Siku Ya Jumamosi Mayahudi Walifanya Nini Hata Wakageuzwa Manyani?
Siku Ya Jumamosi Mayahudi Walifanya Nini Hata Wakageuzwa Manyani?
SWALI:
Ass-salamu allaiqum warahmatulwah wabarakatu, ndugu yangu ninataka msada wako au wenu juu ya maelezo yangu haya. Nimesoma ktk tafsiri ya Quraan juzuu ya 1 Suwrah al-Baqarah ayaa ya 65, Allaah alisema kuwaambia Mayahudi watu wa Nabiy Muwsaa ('A-S), Walishindwa kuihishimu siku wa Jumaamosi basi Allaah (S.W) akawambia kuweni manyani wadhalilifu. ndugu yangu muislam nnataka unisaidie hapa ktk hii siku ya J'mosi binaadamu hawa walifanya nini?
Asalammu alaaiqum warahmatulwahy wabarakatu.
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Nabiy, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'aalaa) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Nabiy. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.
Katika kusoma tafsiri ya Qur-aan na kuweza kupata msaada wa kuielewa vizuri hivo tafsiri ni kujaribu kungalia maelezo ya Mfasiri ambayo huwa ima pamewekwa Aayah nyengine inayoitafsiri hiyo Aayah; kwani Qur-aan inafasiri Qur-aan na ndio kitu cha mwanzo katika kutafsiri Qur-aan ni Qur-aan yenyewe; au pamewekwa Hadiyth za Mtume ya (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yenye kuitafsiri hiyo Aayah au maelezo ya Swahaba yenye ufafanuzi wa Aayah; au pamewekwa ishara ya kukueleza wapi kumetajwa kinachozungumzwa na Aayah hii kwa ufafanuzi au kwa urefu; kama ilivyokuwa katika Aayah hii.
وَلَقَدْ عَلِمْتُمُ الَّذِينَ اعْتَدَوْا مِنكُمْ فِي السَّبْتِ فَقُلْنَا لَهُمْ كُونُوا قِرَدَةً خَاسِئِينَ ﴿٦٥﴾فَجَعَلْنَاهَا نَكَالًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهَا وَمَا خَلْفَهَا وَمَوْعِظَةً لِّلْمُتَّقِينَ ﴿٦٦﴾
Al-Na kwa yakini mlikwishawajua wale miongoni mwenu waliotaadi mipaka ya As-Sabt Tukawaambia: Kuweni manyani waliobezwa.Tukaifanya kuwa ni adhabu ya kuonya kwa waliokuweko zama zao na wataokuja baada yao na ni mawaidha kwa wenye taqwa. [Al-Baqarah: 65-66]
Umeuliza, ‘hii siku ya J'mosi binaadamu hawa walifanya nini?’ Kwa faida ya wengi tutakujibu. Ni kuwa siku ya Jumamosi ilikuwa ni siku ya ibaada tu kwa Mayahudi wa zama hizo na katika walichotakiwa ni kuiheshimu siku hiyo kwa kutojishughulisha na aina yoyote ile ya kazi, na miongoni mwao walikuwa wavuvi wa kijiji kimoja kilicho kuwa karibu na bahari, hivyo Allaah kwa hekima na uadilifu wake na kuelewa fika kuwa uvuvi ndio kipato chao na ndio kitu wanachopenda Alitaka kuwaangalia utiifu wao Kwake kwa kuwakataza kuvua katika siku hiyo ili Awapambanuwe walioamini na wale wenye kujidai kuwa wameamini; na hivyo ndivyo ilivyotokea; kwani miongoni mwao walikuwemo walioamini na kwa kuelewa yanayowapata kila mwenye kuthubutu kuhalalisha Alichokiharamisha Allaah.
