Mshia Anatushawishi Tuache Kuswali Mara Tano Na Tuswali Mara Tatu Tu Kwa Siku, Je, Nini Hukmu Yake?

 

SWALI:

 

Kuna mtu hapa Scotland anajulikana kama *** ***** anasumbua sana watu na hasa sisi tusio na elimu kubwa, ana mengi ya ajabu, mara utamsikia  akidai kuwa Nabii Isa (as) akizaliwa na baba na mama na si na mama pekee  anapingana na aya ziko wazi. Kwa sasa ameleta balaa jipya kuwa eti nyakati za sala ni tatu tu na si tano. Kuwa mtu anatakiwa asali adhuhuri na alasir kwa wakati mmoja na magharib na isha kwa wakati mmoja.

Anasema qurani imetaja nyakati tatu tu na hizi tunazosali sisi nykati tano ni uzushi.

Huyu mtu anatoa aya zifuatazo kutetea vituko vyake, hatujui huyu ni shia au qadiyani au ni bahai, haeleweki haweki wazi itikadi yake na anajichanganya katika shughuli zetu huku Glasgow na kesha ni mtu mwongo mwongo hana ukweli na maneno yake yanageuka geuka, pia anatumia majina mengi hatujui lipi la kweli!? Mimi hisia zangu kubwa ni mshia kwa kuwa nimewahi kumuona akisujudia madongo.

Tusaidieni kufafanua hilo suala tupate kuwahadharisha wengine wasipotezwe na huyu dajal.

Mwenyezimungu awalipe duniani na akhera kwa kutuelimisha bila kuchoka.

tizama dalili za aya na hadithi alizotoa hapa chini na barua yake. Pia amepata nguvu na habri kutoka uturuki na mtu kutoka misr kwamba watu wasali mara tatu na si mara tano. Dalili zake ametoa ni aya hizo na baadhi ya hadithi.

Ayat/4:103

Aat/17:78

Ayat/11:114

Ayat/24:58

Ayat/30:17

Ayat/30:18



Ayat/20:130

 

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza tunashukuru sana ndugu muulizaji kwa swali lako, na kwa kutaka kupata uhakika wa masuala yenye utata kama hayo mliyoletewa.

Pia tunakujulisha kuwa barua ndefu uliyoleta hatukuweza kuiweka yote maana hayahitajiki na pia jina la mtu huyo uliyemtaja tumeliondosha kwa sababu hatuweki majina ya watu na badala yake tunaweka alama za kufutwa.

Kabla ya yote ni muhimu ieleweke kuwa kuzungumzia suala hili kimjadala ni kupoteza muda, na wala halikubali mjadala, lakini kwa kuwa kuna baadhi ya watu wanaeneza ufahamu potofu na kupandikiza uelewa wao wa baadhi ya Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tumeona hatuna budi isipokuwa kuweka wazi suala hili kwa ndugu zetu Waislamu kama ifuatavyo:

  1. Mtu Kukusanya dalili ambazo dhaahir yake ni kupingana, na kuzioanisha baadhi ya dalili hizo na kuziacha nyingine, huo ni utaratibu wa  watu wa Bid'aa na wenye kufuata matamanio yao.

  1. Ni vyema Kutoojiingiza katika mas-ala ya kisheria yanayohitaji uelewa mkubwa katika elimu za misingi ya Fiqhi (Uswuulul Fiqh) na elimu ya Hadiyth (Mustwalahul Hadiyth) kwa wasiobobea katika elimu hizo.

  1. Kutojiingiza katika Ijtihaad wakati Aayah ipo wazi na makubaliano ya wanachuoni wa Kiislamu katika kuielewa Aayah hiyo. Anasema Allaah:

         

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَى وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّى وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ وَسَاءتْ مَصِيرًا

Na atakayemuasi Mtume baada ya kumdhihirikia uongofu na kafuata njia isiyokuwa ya Waislamu tutamgeuza alikogeukia mwenyewe na tutamwingiza katika Jahannam; napo ni pahali pabaya kabisa pa mtu kurudia) [An-Nisaa: 115

 

 

Katika kufafanua maelezo hayo kwa dalili zilizo wazi,

 

Anasema Allaah:

 

{ فَسَوْفَ يَلْقَوْنَ غَيًّا فَخَلَفَ مِنْ بَعْدِهِمْ خَلْفٌ أَضَاعُوا الصَّلَاةَ وَاتَّبَعُوا الشَّهَوَاتِ }

 

(Lakini wakafuatia baada yao kizazi kibaya. Wakapuuza Swalah na wakafuata matamanio mabaya; kwa hiyo watakutana na adhabu kali) 19:59

 

Katika kutafsiri aya hii, Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) anasema ‘kupuuza Swalah’ kama ilivyokuja katika Aayah haina maana ya kuacha Swalah moja kwa moja, bali inakusudia wale wanaoakhirisha Swalah, akaakhirisha Swalah ya adhuhuri hadi alasiri na Swalah ya Maghrib hadi 'Ishaa bila ya dharura.

