Mafunzo Kutoka Kisa Cha Nabiy Ayyuwb
Mafunzo Kutoka Kisa Cha Nabiy Ayyuwb ('Alayhis-salaam)
SWALI:
Considering kisa of nabiy Zakariyyah (AS) and nabiy Ibrahiym (AS) who with ALLAHS grace has bestowed to them children at an old age and nabiy Ayyuwb (AS) got other children after a long illness. What are the lessons do we get from these kisaa of nabiy AS with this respect.
Thanks,
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kwanza tunakunasihi kutokufupisha maamkizi ya Kiislaam au Thanaa au kuwaombea Swalaah na Salaam Manabii, au kuwatakia Radhi Swahaba na mengineyo ambayo watu wanakosea kama hivyo. Jambo hilo limekemewa na ‘Ulamaa wetu. Bonyea viungo vifuatavyo upate faida:
Hukmu Ya Kufupisha Thanaa (Kumtukuza Allaah) Na Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Na Maamkizi Ya Kiislam
Al-Lajnah Ad-Daaimah: Haijuzu Kufupisha Kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Katika Maandishi
Imaam Ibn Baaz: Kufupisha Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Kwa Mfumo Wowote Haijuzu
Hakika ni kuwa visa vyote vilivyotajwa na Allaah Aliyetukuka katika Qur-aan vina mazingatio kwa Ummah huu ikiwa ni visa vya watu wema na Manabii au watu wabaya. Visa vyote vinavyosimuliawa katika Qur-aan ni vizuri kama Anavyotueleza Aliyetukuka:
نَحْنُ نَقُصُّ عَلَيْكَ أَحْسَنَ الْقَصَصِ بِمَا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ هَـٰذَا الْقُرْآنَ
Sisi Tunakusimulia (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) simulizi nzuri kabisa katika Tuliyokufunulia Wahy hii Qur-aan. [Yuwsuf: 3]
Ama kuhusu darsa na mafundisho tunayopata katika visa hivi Allaah Aliyetukuka Anasema:
لَقَدْ كَانَ فِي قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ۗ مَا كَانَ حَدِيثًا يُفْتَرَىٰ وَلَـٰكِن تَصْدِيقَ الَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ وَتَفْصِيلَ كُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿١١١﴾
Kwa yakini katika visa vyao kuna mafunzo kwa wenye akili. Haikuwa (Qur-aan) hadithi zinazotungwa, lakini ni sadikisho la (vitabu) vya kabla yake na tafsili ya waziwazi ya kila kitu, na ni mwongozo na rahmah kwa watu wanaoamini. [Yuwsuf: 111]
Ama tukiangazia mafunzo tunayopata katika kisa cha baba wa Rusuli, Nabiy Ibraahiym ('Alayhis-salaam) tunaona ya kwamba alijitolea mhanga kwa kiasi kikubwa mpaka Allaah Aliyetukuka Akamchagua kuwa Imaam kwa watu. Anasema Aliyetukuka:
إِنَّ إِبْرَاهِيمَ كَانَ أُمَّةً قَانِتًا لِّلَّـهِ حَنِيفًا وَلَمْ يَكُ مِنَ الْمُشْرِكِينَ﴿١٢٠﴾
Hakika Ibraahiym alikuwa Imaam mtiifu kwa Allaah, aliyeelemea haki na wala hakuwa miongoni mwa washirikina. [An-Nahl: 120]
Alipita mitihani mikubwa yote aliyopatiwa kama Alivyoeleza Allaah Aliyetukuka kama ilivyo katika Suwrah Al-Baqarah: 124. Kwa wepesi aliokuja nao katika Dini ndio Allaah Aliyetukuka Akatuamuru tufuate mila hiyo yake [Al-Hajj: 78].
Ama Nabiy Zakariyyah ('Alayhis Salaam) alikuwa ni mnyenyekevu wa hali ya juu wala hakufa moyo akijua hakika kuwa Allaah Aliyetukuka yupo na Atamwitikia du’aa yake aliyoomba. Na tukisoma katika Suwrah Maryam mwanzoni tutapata hayo.
Ama tukija kwa Nabiy Ayyuwb ('Alayhis-salaam) naye pia tunapata mafunzo kemkemu kwani uvumilivu wake ni wa kuigwa na kupigiwa mfano kwa Ummah wote. Daraja yake kwa mpangilio tunapata katika Aayah ifuatayo:
إِنَّا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ كَمَا أَوْحَيْنَا إِلَىٰ نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ مِن بَعْدِهِ ۚ وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَالْأَسْبَاطِ وَعِيسَىٰ وَأَيُّوبَ وَيُونُسَ وَهَارُونَ وَسُلَيْمَانَ ۚ وَآتَيْنَا دَاوُودَ زَبُورًا ﴿١٦٣﴾
Hakika Tumekufunulia Wahy (ee Muhammadصلى الله عليه وآله وسلم) kama Tulivyomfunulia Wahy Nuwh na Manabii baada yake. Na Tumemfunulia Wahy Ibraahiym na Ismaa’iyl na Is-haaq na Ya’quwb na dhuriya, na ‘Iysaa na Ayyuwb na Yuwnus na Haaruwn, Na Sulaymaan. Na Tumempa Daawuwd Zabuwr. [An-Nisaa: 163]
Kuhusu madhara aliyopata Nabiy Ayyuwb ('Alayhis-salaam) na kuyavumilia hadi kumuomba Allaah Aliyetukuka Amuondoshee, na Aliyetukuka Akawa ni mwenye kumuondeshea hilo. Anasema Aliyetukuka:
وَأَيُّوبَ إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ أَنِّي مَسَّنِيَ الضُّرُّ وَأَنتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ ﴿٨٣﴾فَاسْتَجَبْنَا لَهُ فَكَشَفْنَا مَا بِهِ مِن ضُرٍّ ۖ وَآتَيْنَاهُ أَهْلَهُ وَمِثْلَهُم مَّعَهُمْ رَحْمَةً مِّنْ عِندِنَا وَذِكْرَىٰ لِلْعَابِدِينَ ﴿٨٤﴾
Na Ayyuwb alipomwita Rabb wake: Hakika mimi imenigusa dhara, Nawe Ndiye Mbora zaidi wa kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu. Tukamuitikia basi Tukamuondoshea dhara aliyokuwa nayo, na Tukampa ahli zake na mfano wao pamoja nao; ni rahmah kutoka Kwetu na ni ukumbusho kwa wanaoabudu (Allaah). [Al-Anbiyaa: 83 – 84]
Na Allaah Aliyetukuka Anamtaja Nabiy Ayyuwb ('Alayhis-salaam) kuwa ni mja Wake pindi alipomrudia Yeye baada ya kupata madhara na udhia kutoka kwa shetani. Haya yaliyotokea kwa kurudishiwa watu wake ni mawaidha kutoka kwa Allaah Aliyetukuka kwa wenye akili. Baada ya hapo tunaambiwa kuwa alikuwa mja mwenye kusubiri (38: 41 – 44). Kwa mwenye akili hakika atapata mawaidha makubwa sana katika maneno ya Allaah Aliyetukuka tuliyoyaeleza.
Kwa muhtasari tunapata fundisho katika maisha ya Nabii Ayyuwb ('Alayhis-salaam) la kusubiri, unyenyekevu, kumuomba Allaah Aliyetukuka katika matatizo, kuendelea kufanya Ibaadah katika hali zote na shetani hawezi kumghuri mja mwema, na kadhalika.
Na Allaah Anajua zaidi