Analewa Sana Ila Mwezi Wa Ramadhwaan Anaacha Kisha Anarudia Tena Baadae Nini Hukmu Yake?

 

 

Analewa Sana Ila Mwezi Wa Ramadhwaan Anaacha Kisha Anarudia Tena Baadae Nini Hukmu Yake?

 

Alhidaaya.com

 

Swali:

 

Assalam alaykum

 

Swali, mtu anaekunya sana pombe, halafu ukifika mwezi mtukufu, ramazani anastop kunywa pombe kwa sababu ya kufunga mwezi mtukufu, mwezi ukiisha analudia pombe, nini hatima yake.

       

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Unywaji wa pombe una madhara makubwa hapa duniani na Kesho Aakhirah. Allaah Aliyetukuka Anatuambia yafuatayo:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٩٠﴾

Enyi walioamini! Hakika pombe na kamari na masanamu na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli; ni najisi na chukizo kutokana na kitendo cha shaytwaan; basi jiepusheni navyo, mpate kufaulu.

 

إِنَّمَا يُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُوقِعَ بَيْنَكُمُ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ فِي الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ وَيَصُدَّكُمْ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ وَعَنِ الصَّلَاةِ ۖ فَهَلْ أَنتُم مُّنتَهُونَ ﴿٩١﴾

Hakika shaytwaan anataka kukutilieni baina yenu uadui na bughudha katika pombe na kamari na akuzuieni kumdhukuru Allaah na Swalaah; basi je mtakoma? [Al-Maa’idah: 90 – 91]

 

Ulevi umeelezwa hapa kama uchafu, uchafu unaofanana na kamari, kuabudu masanamu na kupiga ramli. Ulevi unatia uadui baina ya watu, chuki na unamzuia mtu kutekeleza ‘Ibaadah ya kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kuswali kwa ajili Yake. Mlevi mara nyingi huwa haswali na hupuuza mengi pamoja na kujiingiza katika madhara makubwa sana.

 

Ama kuhusu hilo, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Mwenye kunywa pombe duniani, kisha hakuleta toba, atanywima Aakhirah" [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Hadiyth hii inamaanisha kuwa mlevi anayaendelea na ulevi wake, na akakosa kuomba maghfira kabla ya kufa kwake hatokuwa ni mwenye kuipata Aakhirah. Hii inatuleta katika masharti ya tawbah. Ni hakika kuwa ili tawbah kukubaliwa ni lazima Muislamu atekeleze masharti kadhaa. Ikiwa kosa lake linaingiliana na haki ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) basi mwenye kutubia anatakiwa atimize masharti matatu, nayo ni kama yafuatayo:

 

1.     Aache maasiya kabisa.

2.     Ajute kufanya maasiya.

3.     Aazimie kuwa hatorudia tena maasiya hayo.

 

Lakini inavyoonekana huyu mlevi ni kama anamcheza shere Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kuacha mwezi wa Ramadhwaan peke yake, akidhani kwamba Allaah ni wa Ramadhwaan pekee. Kwa minajili hiyo, hajatimiza masharti ya kukubaliwa tawbah, hivyo kuingia katika kughadhibikiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share