Hedhi: Kafara Ya Swawm Miezi Miwili Mfululuzo Itimizwe Vipi Na Mwanamke Mwenye Hedhi?
SWALI:
Kwanza napenda kuwashukuru ndugu wa Alhidaya kwakuweza kujibu maswali tupate kuzidi kuilimika swali langu nikuwa mtuakifanya zinaa au kufanya kitendo cha ndowa wakati wamchana wa ramadhani na mumewe,basi hukmu zao katika moja wapo 1 niwawache watumwa 2 walishe maskini 3 wafunge miezi miwili mfulululizo kila mmoja wao ikiwa mwanamke hakulazimishwa basi pia alipe lau amelazimishwa basi makosa anao bwana.
sasa kwa mwanamke ambaye amefanya makosa anatakiwa afunge miezi miwili mfululizo na mwanamke anapata heidh siku zake itakuwaje. naomba mtufahamishe zaidi. jazakalahu kheir
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atuepushe na kukutana na wake zetu mchana wa Ramadhaan seuze zinaa wakati huo. Ni madhambi makubwa zaidi kwa Muislamu kufanya kitendo hicho cha zinaa katika mwezi mtukufu wa Ramadhaan.
Tukija katika swali lako hilo ni kuwa mwanamke au mwanaume aliyefanya kitendo hicho wakati huo wa mchana wa Ramadhaan anatakiwa afanye kafara kwa kuacha mtumwa huru, ikiwa hawezi basi afunge miezi miwili mfululizo na ikiwa hawezi hilo jambo la pili basi alishe masikini sitini.
Tukija katika kipengele cha pili cha kafara, basi Muislamu huyo anafaa kufunga mfululizo miezi miwili. Ni hakika inayoeleweka kuwa wapo baadhi ya watu waliopewa nyudhuru hata ya kutofunga mwezi wa faradhi wa Ramadhaan akiwa katika hali Fulani. Miongoni mwa hali hizo ni safari, ugonjwa, kuwa katika damu ya hedhi au nifasi, uzee na nyinginezo. Hivyo, mfululizo hapa inamaanisha unafaa ufanye hilo na hufai kuacha bila udhuru wowote unaokubalika kisheria. Ikiwa umepatikana na udhuru wa kisheria wakati wa udhuru huo, mfano wa hedhi mwanamke hafai kufunga na hata akifunga haihesabiwi kuwa ni funga. Kwa hiyo, katika udhuru huo anafaa kutofunga na akiwa twahara ataendelea kufunga na hiyo itahesabika kuwa ni mfululizo kwani nia ni kuendelea lakini amepata udhuru wa kishari'yah.
Lile ambalo linakatazwa ni kuacha kufunga bila ya udhuru wowote wa kisheria. Anayefanya hivyo inabidi aanze tena kufunga kuanzia mwanzo tena.
Ingia katika viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi kuhusu Kafara hiyo:
Hukmu Ya Kutenda Kitendo Cha Jimai Mchana Wa Ramadhaan
Alifanya Jimai (Kitendo Cha Ndoa) Zaidi Ya Mara Moja Kwa Siku Moja Ya Ramadhaan
Je, Mke Anatakiwa Kulipa Kafara Ikiwa Alifanya Jimai (Kitendo Cha Ndoa) Na Mumewe Siku Za Ramadhaan?
Na Allaah Anajua zaidi