Imani Yangu Inapungua Nakhofu Kupotoka Nifanyeje?

 

SWALI:  

 

asalam aleikum.

swali langu ni najiona siku zinavyo zidi kenda najiona imani yangu inapungua nakuwa mzito wakufanya ibada na kusoma quraan, nina ogopa nisije nikaendelea hivihivi. naombeni  mnisaidie nifanye nini? niweze kurudi katika msimamo mzuri wa  dini.

na alaah awajaalia kila la kheri kwa kazi mnayo fanya ya kuelimisha watu

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunapenda kujulisha kwamba mja anapotambua kuwa imani yake inakuwa dhaifu na anapotaka kujua njia za kujikurubisha na Mola wake ni dalili ya uongofu na kupendwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Kwani wangapi wanakuwa katika hali kama hiyo lakini hawatambui wala kujali bali kuacha nafsi zao ziendelee kuridhisha matamanio yake.

 

Hivyo inakupasa kwanza kumshukuru Mola wako Mtukufu kwa kukutanabahisha kabla ya kutumbukia kabisa katika upotofu.

 

Pili fanya yafuatayo ili usalimike na urudishe hali yako katika usalama na taqwa:

 

  1. Mlaani shaytwani kwa kusema kila mara  (A’uddhu BiLLahi minashaytwaanir-Rajiym)  
  2. Jieke katika wudhuu kila mara
  3. Soma sana Qur-aan pamoja na maana yake.
  4. Soma nyiradi za asubuhi na jioni kila siku BILA YA KUACHA nazo zinapatikana katika kiungo kifuatacho:

 

Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)

 

027-Hiswnul-Muslim: Nyiradi Za Asubuhi Na Jioni

 

 

  1. Sikiliza sana mawaidha yaliyomo Alhidaaya, chagua mawaidha ya mbali mbali yanayohusu kujikurubisha kwa Allah,
  2. na yatakayokupa  khofu ya adhabu zake.
  3. Jieupushe na mambo yote ya upuuzi bali tumia wakati wako wote katika dhikr, kutafuta elimu na ibada.
  4. Jeipushe na marafiki wabaya.
  5. Omba sana du’aa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akusaidie kukurudisha katika iymaan na taqwa.
  6. Fanya sana Istighfaar.
  7. Kumbuka mauti kila mara na kwamba haya maisha na ya starehe ndogo tu, na kwamba maisha ya Akhera ndiyo ya milele.

 

Tunatumai kwamba utayatekeleza hayo tuliyokuarifu, na tunaomba kuwa yakufae, na Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Azidi Kukuongoza Akutoe katika kiza unachokaribia kuingia na Akuweke katika nuru na Akujaalie uwe katika waja Wake Wema.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share