Mwanamke Anayo Haki Kumzuia Mumewe Asioe Mke Zaidi Ya Mmoja?

 

SWALI:

Je? Nini hukumu ya mwanamke anayemzuia mume wake kuoa mke wa pili, ikiwa mume anauwezo wa kuwatosheleza wake wawili na zaidi, kwa kila kitu. Wabillahi taufiq



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu uke wenza na kuoa wake wengi. Inafahamika na kila mmoja kuwa sheria ya Uislamu imetungwa na Allaah Muumba wa kila kitu na mwenye kujua maumbile yetu. Sheria hiyo inakuwa ni maslahi kwetu hivyo tunapoacha kuifuata huwa tunaleta madhara kwa jamii.

Ni makosa tena sana kwa mwanamke aliyeolewa kumkataza mumewe kuoa mke wa pili hasa kama ana uwezo kama ulivyosema. Mwanamke anatakiwa amsahilishie mumewe katika suala hilo. Leo hekima ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kuweka sheria ya kuoa wake wengi inaonekana dhahiri shahiri kabisa katika ulimwengu.  

Hivi karibuni katika nchi ya Indonesia, wanawake wa Kiislamu walifanya maandamano kuonyesha na kudhihirisha ubora wa uke wenza. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wanne” (4: 3).

Utapata wenye shida hasa ya uke wenza ni Waislamu wenye kuishi katika mwambao wa Afrika Mashariki. Wenzetu wa Afrika Magharibi wako mbali hata hilo si tatizo kwani wake wenyewe ndio wenye kuwasaidia waume zao katika kupata mke wa pili na wa tatu.

 

Hivyo, mke anatakiwa amsaidie mumewe katika hilo na ujira wake kwa Allaah Aliyetukuka utakuwa mkubwa mbali na kumpatia mwenziwe fursa ya kuwa chini ya mume.

Bila kusahau kuwa na wanaume nao wajue kuwa hiyo ni rukhsa na ia masharti yake yaliyowekwa na Muumba, hivyo, wasiichukulie kama ni fursa ya kutekeleza uchu wao wa matamanio na kutokufanya uadilifu na kutekeleza haki kwa mke mmojawapo.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share