Kizazi Cha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Bado Kinaendelea?
SW
Nawaashukuruni sana kwa msaada mnaotoa na daawah mbalimbali, hukumu, fatwa na masihala mbalimbali kuhusu dini. Allah awakubalie kwa kila jambo lifanyikalo kwa njia ya mwenyezimungu.
Kuna watu wanadai kuwa wao ni kizazi zha Mtume Muhammad (S:A:W). Je kizazi cha mtume kweli bado kinaendelea na kipo kwa sasa?
JIBU:
AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.)
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kizazi cha Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam). Utata katika suala hili linakuja kwa sababu watu wanaona kuwa watu wengi miongoni mwetu Waislamu wanajiita kuwa wao ni Sharifu au Sayyid au Badawi kutegemea na nchi atokayo.
Watu wanaojiita hivyo utakuta wanatoka nchi tofauti na pia utapata hata makabila
Hata hivyo hayo si ya kumfanya mtu aone ajabu kwani watu walihama na kuishi katika nchi tofauti na wakawa ni wenye kuzaa. Vizazi vya baadaye vilichanganya damu ya jinsia mbili tofauti kuwafanya watoto wengine wafanane na baba na wengine wafanane na mama.
Tashwishi nyingine inayopatikana ni kuwapata hawa wenye kujiita kuwa wao ni kizazi cha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hawana maadili wala tabia kabisa. Badala kupeleka mbele Uislamu wanaurudisha na kuutukanisha Uislamu. Na katika sehemu nyingine huwa wanapata maslahi hivyo wengine kujinasibisha na damu ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Haya yote tutawaachia wao wenye kufanya hivyo na Mola wao Mlezi ambaye Atawahukumu Kesho Akhera kwa yale waliyoyafanya hapa duniani kwani Yeye ni Mjuzi na Mwenye habari wa hayo. Ama kizazi cha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kipo na kitaendelea kuwepo. Swali laweza kuuliza kitakuwepo vipi? Hakika hili ni swali zuri nasi tutajaribu kulijibu kwa tawfiki ya Allaah Aliyetukuka.
Mwanzo inaeleweka kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa na mtoto wa kiume aliyeishi mpaka akawa mkubwa. Watoto wote watatu wa kiume waliaga dunia wakiwa wachanga – Qaasim, 'Abdallaah na Ibraahim. Watoto walioishi ni wa kike ambao waliolewa wote wane wakiwa ni Zaynab, Ruqayyah, Ummu Kulthuum na Faatwimah.
Kati ya hao Ummu Kulthuum hakuzaa kabisa katika ndoa yake na 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhiya Allaahu 'anhuma). Ama Zaynab (Radhiya Allaahu 'anha) aliolewa na kuzaa watoto wawili – 'Aliy na Umaymah na wote waliaga dunia wakiwa wachanga. Ruqayyah (Radhiya Allaahu 'anha) aliolewa na kuzaa mtoto mmoja kwa jina 'Abdullaah ambaye aliaga dunia akiwa mchanga. Hawa mabinti watatu wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) waliaga dunia nao kabla ya baba
Kuwa kizazi kitaendelea kuwepo ni dhahiri katika Hadiyth sahihi tunazopata katika Vitabu vya Hadiyth. Tunadhani itatosha kutaja Hadiyth
Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amehadithia kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
'Lau siku moja tu itabakia kwa huu ulimwengu, Allaah Atairefusha siku hiyo, mpaka Amlete mtu aliyetokamana nami au familia yangu ambaye jina la babake litakuwa sawa na babangu. Naye mtu huyo atajaza usawa na uadilifu
Katika Hadiyth nyingine, Ummu Salamah (Radhiya Allaahu 'anha) amehadithia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
'Mahdi atakuwa katika familia yangu, katika kizazi cha Faatwimah' (Abu Daawuud na Ibn Maajah).
Ieleweke kuwa Mahdi huyu kwenye Hadiyth hizi si yule anayetajwa na Mashia ambaye wanasema amejificha pangoni hivi sasa.
Kwa hivyo, bila shaka yoyote kuwa kizazi hicho cha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kitakuwa kipo kinaishi katika hii dunia. Je, wanaodai kuwa ni wao, ndio? Hapo hatutaweza kukujibu kwani Anayejua kuhusu
Na Allaah Anajua zaidi