Alikuwa Akifanya ‘Ibaadah Sana Kabla Ya Kumuoa, Kisha Baada Ya Ndoa Mume Haswali Tena Afanyeje
Alikuwa Akifanya ‘Ibaadah Sana Kabla Ya Kumuoa, Kisha Baada
Ya Ndoa Mume Haswali Tena Afanyeje
Swali:
Asalaam aleykum
Napenda kuwapongeza kwa kazi nzuri ya kutuelimisha sisi Waislamu In shaa Allaah Allaah awalipe malipo mema na siku ya mwisho tukutane wote katika pepo Aamiin.
Mimi ni mwanamke niliyeolewa, na hakika mume huyu nilimpenda kutokana na muonekano wake wa kuwa mwenye kufanya ibada sana na ni mtu mwema, anapenda kusaidia watu wenye matatizo n.k, tulikutana tulipokuwa masomoni na alikuwa ni kiongozi wetu katika kikundi cha dini katka hiyo shule, ukweli mashallah Dini ameisoma na anaelewa vizuri sana.
lakini kinachonikwaza kwa mume wangu huyu amekuwa hasimamishi swala, na kila ninapomkumbusha huwa anasema sawa mke wangu ninasali sasa kwa kuwa kila mmoja anashughuli zake tunaachana pale asubuhi na kuonana jioni lkn muda wa magharibi, Ishaa na subhi simuoni mwenzangu kusali, najitahidi kumkumbusha lakini hadi inafikia kipindi amani inatoweka ndani ya nyumba sababu ni kumwambia kila mara bwana muda wa sala huo umefika, na Allaah ametujaalia nyumba yetu inatizamana na msikiti. Ukweli ninasikitika sana nashindwa nifanye nini kwani Nilimuomba Allaah anipe mume mwema lkn mwenzangu anamapungufu hayo tu katika swalah. Naomba mnisaidie nifanye nini ili aweze kusimamisha swala kama inavyotakiwa.
Nawatakia kazi njema wabillah Tawfiq.
Jibu:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakika dunia ina mitihani mingi sana na wakati mwengine sisi wanaadam hushindwa kukabiliana na mitihani hiyo kwa sababu moja au nyingine.
Ndio kwa minajili hiyo tunatakiwa kila wakati tuwe ni wenye kumuomba Muumba wetu, Allaah Aliyetukuka Atupatie hatima njema na tusife ila katika Imani na Uislamu. Kwa njia hii kwa kuwa Uislamu ni muongozo wa maisha yetu hapa duniani umetupatia ufumbuzi wa kila jambo na tatizo linalo mkabili mwanaadamu katika huu ulimwengu.
Kwa ajili hiyo, mwanzo inatakiwa wewe umlilie Rabb wako kwa tatizo unalokabiliana nalo kwa kuishi na mume ambaye haswali. Swalah ndio tofauti baina yetu sisi na makafiri, mwenye kuiacha amekuwa kafiri. Mlilie Rabb wako Amuongoze mume wako na arudi kama alivyokuwa hapo awali na zaidi ndio maombi yetu ya dhati.
Pili, inatakiwa umnasihi mumeo kwani wewe ndio unaomjua yeye kwa kiasi kikubwa sana. Jaribu kuangalia wakati unaofaa na uzungumze naye kwa njia nzuri na upole, kwani Allaah Aliyetukuka Anatuambia:
ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ۚ
"Lingania katika njia ya Rabb wako kwa hikmah na mawaidha mazuri. Na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi". [An-Nahl: 125].
Usizungumze naye kwa ghadhabu wala hasira. Jaribu kumkumbusha yaliyopita alivyokuwa mstari wa mbele shuleni katika mas-ala ya Dini na mjulishe hiyo ndio sababu kubwa iliyokufanya wewe kuvutika kuwa mume wako, na mengineyo mazuri yaliyowakaribisha na Allaah Aliyetukuka. Katika nasaha, inawezekana kumpatia vijitabu au kanda zinazozungumzia kuhusu uzuri na fadhila ya Swalah na adhabu ya asiyeswali. Kuna mawaidha mengi ndani ya Alhidaaya yanayoeleea mas-ala ya Swalah na hukmu ya Taarikus Swalaah.
Ikiwa hakuna mabadiliko yoyote yale itakuwa vyema sasa ushirikishe familia yako na yake katika kusuluhisha tatizo hilo kubwa sana katika Dini. Allaah Aliyetukuka Anasema:
وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ بَيْنِهِمَا فَابْعَثُوا حَكَمًا مِّنْ أَهْلِهِ وَحَكَمًا مِّنْ أَهْلِهَا إِن يُرِيدَا إِصْلَاحًا يُوَفِّقِ اللَّـهُ بَيْنَهُمَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا خَبِيرًا ﴿٣٥﴾
Na mkikhofu mafarikiano baina yao wawili, basi pelekeni mwamuzi kutoka watu wa mume na mwamuzi kutoka watu mke. Wakitaka sulhu Allaah Atawawafikisha baina yao. Hakika Allaah daima ni Mjuzi wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [An-Nisaa: 35].
Wakati wa mkutano huo inatakiwa ueleze dhahiri yanayoendelea katika ndoa yenu na mabadiliko ya mumeo katika mas-ala ya msingi ya Dini.
Ikiwa katika mkutano huo hakukupatikana ufumbuzi itabidi uende ukapeleke kesi yako kwa Qaadhi kama wapo katika mji unaoishi au Shaykh anayejulikana kwa uchaji wa Allaah, Dini na uadilifu. Ikiwa baada ya mzunguko wote huo wa kutafuta suluhisho haukupatikana itabidi ufanye Istaakhaarah kumtaka Allaah Akujulishe kama mume huyo unaweza kuendelea kuishi naye au hapana. Lakini kwa kifupi mume asiyeswali si mume anayefaa katika maisha ya Muislamu.
Twakutakia kila la kheri na tunamuomba Allaah Aliyetukuka mumeo huyo abadilike na kurudia katika hali yake ya zamani.
Na Allaah Anajua zaidi