Amekula Vidonge Kutoa Mimba Nini Hukmu Yake?

 

Amekula Vidonge Kutoa Mimba Nini Hukmu Yake?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Assalam Alaekum wa Rahmatu llahi wa Barakatul, Suala langu linahusu Juu Mwanamke aliyekula Vidonge Kwa ajili ya kutoa mimba Nini hukumu yake ifahamike kuwa mwanamke ana akili timamu ila pengine aliafanya haya kuvunja alakati na Baba watoto wake aliemuacha, Ahsanteni sana wa Jazakumu Allaahu Kheir.

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Haifai kwa mwanamke katika Uislamu kutoa mimba kwani kufanya hivyo ni kuua kiumbe cha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), ambacho kimekatazwa kishari’ah kuuliwa ila kwa sababu inayokubalika Kiislamu. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

وَلَا تَقْتُلُوا النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ ۗ وَمَن قُتِلَ مَظْلُومًا فَقَدْ جَعَلْنَا لِوَلِيِّهِ سُلْطَانًا فَلَا يُسْرِف فِّي الْقَتْلِ ۖ إِنَّهُ كَانَ مَنصُورًا ﴿٣٣﴾

Na wala msiue nafsi ambayo Allaah Ameiharamisha (kuiua) isipokuwa kwa haki. Na atakayeuliwa kwa kudhulumiwa, basi Tumemfanya mrithi wake awe na mamlaka.  Lakini asipindukie mipaka katika kuua. Hakika yeye atasaidiwa (kwa shariy’ah). [Al-Israa: 33].

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Kuondoshwa (kuhalikishwa) kwa dunia mbele ya Allaah ni sahali zaidi kuliko kuuliwa kwa Muislamu" (at-Tirmidhiy, an-Nasaa'iy na Ibn Maajah).

 

Uchukivu wa mke kwa aliyekuwa mume wake usimfanye kufanya dhambi kubwa kama la kutoa mimba. Na huko akidhani anamkomoa mume wake wa zamani au kuvunja mahusiano yoyote baina yao, hajui kuwa amejikomoa mwenyewe kwa kuidhulumu nafsi yake na kujiweka pabaya mbele ya Allaah Mtukufu.

 

Na kwa kuwa tayari ashatoa mimba bila dharura yoyote inayokubaliwa na Shari’ah, anachotakiwa hivi sasa ni arudi kwa Allaah kwa kuomba msamaha wa kikweli kweli. Awe atatimiza masharti haya yafuatayo:

 

1.     Kujiondoa katika maasiya hayo.

2.     Ajute sana katika kufanya kosa hilo.

3.     Aazimie kutolirudia tena kosa hilo.

 

 

Bonyeza kiungo kifautacho upate maelezo zaidi:

 

Kutoa Mimba - Hukmu Na Kafara Yake

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share