Mkiristo Anataka Kujua Kama Nabii Muhammad (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم) Ana Miujiza Kama Ya Nabii ‘Iysa

 

 

Mkiristo Anataka Kujua Kama Nabii Muhammad

(صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم) Ana Miujiza Kama Ya Nabiy ‘Iysa  

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Ndugu Zangu Waislam Ninawapenda, Kwa Maana Allaah (Mungu), Wangu Anahimiza Sana Upendo. Kitu Kimoja Ambacho Ninataka Nijue Kutoka Kwenu, Mimi Ni Mkisto Ambaye Ninampenda Allaah(Mungu) Na Namuamini Yesu, Yesu Alifanya Miujiza Ambayo Hakuna, Ambaye Aliye Weza Kufanya, Na Allaah (Mungu) Aliiruhusu Hiyo Miujiza Ili Watu, Waamini, Allaah Anaweza Na Pia Yupo, Je? Mtume Muhammad Ni Kitu Gani Ambacho, Allaah(Mungu) Alikidhihirisha Kwake Ili Watu Wamuamini, Maana. Sheria Ambazo Anazozieleze Ni Zile Zile Za Enzi Ya Kina Muswaa. Naomba Jibu Tafadhali

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Nasi kwa upande wetu mwanzo twakualika kujiunga na Uislamu, Dini ambayo ndiyo aliyokuja nayo Nabii Aadam, Ibraahiym, Muwsaa, ‘Iysa na Muhammad (Amani ya Allaah iwe juu yao wote).

 

Katika Itikadi yetu, ni kuwaamini Rusuli na Manabii wote waliotumwa, pasi na kufanya hivyo mtu huwa hajakuwa Muumini. Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Anasema:

 

آمَنَ الرَّسُولُ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْهِ مِن رَّبِّهِ وَالْمُؤْمِنُونَ ۚ كُلٌّ آمَنَ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّن رُّسُلِهِ ۚ وَقَالُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۖ غُفْرَانَكَ رَبَّنَا وَإِلَيْكَ الْمَصِيرُ ﴿٢٨٥﴾

Rasuli ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Rabb wake na Waumini (pia). Wote wamemwamini Allaah, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake, na Rusuli Wake. (Nao husema): Hatutofautishi baina ya yeyote kati ya Rusuli Wake. Na wakasema: Tumesikia na tumetii, tunakuomba maghfirah Rabb wetu na Kwako ni mahali pa kuishia [Al-Baqarah: 285].

 

Ama mas-ala ya Miujiza ni kuwa Nabiy au Rasuli hawezi kufanya lolote pasi na amri ya kutoka kwa Allaah. Ndio Qur-aan inatuelezea kuhusu yale yaliyofanywa na Nabiy ‘Iysa,

 

وَرَسُولًا إِلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ أَنِّي قَدْ جِئْتُكُم بِآيَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ ۖ أَنِّي أَخْلُقُ لَكُم مِّنَ الطِّينِ كَهَيْئَةِ الطَّيْرِ فَأَنفُخُ فِيهِ فَيَكُونُ طَيْرًا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۖ وَأُبْرِئُ الْأَكْمَهَ وَالْأَبْرَصَ وَأُحْيِي الْمَوْتَىٰ بِإِذْنِ اللَّـهِ ۖ وَأُنَبِّئُكُم بِمَا تَأْكُلُونَ وَمَا تَدَّخِرُونَ فِي بُيُوتِكُمْ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لَّكُمْ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿٤٩﴾

Na ni Rasuli kwa wana wa Israaiyl (akisema): Hakika mimi nimekujieni na Aayah (ishara, dalili) kutoka kwa Rabb wenu, kwamba mimi nakuundieni kutokana na udongo kama umbo la ndege, kisha napuliza humo basi huwa ndege kwa idhini ya Allaah. Na naponyesha vipofu na wenye ubarasi na nahuisha wafu kwa idhini ya Allaah. Na nakujulisheni mtakavyokula na mtakavyoweka akiba majumbani mwenu. Hakika katika hayo bila shaka kuna Aayah kwenu mkiwa Waumini. [Aal-'Imraan: 49]

 

Bali katika mambo ambayo alishindwa kuyafahamu ni kushindwa kwake baada ya kuwa na njaa ni kujua kama mti uliokuwa mbele yake una matunda au hauna. Alikuwa na njaa sana lakini alipowasili kwenye mti akaukuta hauna matunda, akaulaani na kuanzia wakati huo haukumea tena matunda.

