Wakristo Wanauliza Kwanini Wanaume Wanaruhusiwa Kuoa Wake Wengi Na Wanawake Hawaruhusiwi?
Wakristo Wanauliza Kwanini Wanaume Wanaruhusiwa Kuoa Wake Wengi Na Wanawake Hawaruhusiwi?
Swali:
Swali hili nanukuu kutoka kwa wakristo wauliza kuwa sisi waislamu imeruhusiwa kisheria mwanaume wa kiislamu kuowa mke zaidi ya mmoja. Je, inaswihi mwanaume kufunga ndowa na wanawake 2-3 kwa siku moja? Natanguliza shukran zangu kwenu katika ujenzi wa Ummah.
Wabillah Tawfiiq
Jibu:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakika Muislamu anaruhusiwa kufunga ndoa sio tu siku moja bali wakati mmoja kwa wanawake wawili hadi wanne bila pingamizi wala tatizo lolote lile. Pia waeleze Wakristo waliokuuliza kuwa swali hilo pia ni sawa kwao nao wanaruhusiwa kufanya hivyo bila ya kuwa na pingamizi kutoka katika Biblia.
Hilo la kuoa wake wengi limepatikana kwa Manabii na wateule wa Allaah walioelezewa katika Biblia mfano wa Ibrahimu, Yakobo, Muwsaa, Suleimani na wengineo. Hakika ni kuwa Suleimani alikuwa na wake mia saba.
Ndoa imetajwa na kuhimizwa katika Biblia lakini hakuna hata msitari mmoja ambao unasema uke wenza haufai katika hii dunia. Bali Biblia inaashiria kuwa watu walio bora kama Manabii na Rusuli walikuwa na wake zaidi ya mmoja.
Katika kuwa katika uke wenza yapo masharti ambayo yanafaa kutimizwa. Biblia inatueleza hilo: "Ikiwa mwanamme fulani ana wake wawili naye anampenda mmoja kuliko mwingine. Nao wanawake hao wamemzalia watoto wa kiume, na mtoto wa kwanza kuzaliwa ni wa yule mama asiyempenda" (Kumbukumbu la Sheria 21: 15).
Biblia inatueleza kuwa Ibrahimu (Abramu) alikuwa na wake watatu kama tunavyoelezwa: "…na Sarai mkewe Abramu…" (Mwanzo 11: 31).
Tena: "Kisha, Sarai akampa Abramu Hagari, mtumwa wake wa kike, Mmisri, awe mke wake" (Mwanzo 16: 3).
Na pia: "Abrahamu alioa mke mwingine, jina lake Ketura" (Mwanzo 25: 1). Naye Ya'quub (Yakobo) alikuwa na wake wanne kama tunavyoarifiwa na Biblia: "Kisha Yakobo akamwambia Labani, 'Muda wangu umetimia, kwa hiyo nipe mke wangu'. … Lakini jioni, Labani akamchukua Lea, binti yake mkubwa, na kumpeleka kwa Yakobo. Yakobo akalala naye" (Mwanzo 29: 21 – 23).
Pia: "Na Yakobo alipomtimizia Lea siku zake saba, Labani akampa Raheli, binti yake mdogo awe mke wake" (Mwanzo 29: 28).
Tena: "Kwa hiyo Raheli akampa Yakobo mtumishi wake, Bilha, awe mkewe, naye akalala naye" (Mwanzo 30: 4).
Pia: "Lea alipoona ameacha kuzaa, alimtwaa Zilpa, mtumishi wake wa kike, na kumpa Yakobo ili awe mkewe" (Mwanzo 30: 9).
Biblia inatufahamisha tena kuwa kumbe anayefaa kuwa na mke mmoja ni askofu kumaanisha asiyekuwa askofu anaweza kuwa na zaidi ya mmoja. Hebu tusome: "Basi, askofu anapaswa kuwa mtu asiye na lawama; anapaswa awe na mke mmoja tu, awe mwenye kiasi, nidhamu na utaratibu" (1 Timotheo 3: 2). Hatujui kwa nini maaskofu wa Kikatoliki hawaruhusiwi kuoa kabisa?
Mwengine anayefaa kuwa na mke mmoja ni mzee wa Kanisa kama tunavyoarifiwa: "Mzee wa Kanisa anapaswa kuwa mtu asiye na hatia; aliye na mke mmoja tu, na watoto wake wanapaswa kuwa waumini" (Tito 1: 6).
Lakini pia inatakiwa katika Uislamu wanawake wanapoolewa wafanyiwe ihsani, watendewe wema na uadilifu. Hawafai kuwadhulumu na ikiwa huwezi kufanya hivyo unatakiwa uoe mwanamke mmoja pekee.
Ingia katika viuongo vifuatavyo kupata maelezo zaidi na hikma za wanaume kuruhusiwa kuoa zaidi wa mke mmoja:
Wanaume Kuoa Wake Wanne Na Wanawake Kuolewa Na Mume Mmoja
Na Allaah Anajua zaidi