Apeleke Posa Vipi Mji Mwengine Mbali Na Hana Jamaa Huko

 

SWALI:

aww. Mimi ni kijana wa kiislam ninayetarajia kufanza suala la posa na nyumbani kwa mtarajiwa wangu inshaallah ni dar na kwetu ni muleba na dar sina ndugu wa karibu, na zaidi wazazi wangu wapo mbali ila wamekwisha niridhia kuoa je nitafanzaje ili nitoa posa kwao? naomba nishauliwe

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika  Salaam hazifai kufupishwa kwa kuandikwa (A.A) au (A.A.W.W.) au kama ulivyoandika kwani haijafundishwa hivyo na pia ni kujikosesha fadhila za Salaam kama tulivyoelezwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo nayo tujizoeshe kuandika (Assalaamu ‘alaykum) au (Assalaamu ‘alaykum wa rahmatullaah) au (Assalaamu ‘alaykum wa Rahmatullaah wa Barakaatuh) kwa ukamilifu na tutakuwa tumeiga mafunzo ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia tutakuwa tumezoa thawabu zote za Salaam kama tulivyofundishwa. Na Mafunzo yote na fadhila zake zimo Alhidaaya katika kiungo kifuatacho: Maamkizi Ya Kiislamu.  

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako nasi twakuombea kila la kheri katika kutekeleza jambo hilo la kimaumbile lililo muhimu katika maisha ya Muislamu.

Ama kuhusu kupeleka posa kwako kwa wazazi wa msichana zipo njia nyingi nasi hapa tutakunasihi ili uweze kutekeleza hilo kwa njia iliyo nzuri.

 

Jambo ambalo unaweza kufanya ni kama mkeo mtarajiwa ana jamaa hapo Muleba unaweza kupeleka posa yako kwa jamaa wa msichana hapo hapo. Na ikiwa mkeo mtarajiwa hana jamaa kabisa basi unaweza kuwapigia simu wazazi wa mkeo mtarajiwa na hasa ukazungumza na walii wake yaani babake. Ikiwa baba hayupo kwa kuwa amefariki basi babu ya mchumba wake au ndugu yake wa kiume. Hata hivyo, ingekuwa vyema kama mkeo mtarajiwa hana jamaa hapo wewe mwenyewe ufunge safari uende Dar ili kuonana na jamaa za mkeo mtarajiwa. Kufanya hivyo kunaweza kuchangia kwa njia nzuri zaidi ili baadaye kusije kukatokea sinto fahamu (su-u tafaahum) baina yako na wazazi hao.

Twakuombea kila la kheri katika shughuli hiyo.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share