Swalah Ya Mgonjwa

SWALI

Jamaa anauliza,

Mumewe Mtu mzima hajiwezi, kila kitu lazima asaidiwe, imefika hatuwa hata kula alishwe, lakini anafahamu sala na anasali na Qur’an anasoma kama kawaida.

 Sala ya asubuhi mkewe hawezi kumuinua mumewe na
kumpeleka chooni (hapa anakuwa lazima asafishwe sawa sawa) maana bwana huyu anavalishwa hafadha, kwa ajili haja ndogo au hala nyinginezo na wasaidizi wa mke hujitokeza mnamo saa 06:30 -07:00am. Kwa sababu ya udhru kama huu sala ya Asubuhi kila siku husaliwa saa 08:00 – 09:00am.

 Sala ya Adhuhuri na Alasiri hujamiishwa na Sala ya magharibi na Ishaa hujamiishwa kwa sababu ya udhru zilizo tajwa hapo juu.  Jee nini hukmu yake? 

Thafadhali sana tunaomba Suala hili lichambuliwe kwa inavyo wezekana.  Maana huyu mwenzetu alikuwa swala zake tano msikitini na leo Allah Subhana Wata’Allah kamkirim kwa hala alokuwa nayo.  Nasisi hii ni mafundisho kwetu  hatujuwi nani atakae kukirimiwa na Allah kama hivi au zaidi.  Namuomba Allah Subhana Wa Taala ampe shifaa huyu bwana na akitupa sisi mtihani kama huu tuweze kuchukuwa Amin!!.

 

 


JIBU:

Kwanza, kabisa AL HIDAAYA inamuombea mgonjwa huyu kwa Allaah سبحانه وتعالى   Amuondoshee maradhi aliyonayo na ampe uzima na afya kamili kisha Amlinde na kila maradhi pamoja na wagonjwa wote wa Kiislamu

Pili, tazama Du'aa zilizothibiti katika Sunnah kama zilivyo katika kitabu cha 'Hisnul-Muslim' ambacho kimo katika Tovuti hii ya AL HIDAAYA, ziko za kusoma mwenyewe mgonjwa na ziko za kumsomea.    

Tatu, tunampa bishara njema zifuatazo mgonjwa mwenye kusubiri kwamba:

1)      Maradhi ni katika mitihani Aliyokwishaandikiwa binaadam na kila anaposhukuru na kusubiri hulipwa thawabu bila ya hesabu kama Alivyosema Allaah سبحانه وتعالى  

}}إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ{{

{{Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu}}

Az-Zumar:10

2)      Masaibu haya ya maradhi yaliyompata mgonjwa huwa ni kusafishwa na madhambi na kughufuriwa kwake kama tunavyona katika kauli ifuatayo ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم .

 ((عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه أنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وآله وسلم: مَا يُصِيبُ الْمُسْلِمَ مِنْ نَصَبٍ وَلا وَصَبٍ وَلا هَمٍّ وَلا حُزْنٍ وَلا أَذًى وَلا غَمٍّ حَتَّى الشَّوْكَةِ يُشَاكُهَا إِلا كَفَّرَ اللَّهُ بِهَا مِنْ خَطَايَاهُ ))  رواه البخاري   

 ((Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه   kwamba, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: Muislamu hafikiwi na tabu wala machovu, wala hamu wala huzuni wala madhara, wala dhiki hata mwiba ukimchoma ila Allaah سبحانه وتعالى  Humfutia makosa yake))  Al-Bukhari 

3)       Maadamu alikuwa akitimiza ibada yake kwa ukamilifu wakati alipokuwa mzima, basi malipo ya ibada yake wakati mgonjwa huwa ni vile vile bila ya kupunguka kitu.

