Mume Mlevi, Anazini Mpaka Na Mayaya, Ananitukana Matusi Makubwa, Hakuna Mapenzi, Haswali: Na Anawazuia Watoto Wasiswali

SWALI:

Assalam Alaykum.

Mimi nina mume na watoto wanne Alhamdullilah nimeweza kumstahmilia tangu kanioa leo miaka kumi na nane.analewa lakini Alhamdulillah hatukua na shida yeyote.Ila tabia ya uzinifu nimeigundua na vidhibiti vingi vya kunijulisha kuwa anazini mpaka kwa mayaya wandani nimeamua kukaa bila yaya na mpaka rafiki zangu anawatongoza yaani ananiabisha sana, na ananitukana matusi makubwa makubwa mbele ya watoto nikiwaondoa watoto mbele yake anawazuia na kuhusu salaa watoto walivyokua wadogo walikua wanaswali sasa hivi nikiwahimiza kusali wananiambia unatupigia kelele sisi mbona baba hasali??

Ndugu zanguni naomba ushauri kuhusu hali hii sina raha katika ndoa yangu na wala hatuna mapenzi kabisa kila siku nikutafutiwa sababu ya kutukanwa na kusimangwa hata tendo la ndoa sina hamu naogopa asije kuniletea balaa inshaala ALLAH atuepushia .naomba ushauri ndugu zangu. NAMUOMBA ALLAH AKUZIDISHIENI ELIMU NA AWARAHISISHIE KAZI ZENU NA AKUINGIZENI LLJANA BILA HISABU ALLAHUMA AMEEN.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Tunashukuru kwa swali lako hilo.

Miongoni mwa subira ambazo tunatakiwa tumuombe Allaah Aturuzuku ni kumuomba Atupe subira kwa maasi; kwa maana Aturuzuku subira tusifanye maasi wala tusiyakaribie kwa tawfiki Yake Mola. Ndugu yetu kama unavyoeleza: ‘nimeweza kumstahmilia tangu kanioa leo miaka kumi na nane.analewa’ hakika hukuwa na subira bali ulikuwa na matatizo kuishi na mlevi bila ya kuweza kumbadilisha na kumsaidia kuweza kwa tawfiki Yake Mola kuacha kulewa na kuelewa kuwa ulevi ni katika maasi yenye kuelezewa kama ni mama wa maasi; kwani mwenye kulewa huwa mara nyingi yu mwenye uwezo wa kutekeleza na kufanya maasi yote yaliyosalia yakiwemo hayo ambayo umeyataja na kudai kuwa umeyagundua. Ndugu yetu kama unashukuru kuwa wakati akiwa analewa na kusema, ‘hatukua na shida yeyote’ kwa kweli unajidanganya kwani mlikuwa na shida tena kubwa na shida hiyo ni kuwa ulikuwa ukilea hayo ambayo sasa unayalalamikia; kwani mlevi huwa hana hayaa na hayaa ni katika iymaan katika Uislamu; hivyo mlevi huwa hana iymaan kwa kukosa hayaa na wewe ndie uliyemlea kuweza kufikia hivyo alivyo sasa; kwani kama ulikuwa na mapenzi naye basi ilikuwa ni katika uwezo wako kwa tawfiki yake Mola kuung’owa mzizi toka ulipopandikizwa au ulipopachikwa; lakini kama usemavyo kwa kuwa ulikuwa ukipata kila kitu ukaona kuwa ulevi wake haukushughulishi maadamu unapata fedha na hilo ndio muhimu na kufanya uyatakayo.  Kwani wakati mwengine mlevi huwa si mwenye akili yake na ukawa unachukuwa fursa hiyo, ndio ukawa huna shida. 

 

Ulevi ni mama wa maasi hivyo kama ulivyosema, ‘tabia ya uzinifu nimeigundua na vidhibiti vingi vya kunijulisha kuwa anazini’ hii tabia kwa hakika kama wesemavyo wenye kuelewa si kitu cha kuja mara moja bila shaka yoyote ile imeanza zamani na kama tulivyoeleza umeilea na sasa imekuwa na kipea. Hivyo chako ni kuchuma matunda yake kama ulivyokuwa mpaliliaji na mmwagilia maji na miongoni mwa matunda yake ni kama haya uliyoyataja, ‘kuwa anazini mpaka kwa mayaya wandani nimeamua kukaa bila yaya na mpaka rafiki zangu anawatongoza’ hivyo utaona ndugu yetu kuwa hapo hayaa haipo yawezekana yako zaidi ya hayo na huyaelewi na bora usiyaelewe kwani unaweza kupatwa na magonjwa yasiyosemeka Allaah Akuepusha mbali. Na yawezekana akawa anazini na wa karibu zaidi ya hao kama wako ndani ya nyumba hiyo wakiwemo watoto wako au wake mwenyewe.  Miongoni mwa starehe na vijana huita andisi za ulevi; kuwa walevi hupenda kuimba na kutokwa kwa makusudi maneno yasiyokuwa na maana yoyote kwa kuwa huwa wana kisingizio kuwa wakinywa ulevi akili huwa haipo na huwa hawajijui ndio wakawa wanakojoa ovyo kupita hata mbuzi na mbwa barabarani. Na kwa kuwa huwa hawana hayaa kama tulivyoeleza huwa katika nyimbo au maneno wayapendayo ni kama haya uliyoyaorodhesha, ‘ananitukana matusi makubwa makubwa’ kwa hiyo ndugu yetu lazima ufahamu kuwa hakuna matusi makubwa kwa asiye na hayaa wala hakuna heshima kwa asiye na hayaa wala asiye jiheshimu yeye mwenyewe; hivyo kuwepo kwa yeyote wakati wa furaha yake au wakati wa kuondosha kero zake kama wanavyodai huwa hakuwazuilia kitu; ndio akawa anakumiminia atakacho kama ulivyosema kuwa anatukana ‘mbele ya watoto nikiwaondoa watoto mbele yake anawazuia’

Na hayo ndiyo matunda ya ulevi.

 

Mlevi hategemewi kuswali na akiswali Swalah yake huwa ina mashaka kwani Quraan inasema:

 

“Enyi mlioamini! Msikaribie Swalah, hali mmelewa, mpaka myaelewe na myajue mnayoyasema, wala hali mna janaba -…” An-Nisaa: 43.

 

Allaah Ndiye mwenye uwezo wa kuongoa tena Humuongoa Amtakae, lakini sisi tunatakiwa tujitahidi kadiri ya uwezo wetu na katika kujitahidi ni kuwa sisi wazazi tunatakiwa tuwe ndio TV cha watoto wetu kwani wao huiga kila wanachokiona na sio kusikia tu. Hivyo kama sisi hatuswali na kuwataka wao waswali basi huwa hilo haliwezekani na kama mmoja katika familia haswali basi huwa ni famila kwani wao hakuna tofauti baina ya baba na mama kama ulivyosema kuwa sasa hivi nikiwahimiza kusali wananiambia unatupigia kelele sisi mbona baba hasali??

Ushauri wetu ni kuwa, jaribu kuzungumza naye kwa utulivu aache tabia hiyo mara moja na ikishindikana basi waite jamaa zako wa karibu na wa kwake ili muyazungumzie hayo na ikishindikana basi utakuwa wewe una uamuzi ima wa kwenda kwa wakuu wa Dini sehemu uliyoko kutafuta haki zako za kishari’ah.

 

Tunakuombea kila la kheri kwa hayo na Allaah Amuongoze huyo mumeo na arejee kuwa Muislamu mzuri atakayekuwa mfano kwa watoto wenu inshaAllaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share