Swalah Safari Katika Matreni Na Mabasi


SWALI:

Kwanza ningependa kuwapongeza na kuwapa shukurani kwa kazi nzuri mulofanya kuweka site hii, mungu atujaalie tuwe wenye kuyafuata mafunzo ya Mtume Muhammad (S.A.W). Ni site yenye kutafanya kua naraha kuona mipango kama haya. Ahsanteni na Mungu awajaze Inshaallah.

Suali langu ndugu ni kua sielewi ni vipi, mimi naishi london na mara kwa mara huona watu wanaswali kwa kukaa kwenye matrain na mabasi, naelewa kua labda hawatki kupitwa na wakati lakini inasihi au kuna mpango mwengine?

kisha mimi nafanya kazi kidogo mbali na ninapo ishi tusema dakika 45 kwa train ambapo kwa hakika si mbali na kuna wahindi kazini wananiambia mimi ni swali swala ya msafir, mimi nimekataa na mpango huyo tuna sehemu ya kuswali kazini hakuna shida ila ningependa munielzee kuhusu hizi hoja mbili na Mungu atawabariki.

 Shukraan,

 


 

JIBU: 

AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Shukran ndugu yetu kwa swali lako zuri na tunaomba tawkifi kutoka kwa Mola wetu Mlezi katika kuiona haki katika hilo.

Ni muhimu kwanza tuelewe kuwa Swalah zote zimekewa wakati maalumu. Nazo zinafaa kuswaliwa katika nyakati zake hizo na haifai kuchelewesha Swalah yoyote ile ila kwa nyudhuru zinazokubalika kisheria. Allah Aliyetukuka Anasema: “Kwani hakika Swalah kwa Waumini ni faradhi iliyowekewa nyakati maalumu” (4: 103).

Hivyo, ikiwa upo safarini na unaogopa huenda ukakosa Swalah kwa wakati wake muafaka na wa sawa basi unaweza kuswali sehemu yoyote ile kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ardhi yote imefanywa kwa Ummah wangu kuwa msikiti na twahara. Hivyo, inapomkuta mmoja wenu Swalah basi aswali”. Swalah ya faradhi ni lazima iswaliwe kwa kusimama kwa mwenye uwezo wa kusimama lakini ikiwa hawezi au haiwezekani kwa ile sehemu anayoswalia au kwa dharura inayokubalika kisheria anaweza kuswali kwa kukaa au kwa kulala. Kwa hiyo, ukiwa ndani ya basi au gari la moshi na wakati umefika inafaa uswali kabla ya muda haujatoka. Mpango huu unaswihi na hauna tatizo lolote na usahali wa kutekelezwa. Usimwache shetani kukuchezea katika hilo mpaka ukawa labda unatoa Swalah kwa wakati wake.

Hakika hatujakupata vizuri uliposema mimi nafanya kazi kidogo mbali kisha ukasema kwa hakika si mbali. Je, sehemu unayofanya kazi ni mbali au si mbali? Kwa kila hali tuliache swali hilo kwani huenda likajibika katika maelezo. Ikiwa kutakuwa na utata unaweza kuuliza tena katika vipengele hivyo.

 Bila shaka inaeleweka kuwa Swalah ya Qasr (kupunguza) na kukusanya kama Adhuhuri na Alasiri na Maghrib na Ishaa imethubutu kisheria pale aliposema Allah Aliyetukuka: “Na mnapo safiri katika nchi si vibaya kwenu kama mkifupisha Swalah” (4: 101). Na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoulizwa kuhusu Swalah hiyo akasema: “Ni sadaka aliyokuleteeni Allaah, basi ipokeeni sadaka Yake” (Muslim, Abuu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah). Na amesema tena (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hii ni neema ya Allah kwenu, basi ipokeeni kwa shukrani” (al-Bukhaariy na Muslim).

Kudumu kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya Qasr kunaifanya iwe Sunnah iliyotiliwa mkazo au hata wajibu kwa kauli yenye nguvu pia. Na Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) nao walifuata mwenendo huo.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuweka kiwango cha umbali anaokomea mtu kupunguza Swalah. Hivyo, kutofautiana wanazuoni katika hilo. Baadhi wakaona kuwa ni maili 48 na wengine 56. Ama kuhusu umbali huo ipo Hadithi ya Shu‘bah kutoka kwa Yahya bin al-Hinaiy anayehadithia: “Nilimuuliza Anas kuhusu kupunguza Swalah naye akasema: ‘Mtume wa Allah, alipokwenda maili 3 (si maili hizi za sasa) au parasang 3 (parasang 1 ni sawa na maili 3.25) alikuwa akiswali rakaa mbili” (Muslim).

Safari hiyo inafaa iwe ni ya kheri na si ile safari ya maasi. Msafiri hafai kupunguza Swalah mpaka atoke nje ya mji, vitongoji na mabustani yake yakiwa nyuma yake kabisa.

Hakuna tofauti katika Sunnah ya Qasr kati ya msafiri aliyepanda kipandwa, au anayekwenda kwa miguu, au aliyepanda farasi na punda, au gari au ndege wala muda utakaotumika, kinachotizamwa ni tendo la safari. Mtu mwenyewe ni muelewa kwa kitendo hicho kuwa ni safari au la.

Ikiwa msafiri atanuia kukaa katika mji zaidi ya siku nne kwa kauli maarufu zaidi, basi itamlazimu atimize Swalah na asipunguze kwani kwa kutia nia ya kukaa akili yake itatulia na atafanya mambo yake kwa utulivu. Ama zikizidi hizo siku kwa dharura, basi ataendelea kufupisha hadi dharura yake itakapokwisha kwa ima kurejea au kuweka makazi yake hapo ya kudumu.

Hivyo unatakiwa ujitahidi uwezavyo uswali kazini maadam umesema iko nafasi ya kufanya hivyo na haifai kuswali safari na hali bado upo katika maeneo ya mjini kwako. Ama kuunganisha Swalah kwa kuziswali kikamilifu, yaani Adhuhuri nne na Alasiri nne kwa wakati wa Adhuhuri au kuziswali zote kwa wakati wa Alasiri, inaruhusiwa kwa dharura. Na bila shaka hii ndio inahusiana na suala lako zaidi kuliko Swalah ya safari.

Ama hao waliokushauri kuswali safari kazini na hali bado upo ndani ya mji wako, basi ni vyema kama ungewaomba dalili kuhusiana na hilo.

Pia tunakushauri badala ya kutumia ‘Kuna Wahindi kazini wameniambia…’ bora utumie neno ‘ndugu zangu wa kutoka India, au ndugu zangu kutoka Bara Hindi au Asia wameniambia…’, kutumia lugha kama hivyo kunaleta migawanyiko na chuki baina ya Waislam. Haifai na haipendezi kusema, ‘wabara wanasema kadhaa…’ au ‘wazanzibari wanasema kadhaa’ au ‘yule mbara’, au ‘yule mzanzibari’. ‘yule mpemba’…n.k. Hizo ni lugha zisizofaa kwa Waislam kuzitumia na hazijengi mapenzi baina ta Waislam.

Na Allah Anajua zaidi

 

Share