)) قول النبي صلى الله عليه وآله وسلم : "  إذا مَرِضَ العبدُ أو سافرَ كُتِبَ له مثلُ ما كان يعملُ صحيحاً مقيماً ))  البخاري

((Kauli ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم : Mja akiumwa au akisafiri, huandikiwa thawabu kama vile alivyokuwa akifanya alivyokuwa mzima au wakati hayuko safarini)) Al-Bukhari

 Hadiyth nyengine inayompa bishara njema  mgonjwa:

((عن عبدالله بن عمرو عن النبي صلى الله عليه وآله وسلم :   ما من أحد من الناس يصاب بالبلاء في جسده إلا أمر الله عز وجل الملائكة الذين يحفظونه ، فقال : اكتبوا لعبدي كل يوم وليلة ما كان يعمل من خير ما كان في وثاقي (( مسند أحمد

((Imetoka kwa 'Abdullahi Bin 'Umar kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  kasema: "Hakuna mtu atakayefikwa na masaibu katika mwili wake ila Allaah سبحانه وتعالى Huamrisha malaika wanaomhifadhi kuwaambia, muandikieni  (malipo) mja wangu kila mchana na usiku kwa yale  aliyokuwa akiyafanya  ya kheri kwa  muda   aliokuwa katika hali hii))  Mapokezi  ya Ahmad

Majibu kuhusu kuswali kwake kwanza tujue kwamba  Allaah سبحانه وتعالى   Ametuambia  kufanya ibada   kwa kadiri ya uwezo uwetu.  

}}فَاتَّقُوا اللَّهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ{{

{{Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo}}

At-Taghaabun:16

Kama hakuna njia yoyote iwezekanayo kupatikana mtu wa kumsaidia mkewe kumsafisha huyo mgonjwa wakati inaingia alfajiri baada ya jitihada kufanyika hadi wakati alfajiri itakapoingia, basi ataingia katika ile hukumu ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  aliposema : Ambaye imempita Swalah kwa kulala au kusahau basi aiswali atakapoamka au kukumbuka kama ilivyo katika Hadiyth ifuatayo:

  ‏(( ‏عن ‏ ‏أنس بن مالك ‏ ‏قال: ‏قال نبي الله ‏‏ صلى الله عليه وسلم ‏ ‏من نسي صلاة أو نام عنها فكفارتها أن يصليها إذا ذكرها))  رواه مسلم

((Imetoka kwa Anas bin Maalik ambaye alisema, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  amesema: "Atakayepitiwa na Swalah (kwa kulala) au kwa kusahau  basi aswali atakapokumbuka")) Muslim

Vile vile  kuhusu  kuchanganya Swalah ya Adhuhuri kuswaliwa pamoja na Alasiri na kuchanganywa Magharibi na 'Ishaa hakuna neno kufanya hivyo kutokana na udhuru aliokuwa nao mgonjwa kwani dini yetu haina mashaka kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى 

 }}  وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ{{

{{Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini}}. Al-Hajj: 78

 Wala Allaah سبحانه وتعالى Hakumkalifisha mwanadamu jambo ambalo haliwezi. 

}}لاَ يُكَلِّفُ اللّهُ نَفْسًا إِلاَّ وُسْعَهَا لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ{{

{{Allah haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo. Faida ya iliyoyachuma ni yake, na hasara ya iliyoyachuma ni juu yake pia”}} Al-Baqarah: 286

Na kuswali kwake pia mgonjwa aswali kwa kadiri anavyoweza kama hawezi kwa kusimama basi akae, na kama hawezi kukaa basi hata kwa kulala kama ilivyokuja ruhusa katika Hadiyth ifuatayo:    

)) وعَنْ عِمْرَانَ بْنِ حُصَيْنٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ : كَانَتْ بِي بَوَاسِيرُ ، فَسَأَلْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وآله وَسَلَّمَ عَنْ الصَّلاةِ ، فَقَالَ : صَلِّ قَائِمًا ، فَإِنْ لَمْ تَسْتَطِعْ فَقَاعِدًا ، فَإِنْ لَمْ تَسْتَطِعْ فَعَلَى جَنْبٍ (( رواه البخاري

((Kutoka kwa 'Imraan bin Huswayn رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ ambaye kasema: Nilikuwa (naumwa) na bawasiir nikamuuliza Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  kuhusu Swalah akasema; Swali kwa kusimama, ukiwa huwezi basi kwa kukaa, ikiwa huwezi basi kwa kulala))  Al-Bukhari

Tafadhali soma  Swali na Jibu lake la 'Kuswali Kwa Kukaa' kwenye kitengo cha 'Swalah' ndani ya tovuti hii upate maelezo na faida zaidi kuhusu Swala yenye udhuru kama hali ya huyu mgonjwa ilivyo.

Wa Allaahu A'aalam

 

Share