Nabiy ‘Iysaa (عَلَيْهِ السَّلام) Alibatizwa? Na Je, Biblia Imeruhusu Ala Za Muziki Na Misalaba Kanisani
Nabiy ‘Iysaa (عَلَيْهِ السَّلام) Alibatizwa? Na Je, Biblia
Imeruhusu Ala Za Muziki Na Misalaba Kanisani
SWALI:
Nia yangu hasa ni kutaka kujua kama Nabii Issa (YESU) Alibatizwa? Kwa mujibu wa Biblia na je vinanda na magitaa kanisani yanaruhusiwa pamoja na kuvaa misalaba mikubwa shingoni ni ruksa nina maana kubwa ndugu zangu kuuliza maswali haya kwani Allah anaweza akaniwezesha kuwatoa watu katika ukafir naoomba majibu yake.
Asalaam Aleykhum.
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Biblia yenyewe tuelewe ina utata mkubwa katika mas-ala mengi hivyo kwa Mkristo aliyebobea huweza kukuvuruga wewe bila wasiwasi. Pia tufahamu hakuna kitabu kilichoteremshwa na Allaah kinachoitwa Biblia.
Mas-ala mengi yana utata katika Biblia hivyo kuwachanganya hata wenye kuifuata Dini hiyo. Tukija katika suala lako twaweza kusema yafuatayo:
Ama kuhusu ubatizo wa Yesu Biblia inatueleza wazi kuwa alibatizwa kama mistari ifuatayo inavyosema:
1) "Mara tu Yesu alipobatizwa" (Mathayo 3: 16). Aliyembatiza ni Yohane kama ilivyo katika msitari wa 15 katika kitabu hicho cha Mathayo.
2) "Yohane mbatizaji alitokea jangwani…Siku hizo, Yesu alitoka kutoka Nazareti, mji wa Galilaya, akabatizwa na Yohane katika mto Yordani" (Marko 1: 4 – 9).
3) "Watu wote walipokuwa wamekwisha batizwa, Yesu naye alibatizwa" (Luka 3: 21).
4) Kitabu cha Yohane kinatueleza kuwa Yohane alikuwa anabatiza lakini hakumbatiza Yesu, kwani alishuhudia tu kuwa Yesu ni mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu (Yohane 1: 24 – 29).
Ama kuhusu vinanda na magitaa (ala za muziki) yapo mistari yanayoruhusu na mengine kukataza. Hilo linatuweka sisi katika hali ya utata kuwa ni lipi lililo sawa. Hebu tutazame baadhi ya maandiko:
1. "Mwenyezi-Mungu asema hivi: 'Nazichukia na kudharau sikukuu zenu; siifurahii mikutano yenu ya kidini. Mjaponitolea sadaka zenu za kuteketezwa za nafaka, mimi sitakubali kuzipokea; na sadaka zenu za amani za wanono mimi sitaziangalia kabisa. Ondoeni mbele yangu kelele za nyimbo zenu! Sitaki kusikiliza muziki wa vinubi vyenu" (Amosi 5: 21 - 23). Tunaelezwa katika kitabu hicho hicho tena: "Nyinyi mnapenda kuimba ovyo na sauti ya vinubi na kubuni ala mpya za muziki mkimwiga mfalme Daudi" (Amosi 6: 5). Hizi ibara zinatuelezea nini sisi? Ibara ya awali inakataza muziki na ya pili inatuelezea kuwa kulikuwa kukibuniwa ala mpya za muziki kwa kumwiga mfalme Daudi. Je, ibara ya pili inaunga mkono muziki au inakataza? Kipengele kimoja kinakataza lakini cha pili kinaunga. Hili linatubabaisha zaidi kuhusu suala hili.
