Mke Mjeuri Juu Ya Kwamba Anapewa Raha Na Mahitajio Yote Na Mume

SWALI:

 

Ikiwa mwanamke amepewa raha zote na mahitajio yote nyumbani kwake lakini haachi kugombana na mumewe kila siku mpaka mumewe hawezi tena kukaa dakika moja nyumbani kwa sababu ya ulimi wake nipeni solution ya hili jambo.

 

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mume kumpatia mkewe mahitaji yote. Hata hivyo, hili ni suala ambalo limeletwa na upande mmoja na kisha maneno yenyewe yana utata kwani hukuelezea raha zote ni nini? Mara nyingi huwa tunachukulia kuwa raha anayohitaji mke ni kumpa chakula na kivazi kizuri, kinywaji na samani za nyumba pamoja na vifaa vyengine. Lakini kumpatia vitu hivyo huwa bado hujamuonyesha raha kwani mara nyengine mke mwenyewe alikuwa na zaidi ya hivyo nyumbani kwao alikotoka. Mara nyingi waume husahau hilo na hivyo kuingia katika matatizo ambayo hayana ufumbuzi aina yoyote ile. Mke kuja kwako huwa anahitajia kitu ambacho hawezi kupata kwa yeyote yule, si kwa babake wala kakake isipokuwa kwa mumewe. Jambo lenyewe ni jimai, na mume kushindwa kumpatia raha hiyo ni kutaka matatizo nyumbani au mke awe ni mwenye kuzini ili kupata hilo. Suali ni kuwa je, mume anampatia mkewe raha hiyo pia?

 

Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametupatia mafundisho kuhusu maingiliano baina ya mume na mke kwa jinsi ambayo mwenye kufanya kitendo hicho kwa halali anakuwa ni kama ametoa sadaka (Muslim).

 

Pia akatupatia muongozo kuwa asiende mtu kwa mkewe kama anavyofanya hivyo mnyama bali kuwe na mjumbe baina yao. Akaulizwa: Mjumbe ni nini, ewe Mtume wa Allaah? Akasema: Maneno matamu, busu, kukumbatiana na kushikana. Pia aliwakataza wanaume wasiwe ni wenye kumaliza mwanzo na kumuacha mke katika hali ngumu. Mume anafaa baada ya kummalizia mkewe afanye bidii asitoe uchi wake mpaka na mke naye atosheke na mengineyo.

 

Hakika ni kuwa wapo wake majeuri kama vile walivyo wanaume wengine katika hilo na zaidi ya hilo. Ujeuri hutokea ima kwa sababu ya malezi aliyepata mtu yeyote yule au kwa sababu ambayo wewe ndio umeisababisha. Jambo hilo hutokea kwa kuwa labda hatujawatendea wema kama alivyotuamrisha Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na kaeni nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkakichukia kitu, na Allaah Ametia kheri nyingi ndani yake” (4: 19). Huu ndio msimamo wa Uislamu huenda mke akawa mjeuri lakini ana mazuri mengine jaribu kumrekebisha kwa njia ambayo ni nzuri. Hata hivyo, tufahamu kuwa huenda mume akawa na makosa. Na ikiwa ni hivyo inabidi pia naye ajirekebishe ili waweze kufahamiana.

 

Ikiwa yote umefanya na kweli makosa ana mke nawe umejaribu uwezavyo jiwekee kuanzia sasa muda kwa kufanya yafuatayo:

 

  1. Zungumza naye tena kwa hekima na maneno matamu kuhusu tatizo hilo.

  2. Itisha kikao ikiwa hakujirekebisha baina yako, yeye, wazazi wako na wake (au wawakilishi wenu).

  3. Ikiwa hakujirekebisha basi mhame katika malazi.

  4. Ikiwa hakujirekebisha pia basi umeruhusiwa kumpiga kipigo ambacho hakimuumizi kama kwa leso kumfahamisha kuwa amefanya makosa.

  5. Ikiwa hakujirekebisha basi peleka kesi yako kwa Qaadhi au Shaykh mwadilifu.

  6. Ikiwa bado yuko vile vile basi itabidi labda muachane ili musiendelee na matatizo hayo. Kwa kufanya hivyo, huenda yeye akapata mume watakaosikilizana na kupata mke mtakayeridhiana.

 

Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

Basi wanawake wema ni wale wenye kutii na wanaojilinda hata katika siri kwa kuwa Allaah Ameamrisha wajilinde. Na ambao mnachelea kutoka katika utiifu wanasihini, muwahame katika malazi na wapigeni. Wakikutiini msiwatafutie njia ya kuwaudhi bure” (4: 34).

 

Na Allaah Anajua Zaidi

 

 

 

Share