 

Kwa mujibu wa maelezo yaliotangulia ieleweke wazi kuwa; zimekuja dalili sahihi na zenye mashiko na ambazo hazitafsiriki vingine kuwa Swalah zipo tano kwa siku, na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zimejaa hadiyth zenye kubainisha hivyo. 

 

 ذلك ما رواه الإمام أحمد وغيره عن جابر بن عبد الله الأنصاري: أن النبي صلى الله عليه وسلم جاءه جبريل فقال: قم فصله، فصلى الظهر حين زالت الشمس، ثم جاءه العصر فقال: قم فصله، فصلى العصر حين صار ظل كل شيء مثله أو قال صار ظله مثليه، ثم جاءه المغرب فقال: قم فصله، فصلى حين وجبت الشمس، ثم جاءه العشاء فقال: قم فصله، فصلى حين غاب الشفق، ثم جاءه الفجر، فقال: قم فصله، فصلى حين برق الفجر أو قال حين سطع الفجر. ثم جاءه من الغد للظهر فقال: قم فصله، فصلى الظهر حين صار ظل كل شيء مثله، ثم جاءه العصر، فقال: قم فصله فصلى العصر حين صار ظل كل شيء مثليه، ثم جاءه للمغرب المغرب وقتاً واحداً لم يزل عنه، ثم جاء للعشاء العشاء حين ذهب نصف الليل أو قال ثلث الليل فصلى العشاء، ثم جاءه للفجر حين أسفر جداً فقال قم فصله فصلى الفجر ثم قال: ما بين هذين وقت

.

Katika Hadiythi iliyopokelewa na Imam Ahmad na wengineo kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah Al-Answaariy (Radhiya Allaahu ‘anhum) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alijiwa na Jibriyl na akamwambia; simama uswali, akaswali adhuhuri jua lilipomili (kidogo Magharibi) kisha akamjia Alasiri na akamwambia simama uswali, akaswali Alasiri kivuli kilipokuwa usawa wa mtu, kisha akamjia Maghrib akamwambia simama uswali, akaswali jua lilipozama tu, kisha akamjia ‘Ishaa akamwambia simama uswali, akaswali pale ambapo umanjano ulipoondoka (kiza kuingia) kisha akamjia Alfajri na kumwambia simama uswali,akaswali pale ambapo alfajri ilipochomoza.  kisha Jibriyl akamjia tena siku inayofuata katika wakati wa Adhuhuri akamwambia simama uswali, akaswali adhuhuri kivuli kilipokuwa usawa wa mtu, kisha akamjia Alasiri na akamwambia simama uswali, akaswali pale ambapo kivuli cha kila kitu kilikuwa mara mbili yake, kisha akamjia Maghrib katika wakati mmoja usiobadilika, kisha akamjia ‘Ishaa baada ya usiku wa manane au theluthi ya usiku kama alivyosema akaswali ‘Ishaa, kisha akamjia alfajiri pale ilipokaribia sana kuchomoza na akamwambia simama uswali, akaswali Alfajiri, kisha Jibriyl akasema; baina ya nyakati hizi mbili ni wakati wa Swalah).

 

Maulamaa wote wenye kuzingatiwa tangu zama za As-Salaf Asw-Swaalih hadi sasa hawana mashaka kabisa kuwa Swalah zilizofaradhishwa na Allaah kwa Umma huu ni tano na zinaswaliwa kwa wakati wake (nyakati tano) uliobainishwa na Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hapo juu, na walikubaliana kuwa Swalah tano haziwezi kuwa Swalah tatu isipokuwa kwa vigezo vifuatavyo:

 

  1. Safari; mtu anapokuwa safarini anaruhusiwa kukusanya Swalah baina ya Adhuhuri na Alasiri, Maghrib na Isha'a, Alfajiri inaswaliwa katika wakati huo huo, kwa mantiki hii ndio Swalah tano kwa siku zinaswaliwa mara tatu tu.

