Msafiri Anatakiwa Aswali Vipi Nyuma Ya Imaam Mkaazi?

 

SWALI:

mimi ni mkaazi wa Pemba nipo Dar kwa masomo ya muda wa mwaka mmoja. Je! Inakubalika kufupisha sala? Kama ni sawa inakubalika, vipi nitaisali sala ya Adhuhuri niliyoniwia kuichelewesha na kuisali wakati wa Alasiri kwasababu ya kuwemo darasani wakati wa Adhuhuri. ikiwa kuna uwezekano nipe taratibu za Sala ya safari hususan kwa wakati wa magharibi na siku ya Ijumaa. Na vipi nitasali nyuma ya Imamu mkaazi nami nafupisha Sala? Je! Rakaa mbili za ziada kutoka kwa Imamu mkaazi kwangu mie itakuwa ni sunna au vipi?

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Tufahamu kuwa Swalah ya safari ina masharti yake ili kuweza kutekezwa na msafiri anapokuwa katika safari au sehemu aliyoshukia kutoka mji wake. Kwa jinsi ulivyoeleza ni kuwa wewe ni mkaazi wa Pemba lakini umekwenda Dar kwa ajili ya masomo. Swalah ya safari inafanyika kwa muda fulani (siku zikiwa nyingi ni 18) kwa riwaya moja kutegemea wingi wa siku alizokaa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa Taabuuk na pia Makkah. Zaidi ya siku hizo huwa huhesabiki kisheria kuwa wewe ni msafiri bali unachukuliwa kuwa umekuwa mkaazi katika sehemu hiyo uliyopo wakati huo ukiwa katika masomo au shughuli nyingine yoyote ile. Ingawa Maulamaa na Maimaam wengi wamesema ni bora isizidi siku nne.

Kulingana na maelezo yako ni kuwa ulijua ulipokuwa unakwenda Dar kuwa utakaa mwaka mzima kwa masomo, hivyo kukutoa katika istilahi ya mgeni au msafiri. Kwa hiyo, inabidi wewe uswali Swalah kamili kwa wakati wake maalumu uliowekwa na sheria bila kukosa.

Kwa minajili hiyo inafaa wakati wa Swalah ya Adhuhuri utoke darasani na upate mahali pa kuswali. Swalah kwa Muislamu ni sahali sana kwani sheria imempatia nafasi ya kuswali sehemu yoyote katika ulimwengu isipokuwa anapoona najisi katika sehemu anayotaka kuswali.

Ama kwa msafiri wa kweli, Swalah zinaweza kuunganishwa na kupunguzwa. Unaweza kuswali Swalah ya Adhuhuri na Alasiri wakati wa Adhuhuri au Alasiri rakaa mbili mbili ukitoa salamu baada ya kila Swalah. Ama Swalah ya Maghrib na Ishaa pia zinaweza kuchanganywa kwa kuswaliwa wakati wa Maghrib au Ishaa, Maghrib ikibaki rakaa tatu na Ishaa rakaa mbili.

Ikiwa msafiri anaswali nyuma ya Imaam ambaye ni mkaazi, msafiri anafaa akamilishe Swalah kwa kumfuata Imaam kwa ukamilifu wake. Anapomaliza na Imaam Swalah hiyo ndio anaweza kuswali Swalah nyingine inayofuata kwa kupunguza.

Soma zaidi kuhusu masuala ya Swalah ya msafiri hapa:

Swalah Ya Safari Ya Mtu Anayeishi Katika Nchi Muda Mrefu

Na Allaah anajua zaidi

 

 

Share