Anataka Kuishi Na Mchumba Wake Chumba Kimoja Kabla Ya Kuoana

 

Anataka Kuishi Na Mchumba Wake Chumba Kimoja Kabla Ya Kuoana

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Je, unaweza kumpokea mwanaume mukawa faragha mwenye niya yakukuowa kwa ajili ya kumsaidia pahala pa kulala ambapo ni chumba chako kwa muda hadi apate kazi ndio muowane?

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Maswali haya ya kuhusiana na uchumba yamekuwa mengi na yanakithiri kila uchao. Hii inatokana na kuacha maagizo tuliyoamriwa na Allaah Aliyetukuka na Nabiy wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Kuiga tabia na maadili ya Wamagharibi kumekuwa ni mfumo wetu wa maisha.

 

 

Katika njia ambazo zilizozibwa na Uislamu ni kukaa faragha baina ya mwanamme na mwanamke ajnabi bila kuwepo maharimu wa mwanamke pamoja nao. Mwanamke ajnabi ni yule ambaye si mke wa huyo mwanamume wala mmoja katika watu wake ambao ameharamishiwa kuwaoa kabisa kama mama, dada, na kadhalika.

 

 

Huku kufanya hivi sio kwa kuwa hatuwaamini au hatumuamini mmoja wao, lakini ni kuwahifadhi kutokana na kushawishiwa na shetani na kupitiwa na fikra mbovu ambazo kwa kawaida huwapitia wakati wanapokutana mwanamke na mwanamme katika faragha. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuhusu haya:

 

'Mwenye kumuamini Allaah na siku ya mwisho basi asikae peke yake na mwanamke asiyekuwa na maharimu wake pamoja naye, kwani watatu wao ni shetani' [Ahmad].

 

 

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhuma) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 'Asikae faragha mmoja wenu na mwanamke isipokuwa awe pamoja na maharimu wake' [al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) akahadharisha zaidi mwanamke kukaa peke yake na jamaa zake mumewe kama shemeji au binamu yake mume kwa ajili ya kuchukuliwa kuwa hawa ni watu wa nyumbani na hawadhuru neno, lakini mara nyingine haya huleta madhara makubwa sana, kwani kukaa faragha na mtu wa nyumbani ni hatari zaidi kuliko kukaa na mtu wa nje. Halikadhalika, jamaa zake mke wanaoweza kumuoa kama binamu yake, mtoto wa mjomba au shangazi au ami au halati kwani hawa wote haijuzu kwa mwanamke kukaa nao peke yake bila maharimu.

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 'Tahadharini na kuingia kwa wanawake'. Akasema mmoja katika Answaar, 'Ee Rasuli wa Allaah, unaonaje jamaa zake mume?' Akajibu: 'Jamaa zake mume ni mauti' [al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Kwa hiyo, kukaa faragha na mchumbako kisheria haifai. Jambo ambalo unaweza kumnasihi mchumbako ni aje akuoe baada ya posa au muvumilie mpaka mtakapokuwa tayari kuingia katika uanandoa.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share