 

  1. Kukusanya kwa aliye katika ibada ya Hijja anapokuwa ‘Arafah, Muzdalifa na Minaa.

 

  1. Kukusanya Swalah wakati wa mvua kali, au wakati wa hofu na kukosekana amani.

 

  1. Mtu anapokuwa mgonjwa.

 

Hoja na dalili zinazotolewa kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikusanya Swalah bila ya sababu yoyote na hivyo kutoa hoja kuwa Swalah ni mara tatu kwa siku badala ya mara tano haina msingi wowote, bali ni kutaka kuwavuruga waislamu na ibada yao muhimu ya Swalah ambayo ndio nguzo ya dini.

 

ففي الصحيحين عن ابن عباس قال: صلى رسول الله صلى الله عليه وسلم الظهر والعصر جميعاً بالمدينة في غير خوف ولا سفر، قال أبو الزبير: فسألت سعيداً لم فعل ذلك؟ فقال سألت ابن عباس كما سألتني فقال: أراد أن لا يحرج أحداً من أمته.

 

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas Amesema; Aliswali Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Adhuhuri na Alasiri kwa kukusanya katika mji wa Madiynah bila ya khofu wala safari, akasema Abu Az-Zubayr: nilimuuliza Sa’iyd kwa nini Mtume alifanya hivyo? Sa’iyd akasema; nilimuuliza Ibn ‘Abbaas kama ulivyoniuliza akasema: alitaka Mtume kutomwekea uzito yeyote katika umma wake.

Maelezo haya ambayo hutumiwa kama dalili ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikusanya Swalah bila udhuru wowote, ni dalili kuwa Swalah ni mara tano kwa siku, na Mtume alitaka kuufundisha umma wake kuwa kuna wepesi katika dini, na ndio maana Maswahaba waliulizana sababu ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kufanya hivyo, kwani haikuwa kawaida kufanya hivyo katika nyakati ambazo si za dharura.

Bali, mafundisho mengi yaliyopokewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yako wazi kuwa idadi ya Swalah kwa siku ni Swalah tano na sio vinginevyo.

 

  أرأيت لو كان بفناء أحدكم نهر يجري يغتسل منه كل يوم خمس مرات ما كان يبقى من درنه قالوا : لا شيء قال : إن الصلوات تذهب الذنوب كما يذهب الماء الدرن

الراوي: عثمان بن عفان  -  خلاصة الدرجة: إسناده صحيح  -  المحدث: أحمد شاكر  -  المصدر: مسند أحمد 

 

Kutoka kwa Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) Amesema: Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Je, unaonaje kama kungekuwa na mto upitao mbele ya nyumba ya mmoja wenu, anaoga humo kila siku mara tano, je, uchafu ungebaki katika mwili wake? Wakasema, hakuna (uchafu) Akasema hakika ya Swalah huondosha madhambi kama maji yanvyoondosha uchafu.) Ahmad

 

الصلوات الخمس والجمعة إلى الجمعة كفارات لما بينهن

الراوي: أبو هريرة  -  خلاصة الدرجة: صحيح  -  المحدث: مسلم  -  المصدر: المسند الصحيح

 

kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Amesema: Swalah tano, na Ijumaa hadi Ijumaa, ni vifutio vya madhambi baina ya vipindi hivyo.  Muslim

 

Hizi ni baadhi tu ya dalili kuwa Swalah zilizofaradhishwa na Allaah kwa Umma huu ni mara tano kwa siku, na yeyote atakayepinga hivyo, atakuwa anapinga mambo yaliyojulikana katika dini kama ni mambo ya dharura na msingi.

 

Tunakushauri utakapopata jambo lolote lenye kutaka kutia mashaka imani yenu au lenye utata kutoka kwa mtu kama huyo basi mfanye upesi kutufikishia ili tuwapatie usahihi na uhakika wake inshaAllaah.

 

Kadhalika tunawashauri mkae mbali na watu wa aina hiyo na msipoteze muda wenu wa kheri, watu kama hao na kama ulivyosema kwenye swali lako, ni watu waongo na wapotofu na ambao tayari Allaah keshawaondoshea kheri Zake na neema Zake na wamebaki kuchukua nafasi ya Ibilisi ya kupoteza watu na kuwatia mashaka katika imani zao.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share