Amesafiri Muda Mdogo Kabla Ya ‘Alasiri Akafika Aendako Wakati Wa ‘Ishaa, Je, Ataswali ‘Alasiri Na Magharibi Vipi?

SWALI:

 

 

A Alaikum,

Natuma u buheri wa afya sheikh naomba kidogo nisaidiwe katika hili la swala ya safari, kwa uelewa wangu mdogo ninafahamu unaweza kuchanganya adhuhur na alaasir, magharib na isha, swali langu je kama niliswali swala ya adhuhur kwa jamaa punde kabla ya swala ya alaasir nikapata safari ambayo umbali wake nikafika niendapo wakati wa swala ya isha, je katika hili niswali jamaa ya isha alaf nilipe alaasir na magharib au nisiswali jamaa ili niswali safari kwa kuchanganya magharib na isha kama ni hivyo vipi kuhusu ile swala ya alaasir nayo nitanuia na swali safari au inakuaje, hilo ndo swali langu sheikh,

 

Wabilah Taufiq


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kufupisha kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kufupisha kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu Swalah ya safari.

Ama kuhusu swali lako hakuna utata wowote isipokuwa katika Swalah ya Alasiri. Haifai kabisa kwa Muislamu kutoa wakati wa Swalah moja isipokuwa katika safari ambayo ameruhusiwa kuchanganya kwa kuswali kwa kutanguliza au kuchelewesha. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema: “Kwa hakika Swalah kwa Waumini ni faradhi iliyowekewa nyakati makhsusi” (4: 103).

 

Tukija katika swali lako ilikuwa haifai kuiswali Swalah ya Alasiri wakati wa ‘Ishaa bali ilikuwa uombe gari lisimamishwe na ukaswali, kama ambavyo wanaweza kusimamishiwa mabasi wale wanaotaka kujisaidia bila shaka unaweza kusimamishiwa na wewe. Na kama ikishindikana basi au gari kusimama, basi uiswali ndani ya gari ikiwa unaelekea katika sehemu unayokwenda. Ikiwa hukuwa na wudhuu wakati wa safari na hamkusimama mahali ambapo unaweza kuchukua wudhuu unaweza kutayamamu na kuswali kwa kuketi. Ama Swalah ya Magharibi na ‘Ishaa utaziswali unapofika unakokwenda kwa kuswali Swalah hizo kwa kuakhirisha (kuchelewesha) kwa pamoja zote mbili, Utaadhini na kuswali Swalah ya Magharibi rakaa tatu na kisha utaqimu na kuswali Swalah ya ‘Ishaa rakaa mbili badala ya nne kwa sababu wewe ni msafiri.

 

Soma majibu yafuatayo upate maelezo zaidi:

 

Swalah Mwenye Kusafiri Mara Kwa Mara

 

Swalah Safari Katika Matreni Na Mabasi

 

Kukidhi Swalah Ya Safari Na Namna Ya Kunuia

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share