadamu ni wanadamu na mara moja au nyingine hukosea au kukoseana na hili jambo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuelezea na halina budi kutokea, lakini mbora ni yule anayejirekebisha anapokosa au akamkosea mwenziwe.
Matatizo haya ya mume kumkosea mke au kinyume chake ni mengi na ikiwa hatutofuata Uislamu katika utatuzi wa hilo basi nyumba zitavurugika na kubomoka, na hivyo familia kuzorota.
Mume na mke wanatakiwa wakae kwa wema kama Alivyotuamrisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَعَاشِرُوهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۚ فَإِن كَرِهْتُمُوهُنَّ فَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَيَجْعَلَ اللَّـهُ فِيهِ خَيْرًا كَثِيرًا ﴿١٩﴾
Na kaeni nao kwa wema. Na mkiwachukia, basi asaa ikiwa mnachukia jambo na Allaah Akalijaalia kuwa lenye khayr nyingi [An-Nisaa 4: 19).
Katika Aayah hii anaambiwa mwanamme awe na uvumilivu kwa mkewe kwani yeye ndiye mwenye uwezo mkubwa wa talaka na hivyo haitakiwi aitumie vibaya. Lakini aya hii pia inamlenga mke asiwe ni mwenye kumchukia mume kwa ajili ya kosa ambalo linaweza kurekebishwa. Na hakuna kosa ambalo haliwezi kurekebishwa na hasa ikiwa watu hao wawili wana maingiliano ya kina na ndani zaidi, kama mume na mke.
Hivyo, tunaona ili kurekebisha tatizo hili dada yetu afanye yafuatayo na tunamuombea taufiki katika kusuluhisha huo mgogoro ambao ni mdogo lakini wenye uwezo wa kulipuka:
1. Nasiha:
Hili ni jambo muhimu na inatakiwa tuwe tunapendeleana mema na kuitoa kwa Ikhlasi. Jariyr bin ‘Abdillaahi (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Nilimbai Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kusimamisha Swalaah, kutoa Zakaah na kumnasihi kila Muislamu” [Al-Bukhaariy, Muslim, Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy].
Na ndio Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaifanya nasiha ndio kusimamisha Dini pale aliposema: “Dini ni nasiha” [Muslim, Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy kutoka kwa Abuu Ruqayyah Tamiym bin Aws Ad-Daariy Radhwiya Allaahu 'ahnu].
Nasiha inatakiwa iwe tofauti na fedheha, hivyo ifanywe kwa hekima, upole, maneno matamu na mawaidha yaliyo mazuri kwani hii pia ni da‘wah na njia hizo ni lazima zitumiwe. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ۚ
Lingania katika njia ya Rabb wako kwa hikmah na mawaidha mazuri. Na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi. [An-Nahl: 125]
Jaribu kuzungumza naye wakati ametulia na hana shughuli nyengine ambazo zinamtatiza na mke kawaida atajua wakati huo ili muweze kutatua tatizo hilo kwa njia iliyo nzuri. Ikiwa kwa kutumia njia hii hukufanikiwa basi fuata hatua ya pili.
2. Ushauri Nasaha:
Jaribu kutumia watu ambao wako karibu naye na ambao unawaamini ili waweze kuzungumza naye kuhusu hilo tatizo kwa njia ilio nzuri. Na Maimamu au masheikh huwa wanacheza dauru muhimu katika hili, kwani wao bila ya upendeleo wanaweza kutatua tatizo hili kwa uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) lakini uwe na tahadhari katika kuchagua maimamu kwani wengine hawana uzoefu na wanaweza kuongeza shida zako. Ikiwa hatua hii haikuleta natija basi fuata hatua ya tatu.
3. Suluhisho na sulhu kwa kuita wawakilishi katika upande wa mke na mume:
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametupatia mlango huu wakuweza kutatua matatizo ya ki-ndoa baina ya wanandoa. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ بَيْنِهِمَا فَابْعَثُوا حَكَمًا مِّنْ أَهْلِهِ وَحَكَمًا مِّنْ أَهْلِهَا إِن يُرِيدَا إِصْلَاحًا يُوَفِّقِ اللَّـهُ بَيْنَهُمَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا خَبِيرًا ﴿٣٥﴾
Na mkikhofu mafarikiano baina yao wawili, basi pelekeni mwamuzi kutoka watu wa mume na mwamuzi kutoka watu mke. Wakitaka sulhu Allaah Atawawafikisha baina yao. Hakika Allaah daima ni Mjuzi wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [An-Nisaa: 35]
Na hii ni njia ambayo bila shaka kutapatikana ufumbuzi lau kweli munataka suluhisho la tatizo hilo la kwenu na kuwaokoa watoto na shida za talaka.
Kwa hakika ni makosa kwa mume kumhama mkewe kwa sababu hiyo uliyoitaja na haifai kwake kutozungumza nawe hata ikiwa wewe ni mkosa. Haya ni mambo ambayo yamekatazwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), lakini ndiyo inatokea kwako, fanya subira na Allaahs Ataleta tawfiyq Yake baada ya kufanya juhudi.
Na Allaah Anajua zaidi.