2. Mistari ifuatayo inaruhusu suala hilo kwa uwazi kabisa. Hebu tutazame haya: "Mwimbieni kwa sauti Mungu, nguvu yetu mshangilieni Mungu wa Yakobo; vumisheni wimbo wa shangwe, pigeni ngoma, chezeni zeze na kinubi cha sauti nzuri. Pigeni tarumbeta kutangaza mwezi mwandamo, na pia mwezi mpevu, wakati wa sikukuu yetu" (Zaburi 81: 1 – 3). Hata hivyo, suala linakuja ni nani aliyeruhusu jambo hilo ikiwa Zaburi 72: 20 inasema: "Mwisho wa sala za Daudi, mwana wa Yese". Ikiwa ibara hii ndio mwisho wa Zaburi ya Daudi, sasa hii sura ya 81 inayoruhusu nyimbo na ala za muziki imeruhusiwa na nani? Bila shaka, itakuwa imeruhusiwa na mwingine na wala sio Daudi.
3. Katika Agano la Kale tunaelezwa: "Kwa nini ulitoroka kisiri, ukanihadaa wala hukuniarifu ili nipate kukuaga kwa shangwe, nyimbo, matari na vinubi" (Mwanzo 31: 27). Ibara hii haiwezi kuchukuliwa kama ni ruhusa kwani aliyesema ni mshirikina ambaye katika msitari wa 32 amesema: "Lakini kwa nini uliiba vinyago vya miungu yangu?"
4. Ruhusa nyingine inapatikana katika Kutoka 15: 20: "Basi nabii Miriamu, dada yake Aroni, akachukua kigoma mkononi, na wanawake wengine wote wakamfuata wakiwa na vigoma vyao wakicheza". Hii ni taarifa ya furaha iliyopatikana kwa upande wa wanawake pale Firauni alipoangamizwa na Mwenyezi Mungu wakiwa wanawake wapo peke yao.
Suala hili mbali na kuwa na utata dalili ya ibara zenye nguvu ni zile zinazokataza matumizi ya ala hizo.
Ama utumiaji wa msalaba katika kuvaa umezagaa kabisa kwa Wakristo wa zamani na wa sasa. Kufanya hivyo kwao ni kukumbuka kule kusulubiwa kwa Yesu kwa ajili ya dhambi za wanadamu nao waingie katika kusamehewa dhambi zao hapa duniani na kurithi uzima wa milele Siku ya Qiyaama. Hata hivyo, tukisoma katika Biblia tunapata kuwa Yesu hakusulubiwa kwani aliyesulubiwa atakuwa amelaaniwa. Hebu tutazame mistari ifuatayo:
a) "Kama mtu amefanya kosa la jinai linalompasa auawe na akauawa kwa kutundikwa mtini" (Kumbukumbu la Sheria 21: 23).
b) "Kristo alitukomboa kutoka katika laana ya sheria kwa kujitwalia laana hiyo kwa ajili yetu; maana Maandiko yanasema: 'Yeyote aliyetundikwa msalabani amelaaniwa" (Wagalatia 3: 13).
Hakika ni kuwa wenye kuamini kuwa Yesu kasulubiwa na misalaba kwa ajili ya kusamehewa dhambi wanapingana na Biblia. Hebu tusome mistari ifuatayo:
i. "Maana ninachotaka kwenu ni upendo na si dhabihu, kumjua Mungu na si kutoa sadaka za kuteketezwa" (Hosea 6: 6).
ii. "Basi, kajifunzeni maana ya maneno haya: 'Nataka huruma, wala si dhabihu'. Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi" (Mathayo 9: 13).
iii. "Kama tu mngejua maana ya maneno haya: 'Nataka huruma wala si dhabihu', hamngewahukumu watu wasio na hatia" (Mathayo 12: 7).
Kwa hivyo Yesu hakuja kuwa dhabihu, yaani kuuliwa msalabani bali amekuja kuwaokoa wenye hatia waingie katika mafundisho ya haki na hivyo kupata msamaha wa Allaah.
Na Allaah Anajua zaidi