Mzee Wangu Ni Mlevi, Je, Naweza Kumtolea Fidia Asamehewe Madhambi Yake? Na Je, Naruhusiwa Kumpa Pesa Za Matumizi?

 

Mzee Wangu Ni Mlevi, Je, Naweza Kumtolea Fidia Asamehewe Madhambi Yake? Na Je, Naruhusiwa Kumpa Pesa Za Matumizi?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Sina budi kumshukuru Allaah S.W kwa kutujaalia uzima na afya njema na kutuwezesha kuufunga mwezi huu mtukufu wa Ramadhan; ninamuomba Allaah S.W yawe makubuli kwake matendo yetu yote mema tutakayoyafanya katika mwezi huu mtukufu. Na pia sina budi kumuomba yeye Allaah S.W kukujaalieni nyinyi ndugu zetu kila lenye kheir kwa kutufikishia mafundisho mema.  

 

Suala langu ni kama ifuatavyo:-

 

Mimi dada yenu nina umri wa miaka 35 hivi sasa; na tokea kupata fahamu kwangu baba yangu mzazi mpaka hivi sasa ninaandika maelezo haya basi hajaacha ulevi yaani tokea mimi sijazaliwa mpaka leo anaendelea na ulevi kiasi ya kwamba sisi watoto tumemaliza maneno kwa mzee wetu huyu awache maasi haya lakini wapi ataacha siku tu ambazo hana pesa lakini akipata tu kazi inaendelea. 

 

Suala lipo kama ifuatavyo:-

 

Kuna njia zozote za kufanya iwe kama fidia kwa mzee wetu huyu kutokana na hii hali ya kutokuacha ulevi?

 

Ikiwa mimi ndie ninaemshughulikia mzee wangu huyu je ninapaswa kumpa pesa za matumizi kama kawaida? kwani nikimpelekea pesa kidogo analalamika na nikimpelekea nyingi ndipo anazidi kulewa kwa hivyo nini nifanye kwa mzee wangu huyu? Ninaomba muongozo wenu ndugu zangu waislam na pia naomba dua zenu kwa wingi kwa ajili ya mzee wangu huyu ili awache mambo haya na aweze kushikamana na dini ya Allaah kikweli kweli. Ahsanteni.

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’aalaa) baada ya kumtaja Allaah, na andika (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Nabiy. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu.

 

Pili, tunashukuru kwa swali lako kuhusu mahusiano yako na baba yako. Hakika huo ni mtihani kwako na inafaa uwe na uvumilivu na natija ya hilo itakuwa nzuri. Endeleeni kuzungumza naye kwa wema, busara na njia nzuri kwani uovu haudumu milele hata ukichukua muda mrefu.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anatuhimiza kutumia hayo pale Alipotueleza:

 

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ۚ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ ۖ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ﴿١٢٥﴾

Lingania katika njia ya Rabb wako kwa hikmah na mawaidha mazuri. Na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi. Hakika Rabb wako Yeye Anamjua zaidi aliyepotea njia Yake, Naye Anawajua zaidi waliohidika. [An-Nahl: 125].

 

 

Katika madhambi anayofanya mja hakuna fidia kutoka kwa mtu mwengine hata akiwa ni binti yake na ni juu yake kubadilika na kutubia kwa kutimiza masharti yafuatayo:

 

1.Kujiondoa katika maasiya.

2. Kujuta kwa kufanya maasiya.

3. Kuazimia kutorudia tena katika hayo maasiya.

 

 

Wewe lako ni kila wakati kumuombea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Amsaidie kuacha. Kuna wakati ambamo du‘aa za mja zinakubaliwa kwa hivyo jitahidi sana katika nyakati hizo kumuombea kwa dhati na ikhlaasw. Nyakati zenyewe ni:

 

1). Wakati umefunga na hasa unapofungua wakati wa Magharibi.

2). Wakati wa usiku unapoamka kwa ajili ya Tahajjud.

3). Baina ya Adhana na Iqaamah.

4). Ukiwa safarini.

5). Siku ya Ijumaa nyakati za Alasiri hadi linapozama jua.

6). Pia wakati unaposwali ukiwa katika Sujuud na kabla ya kutoa Salaam.

 

 

Ili kumsaidia apunguze unywaji ni lazima umpunguzie masurufu unayompelekea wala isikutishe kupiga kwake kelele. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:

 

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿٢﴾

Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. Na Mcheni Allaah; hakika Allaah ni Mkali wa kuakibu. [Al-Maaidah: 2.]

 

 

Haifai kumsaidia mtu katika madhambi bali inafaa umsaidie katika kujirekebisha na hayo maovu.

