Kuna Aina Ngapi Za Dhulma?

 

Kuna Aina Ngapi Za Dhulma?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Assalama Alykum

 

Dhumunio ya email hii ni kutaka kuuliza  je kuna aina ngapi za Dhulm

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Dhulma inaweza kuwa ni baina ya binaadamu na Rabb wake au dhulma baina yake na mwenzake.

 

Kumfanyia dhulma Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) nayo ni kumshirikisha, nayo ni dhulma kubwa kabisa. Ilipoteremshwa aayah:  

 

الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ ﴿٨٢﴾

Wale walioamini na hawakuchanganya iymaan zao na dhulma; hao ndio watakaopata amani nao ndio waliohidika. [Al-An'aam: 82]

 

 

Iliwaingiza shaka Swahaba wakamuuliza Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa salaam) "Ee Rasuli wa Allah, nani katika sisi asiyejidhulumu?" Akasema: ((Sivyo hivyo mlivyofahamu, hamkusikia mja mwema (Luqmaan) alivyosema:

 

...يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ﴿١٣﴾

Ee mwanangu! Usimshirikishe Allaah, hakika shirki ni dhulma kubwa mno! [Luqmaan:13]

 

Kwa hiyo kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni dhulma kubwa ambayo inampasa kila Muislamu ajiepueshe na hatari yake kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Humsamehe binaadamu madhambi yote ila yenye kumshirikisha:

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا ﴿٤٨﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amezua dhambi kuu. [An-Nisaa:48]

 

Dhulma baina ya binaadamu ni kuoneana, kuchukuliana haki ya kila aina ikiwa ni mali au inayomhusu mtu kama kumvunjia heshima yake na kadhalika, kama tunavyopata mafundisho katika Hadiyth hizi ziufatazo:

 

Hadiythi ya kwanza:

 

عن ‏ ‏أبي هريرة رضي الله عنه ‏ ‏أن رسول الله ‏ ‏صلى الله عليه وسلم ‏ ‏قال ‏‏)) أتدرون ما المفلس قالوا المفلس فينا يا رسول الله من لا درهم له ولا متاع قال رسول الله ‏ ‏صلى الله عليه وسلم ‏‏ المفلس من أمتي من يأتي يوم القيامة بصلاته وصيامه وزكاته ويأتي قد شتم هذا ‏ ‏وقذف ‏ ‏هذا وأكل مال هذا وسفك دم هذا وضرب هذا فيقعد ‏ ‏فيقتص ‏ ‏هذا من حسناته وهذا من حسناته فإن فنيت حسناته قبل أن ‏ ‏يقتص ‏ ‏ما عليه من الخطايا أخذ من خطاياهم فطرح عليه ثم طرح في النار)) ألترمذي

Imetoka kwa Abu Hurayrah Radhwiya Allaahu 'anhu kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa salaam) amesema: ((Mnamjua nani aliyefilisika?)) Wakasema (Swahaba): Aliyefilisika ni yule miongoni mwetu asiyekuwa na diraham au mali. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa salaam) akasema: ((Aliyefilisika katika umma wangu ni yule atakayekuja siku ya Qiyaamah na Swaalah zake, Swawm zake na Zakah zake, lakini atakuja akiwa amemtukana huyu, amemtuhumu huyu, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya huyu na amempiga huyu, yatachukuliwa mema yake na kulipwa wale aliowadhulumu. Yatakapomalizika mema yake kabla ya kufidia madhambi aliyowakosea wenzake, zitachukuliwa dhambi za wale aliowakosea kisha atajaliziwa yeye na mwishowe atakuwa ni wa kutupwa motoni)) [At-Tirmidhiy]    

 

Hadiyth ya pili:

 

عن أبي هُريرةَ رضي اللهُ عنه قال: قال رسوُل الله صلى الله عليه وسلم (( لا تَحَاسَدُوا، ولا تَنَاجَشُوا، ولا تَباغَضُوا، ولا تَدَابَرُوا، ولا يَبعْ بَعْضُكُمْ على بَيْعِ بَعْضٍ، وكُونُوا عِبادَ اللهِ إخْوَاناً، المُسْلمُ أَخُو المُسْلمِ: لا يَظْلِمُهُ، ولا يَكْذِبُهُ، ولا يَحْقِرُهُ، التَّقْوَى هاهُنا - ويُشِيرُ إلى صَدْرِه ثَلاثَ مَرَّاتٍ - بِحَسْبِ امْرِىءٍ مِنَ الشَّرِّ أن يَحْقِرَ أخاهُ المُسْلِمِ، كُلُّ المُسْلِمِ على الْمسْلِم حَرَامٌ: دَمُهُ ومالُهُ وعِرْضُهُ))رَوَاهُ مُسْلِمٌ     

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya 'anhu)   ambaye amesema: Nabiy (Swalla Allaah 'alayhi wa salaam) kasema: ((Msioneane choyo, wala msizidishiane bei (za vitu), wala msichukiane, wala msipigane mapande (msitengane), wala msishindane kwa kupunguza bei. Lakini kuweni ndugu, enyi  waja wa Allaah, Muislamu ni ndugu wa Muislamu mwenzake, hamdhulumu wala hamvunji, hamwambii uongo wala hamdharau. Ucha wa Allaah  uko hapa (huku akiashiria kifuani kwake kwa vidole vyake) mara tatu. Ni uovu wa kutosha kwa mtu kumdharau ndugu yake Muislamu. Muislamu ameharamishiwa kwa Muislamu mwenzake: damu yake, mali yake na heshima yake)) (Yaani haramu kuchukua mali ya mwenzako, kumuua na kumdhalilisha) [Imesimuliwa na Muslim]  

 

 

Na Allah Anajua zaidi.

 

  

Share