Mke Anadai Alipwe Chochote Kabla Ya Tendo La Ndoa

 

SWALI:

Mke anadai alipwe chochote kabla ya tendo la ndoa. Nini hukmu yake.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Hili ni suala la ajabu sana kwa Muislamu kuuliza kwani hili ni jambo ambalo linafaa kujulikana na hasa wanandoa. Inafaa Waislamu wanaume na wanawake kabla ya kuingia katika ndoa wawe watalelewa kwa kufundishwa majukumu na wajibu wao ili wasipate matatizo au shida wanapoanza kuishi pamoja baada ya nikaha.

 

Mke ana wajibu wa kumtimizia mumewe tendo la ndoa pindi mume anapohitajia. Na ni makosa makubwa kwa mke kukataa kumtimizia mumewe suala hilo au kutaka pesa kwa ajili hiyo. Mke yeyote atakayekataa kumtimizia mumewe tendo la ndoa akalala huku amemkasirikia, basi Allaah Aliyetukuka Anamkasiria mke huyo mpaka mume atakapokuwa radhi naye.

Anasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Mume atakapomwita mkewe kitandani na akikataa mke, basi Malaika watakuwa wanamlaani huyo mke mpaka asubuhi” Imepokewa na   Imaam Al-Bukhaariy

Madai hayo ya ajabu ya mke kwa mumewe hayana tofauti kubwa sana na mtu anayefanya biashara ya mwili wake. Ikiwa tayari mwanamke keshapewa mahari, anagharamiwa mahitaji yote ya nyumbani kwake, anavishwa, analishwa na isitoshe anapewa matumizi mbalimbali kama pesa ya mfukoni, bado tena madai hayo ni ya nini kwa mwanamke wa Kiislam?

Hata hivyo, wanaume nao wasitoe upenyo wa kusababisha hayo kwa kuwanyima wanawake matumizi ya muhimu na pia kuwapa pesa za mfukoni kwa mahitaji yao mengine wanayotaka wao maadam si mahitaji mabaya au yasiyoendana kinyume na sheria.

Hivyo, mke huyo anatakiwa anasihiwe na afundishwe ya Dini kwani huenda akawa hajui hayo. Lau atakuwa anajua hilo lakini anafanya makusudi basi atakuwa anachuma madhambi mengi kwa kitendo chake hicho na atakuwa hatimizi haki za mume zipasavyo kutimizwa.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share