 

Lakini ukitizama katika Biblia utakuta muujiza wa kwanza wa Nabiy ni kugeuza maji kuwa pombe safi (Yohana 2: 2 – 11) ilhali Qur-aan inatufahamisha kuwa muujiza wake wa kwanza ni kuzungumza akiwa mchanga,

 

قَالَ إِنِّي عَبْدُ اللَّـهِ آتَانِيَ الْكِتَابَ وَجَعَلَنِي نَبِيًّا ﴿٣٠﴾وَجَعَلَنِي مُبَارَكًا أَيْنَ مَا كُنتُ وَأَوْصَانِي بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ مَا دُمْتُ حَيًّا ﴿٣١﴾وَبَرًّا بِوَالِدَتِي وَلَمْ يَجْعَلْنِي جَبَّارًا شَقِيًّا ﴿٣٢﴾

(Mtoto) Akasema: Hakika mimi ni mja wa Allaah; Amenipa Kitabu (Injiyl) na Amenijaalia kuwa Nabiy. Na Amenijaalia kuwa mwenye kubarikiwa popote nitakapokuweko, na Ameniusia Swalaah na Zakaah madamu niko katika uhai. Na niwe mtiifu kwa mama yangu na wala Hakunijaalia kuwa jeuri, mwovu. [Maryam: 30 – 32]

 

Na tufahamu kuwa Yesu hakuleta lolote jipya katika sheria isipokuwa kwa uchache sana kama anavyosema Allaah:

 

 وَمُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيَّ مِنَ التَّوْرَاةِ وَلِأُحِلَّ لَكُم بَعْضَ الَّذِي حُرِّمَ عَلَيْكُمْ ۚ وَجِئْتُكُم بِآيَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿٥٠﴾

Na mwenye kusadikisha yaliyo kabla yangu katika Tawraat na ili nikuhalalishieni baadhi ya yale yaliyoharamishwa kwenu. Na nimekujieni na Aayah (ishara, hoja) kutoka kwa Rabb wenu. Basi mcheni Allaah na nitiini. [Aal-'Imraan: 50]

 

Nabiy Muhammad aliridhiwa na mengi na Allaah, ikiwa moja ni kufanywa yeye ni Nabiy wa mwisho ambaye kuondoka kwake hakutakuja Nabiy mwengine yeyote,

 

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ﴿٤٠﴾

Hakuwa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Rasuli wa Allaah na ni mwisho wa Manabii. Na Allaah daima ni Mjuzi wa kila kitu. [Al-Ahzaab: 40]

 

Kisha yeye ametumwa kuwa ni rehma kwa walimwengu wote, kama alivyosema Allaah,

 

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ ﴿١٠٧﴾

Na Hatukukutuma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) isipokuwa ni rahmah kwa walimwengu. [Al-Anbiyaa: 107]

 

Allaah Alimdhihirishia na kumteremshia Qur-aan ambacho ni kitabu cha mwisho kitukufu ambacho hakijabadilika na kimebakia kama kilivyoteremshwa mwanzo. Allaah Anasema,

 

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ ﴿٩﴾

Hakika Sisi Tumeteremsha Adh-Dhikra (Qur-aan) na hakika Sisi bila shaka ndio Wenye kuihifadhi. [Al-Hijr: 9].

 

Qur-aan ndio iliyo na sharia ya kufuatwa na Muislamu, nayo imekuja kusahilisha katika mazito mengi yaiyopatikana katika sharia zilizotangulia. Hivyo, yapo mambo yanayofanana na ya Nabiy Muwsaa kwani wote wameteremshiwa ufunuo na Allaah huyo huyo mmoja.

 

Kwa minajili hiyo, jumbe za Manabii wote ni hii,

 

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ ۖ

Na kwa yakini Tulituma katika kila ummah Rasuli (alinganie) kwamba: Mwabuduni Allaah na jiepusheni na twaghuti.  [An-Nahl: 36]

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alete tawfiki Yake.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share