Mume Wangu Anazungumza Na Mwanamke Asiye Mahram Wake, Nikimkataza Anasema Niache Wivu
SWALI:
asalam alaykum, nina suala kuhusu mume wangu yeye yuwazungumza na mwanamke na nikimuambiya si vizuri yuwakasirika mimi sipendelei kwa sababu mwanamke huyo huyo alikuwa akipiga simu siku za nyuma na akizungumza nae karibu nusu saa, na sasa wakionana mpaka wasimame wazungumze,mimi nishamueleza mume wangu kua sipendi lakini hasikii ameniambia nina wivu, najua kua afanyavyo si sawa kwani mimi mwenyewe najiweka mbali sana na wanaume wala sipendi kuzungumza nao, naomba munieleze ni kweli mimi nina wivu ama maoni yangu ni sawa, pia naomba mumpe nasaha mume wangu kwa sababu hii e-mail mukinijibu nitamuonesha kwa sababu hapa niliko sijui nimfate nani azungumze nae inshaalah nitafurahi mukinijibu mapema.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mumeo kuzungumza na mwanamke asiye Mahram yake.
Hili ni suala muhimu katika Dini yetu ambayo imeweka mpangilio na nidhamu katika kila jambo.
Hakuna jambo lolote isipokuwa limeelezwa kinaganaga. Allaah Aliyetukuka anatuambia:
“Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote. Kisha kwa Mola wao Mlezi watakusanywa” (6: 38).
Huo wako wa kumkataza mumeo kutoingia katika haramu ni kumkinga yeye na Moto wa Siku ya Qiyaamah na ni ulinganizi kwake. Nawe kwa kufanya hivyo unapata thawabu. Itabidi usichoke kumwambia mumeo na kumuelekeza kwani siku moja bila ya shaka ataongoka na kurudi katika njia ya sawa. Allaah Aliyetukuka Ametukataza kuikaribia zinaa
“Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya” (17: 32).
Ukaribiaji zinaa ni kuzungumza na mwanamke ambaye si Mahram wako, kutazama ambayo umekatazwa, kusikia ambayo hayafai kusikiwa na wewe
Tunakuombea kila la kheri katika juhudi zako hizo za kumsaidia na kumuokoa mumeo katika balaa hizo. Na bila shaka inshaAllaah utafanikiwa.
Na Allaah Anajua zaidi