Waliwakataza wenzao (ni watu wa kijiji kimoja lakini kila mmoja na imani yake, wengine wanakwenda darsa na wengine wanaona hakuna haja, kwani wanaelewa kila kitu katika dini) kundi lililokuwa linataka kuvunja amri ya Allaah kwa kwenda kuvua (na hivi ndivyo wanavyotakiwa Waislamu kuamrishana mema na kukatazana mabaya sio kusema, kwani hawaelewi?!); kundi jingine likaona hakuna haja ya kuwakataza kwani wanaelewa uharamu na yatakayokuja kwa kuvunja amri ya Allaah; hivyo wale wakaidi baada ya kukumbusha na kuwaidhiwa hawakufaidika na mawaidha wala hawakuona umuhimu wa kukumbushana, matamanio yao yakawa ndio mungu wao hivyo wakamua kuivunja amri ya Allaah ya kutovua samaki siku ya Jumaamosi, kwani ni siku pekee wanayoweza kupata kipato kikubwa na bila ya kupata taabu kwani siku hii iliyokatazwa kuvua samaki walikuwa wakiwajia vururu juu ya maji, wakati siku isiyo kuwa Jumaamosi samaki hawaji kama hivi (hii ni katika mitihani wa Allaah), kama ilivyoweka wazi Qur-aan kwa kusimulia:
وَاسْأَلْهُمْ عَنِ الْقَرْيَةِ الَّتِي كَانَتْ حَاضِرَةَ الْبَحْرِ إِذْ يَعْدُونَ فِي السَّبْتِ إِذْ تَأْتِيهِمْ حِيتَانُهُمْ يَوْمَ سَبْتِهِمْ شُرَّعًا وَيَوْمَ لَا يَسْبِتُونَ ۙ لَا تَأْتِيهِمْ ۚ كَذَٰلِكَ نَبْلُوهُم بِمَا كَانُوا يَفْسُقُونَ ﴿١٦٣﴾وَإِذْ قَالَتْ أُمَّةٌ مِّنْهُمْ لِمَ تَعِظُونَ قَوْمًا ۙ اللَّـهُ مُهْلِكُهُمْ أَوْ مُعَذِّبُهُمْ عَذَابًا شَدِيدًا ۖ قَالُوا مَعْذِرَةً إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ ﴿١٦٤﴾فَلَمَّا نَسُوا مَا ذُكِّرُوا بِهِ أَنجَيْنَا الَّذِينَ يَنْهَوْنَ عَنِ السُّوءِ وَأَخَذْنَا الَّذِينَ ظَلَمُوا بِعَذَابٍ بَئِيسٍ بِمَا كَانُوا يَفْسُقُونَ ﴿١٦٥﴾فَلَمَّا عَتَوْا عَن مَّا نُهُوا عَنْهُ قُلْنَا لَهُمْ كُونُوا قِرَدَةً خَاسِئِينَ ﴿١٦٦﴾
Na waulize kuhusu mji ambao ulikuwa kando ya bahari, waliporuka mipaka ya As-Sabt walipowajia samaki wao waziwazi siku yao ya Sabt Na siku zisizokuwa za Sabt hawakuwajia. Hivyo ndivyo Tulivyowajaribu kwa yale waliyokuwa wakifanya ufasikiNa pindi ummah miongoni mwao uliposema: Kwa nini mnawawaidhi watu ambao Allaah Atawahiliki au Atawaadhibu adhabu kali? Wakasema: Tupate kuwa na udhuru mbele ya Rabb wenu na huenda wakawa na taqwa. Waliposahau yale waliyokumbushwa nayo; Tuliwaokoa wale wanaokataza uovu, na Tukawachukua wale waliodhulumu kwa adhabu mbaya kabisa kwa yale waliyokuwa wakifanya ufasiki. Basi walipozidi kuasi kuhusu yale waliyokuwa wakikatazwa, Tulisema: Kuweni manyani waliotezwa. [Al-'Araaf: 163-166]
La muhimu hapa ni kuelewa kuwa kilichowafika waliovunja amri za Allaah katika zama zile kinaweza kuwafika wanaozivunja na kuzikejeli wa zama hizi kama hakutokuwa na wenye kuamrisha mema na kukataza mabaya katika jamii; kwani kilichowafika ni kama funzo na onyo kwa wengine (tukiwemo sisi), kilichowafika ni zingatio kwa watu wa zama ile na watakaokuja baada yao.
Na Allaah Anajua zaidi