 

 

Tufahamu kuwa baadhi ya Rusuli watukufu walipata matatizo makubwa zaidi kutoka kwa baba zao lakini wakavumilia na kuendelea kuwaheshimu katika mipaka ya Dini. Mmojawapo ni Nabiy Ibraahim (‘Alayhis-salaam) ambaye baba yake alikuwa ni mshirikina mkubwa sana naye akawa anamlingania. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anatupasha habari hiyo:

 

وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ إِبْرَاهِيمَ ۚ إِنَّهُ كَانَ صِدِّيقًا نَّبِيًّا ﴿٤١﴾إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ يَا أَبَتِ لِمَ تَعْبُدُ مَا لَا يَسْمَعُ وَلَا يُبْصِرُ وَلَا يُغْنِي عَنكَ شَيْئًا ﴿٤٢﴾يَا أَبَتِ إِنِّي قَدْ جَاءَنِي مِنَ الْعِلْمِ مَا لَمْ يَأْتِكَ فَاتَّبِعْنِي أَهْدِكَ صِرَاطًا سَوِيًّا ﴿٤٣﴾يَا أَبَتِ لَا تَعْبُدِ الشَّيْطَانَ ۖ إِنَّ الشَّيْطَانَ كَانَ لِلرَّحْمَـٰنِ عَصِيًّا ﴿٤٤﴾يَا أَبَتِ إِنِّي أَخَافُ أَن يَمَسَّكَ عَذَابٌ مِّنَ الرَّحْمَـٰنِ فَتَكُونَ لِلشَّيْطَانِ وَلِيًّا ﴿٤٥﴾قَالَ أَرَاغِبٌ أَنتَ عَنْ آلِهَتِي يَا إِبْرَاهِيمُ ۖ لَئِن لَّمْ تَنتَهِ لَأَرْجُمَنَّكَ ۖ وَاهْجُرْنِي مَلِيًّا ﴿٤٦﴾قَالَ سَلَامٌ عَلَيْكَ ۖ سَأَسْتَغْفِرُ لَكَ رَبِّي ۖ إِنَّهُ كَانَ بِي حَفِيًّا ﴿٤٧﴾وَأَعْتَزِلُكُمْ وَمَا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَأَدْعُو رَبِّي عَسَىٰ أَلَّا أَكُونَ بِدُعَاءِ رَبِّي شَقِيًّا ﴿٤٨﴾

Na mtaje katika Kitabu Ibraahiym. Hakika yeye alikuwa mkweli wa dhati, Nabiy. Pale alipomwambia baba yake: Ee baba yangu! Kwa nini unaabudu vile visivyosikia na visivyoona na visivyokufaa kitu chochote? Ee baba yangu! Hakika mimi imekwishanijia elimu isiyokufikia wewe; basi nifuate nikuongoze njia iliyonyooka. Ee baba yangu! Usimwabudu shaytwaan. Hakika shaytwaan kwa Ar-Rahmaan daima ni muasi. Ee baba yangu! Hakika mimi nakhofu kukushika adhabu kutoka kwa Ar-Rahmaan, utakuja kuwa rafiki kwa shaytwaan. Akasema: Unachukia waabudiwa wangu ee Ibraahiym? Usipokoma, bila shaka nitakupiga mawe; na niondokelee mbali kwa muda mrefu! (Ibraahiym) Akasema: Amani iwe juu yako. Nitakuombea maghfirah kwa Rabb wangu. Hakika Yeye daima kwangu ni Mwenye huruma sana. Na natengana nanyi na mnavyoviomba pasi na Allaah; na namuomba Rabb wangu asaa nisijekuwa kwa kumwomba Rabb wangu, mwenye kukosa baraka. [Maryam: 41 – 48].

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anatuekea mipaka katika kuwahudumikia wazazi wetu walioasi mbali na kuwa tunatakiwa tuwaheshimu. Anasema Aliyetukuka:

 

وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَىٰ وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ ﴿١٤﴾وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۖ وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا ۖ وَاتَّبِعْ سَبِيلَ مَنْ أَنَابَ إِلَيَّ ۚ ثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿١٥﴾

Na Tumemuusia insani kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameibeba mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa katika miaka mwili; ya kwamba, unishukuru Mimi, na wazazi wako; Kwangu ndio mahali pa kuishia. Lakini wakikushikilia kuwa Unishirikishe na ambayo huna elimu nayo, basi usiwatii. Na suhubiana nao kwa wema duniani, na fuata njia ya anayerudi kutubia Kwangu. Kisha Kwangu ndio marejeo yenu, na Nitakujulisheni yale mliyokuwa mkiyatenda. [Luqmaan: 14 – 15].

 

 

Tuko nawe katika kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Amuondolee baba yako na wazazi wa wengine wenye matatizo kama hayo. 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share