Asili Ya Roho Zetu
Asili Ya Roho Zetu
Roho ni siri ya Allaah (‘Azza wa Jalla), hakuna ajuaye siri hiyo hata Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakujulishwa. Anasema Allaah (Subhaanau wa Ta’aalaa):
وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ ۖ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٨٥﴾
Na wanakuuliza kuhusu roho. Sema: “Roho ni katika amri ya Rabb wangu. Na hamkupewa ujuzi isipokuwa kidogo tu.” [Al-Israa: 85]
Kwa hiyo hakuna yeyote yule awezaye kuumba roho hata ya kidudu, na Allaah (‘Azza wa Jalla) Ametoa changamoto kwa wanaoabudu na wanaoabudiwa pasi Naye kwamba hawataweza kamwe kuumba roho hata ya nzi kama Anavyosema:
يَا أَيُّهَا النَّاسُ ضُرِبَ مَثَلٌ فَاسْتَمِعُوا لَهُ ۚ إِنَّ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ لَن يَخْلُقُوا ذُبَابًا وَلَوِ اجْتَمَعُوا لَهُ ۖ وَإِن يَسْلُبْهُمُ الذُّبَابُ شَيْئًا لَّا يَسْتَنقِذُوهُ مِنْهُ ۚ ضَعُفَ الطَّالِبُ وَالْمَطْلُوبُ ﴿٧٣﴾
Enyi watu! Imepigwa mfano basi isikilizeni kwa makini! Hakika wale mnaowaomba badala ya Allaah hawawezi kuumba nzi japo wakijumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu chochote kile hawawezi kukiambua tena. Amedhoofika mwenye kutaka matilabu na mwenye kutakiwa.
مَا قَدَرُوا اللَّـهَ حَقَّ قَدْرِهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ ﴿٧٤﴾
Hawakumkadiria Allaah kama inavyostahiki kumkadiria. Hakika Allaah bila shaka ni Mwenye nguvu zote, Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika. [Al-Hajj: 73-74]
Aayah hizo tukufu ni dalili kwamba hao wanaoabudiwa au vitu vinavyoabudiwa si lolote wala si chochote na wala hawawezi kunufaishana au kusaidiana wao kwa wao bali ni wenye kudhalilika duniani na Aakhera.
Allaah (‘Azza wa Jalla) Alikusanya roho za wana Aadam wote baada ya kumuumba Aadam ('Alayhis-Salaam), mpaka za ambao hawakuzaliwa bado, zikachukua ahadi Naye kwamba watamwabudu bila ya kumshirikisha na watamtii. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَأَشْهَدَهُمْ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ ۖ قَالُوا بَلَىٰ ۛ شَهِدْنَا ۛ أَن تَقُولُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَـٰذَا غَافِلِينَ ﴿١٧٢﴾
Na pindi Rabb wako Alipowaleta katika wana wa Aadam kutoka migongoni mwao, kizazi chao, Akawashuhudisha juu ya nafsi zao, “Je, Mimi siye Rabb wenu?” Wakasema: “Ndio bila shaka, tumeshuhudia!” (Allaah Akawaambia): “Msije kusema Siku ya Qiyaamah: hakika sisi tulikuwa tumeghafilika nayo haya.”
أَوْ تَقُولُوا إِنَّمَا أَشْرَكَ آبَاؤُنَا مِن قَبْلُ وَكُنَّا ذُرِّيَّةً مِّن بَعْدِهِمْ ۖ أَفَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ الْمُبْطِلُونَ ﴿١٧٣﴾
Au mkasema: “Hakika baba zetu ndio walioshirikisha kabla, nasi tulikuwa kizazi baada yao. Basi Utatuangamiza kwa yale waliyoyafanya wabatilifu?” [Al-A’araaf: 173]
Hali hiyo ya roho kuwa katika asili yake inaitwa Fitwrah (asili ya maumbile), na imaanisha pia ni kuelemea katika Dini ya haki inayowapasa wana Aadam wote waifuate, na kwamba wajiepushe na upotofu kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا ۚ فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا ۚ لَا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٣٠﴾
Basi elekeza uso wako kwenye Dini yenye kujiengua na upotofu inayoelemea haki. Umbile la asili la kumpwekesha Allaah Aliyowaumbia watu. Hakuna mabadiliko katika uumbaji wa Allaah. Hivyo ndio Dini iliyonyooka sawasawa, lakini watu wengi hawajui. [Ar-Ruwm: 30]
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuthibitishia kwamba wana Aadam wote walizaliwa katika hali ya Fitwrah isipokuwa wazazi wa mtoto ndiyo wanaobadilisha Fitwrah hiyo:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ أَنَّهُ كَانَ يَقُولُ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((مَا مِنْ مَوْلُودٍ إِلَّا يُولَدُ عَلَى الْفِطْرَةِ فَأَبَوَاهُ يُهَوِّدَانِهِ ، وَيُنَصِّرَانِهِ وَيُمَجِّسَانِهِ كَمَا تُنْتَجُ الْبَهِيمَةُ بَهِيمَةً جَمْعَاءَ ، هَلْ تُحِسُّونَ فِيهَا مِنْ جَدْعَاءَ؟)) ثُمَّ يَقُولُ أَبُو هُرَيْرَةَ: وَاقْرَءُوا إِنْ شِئْتُمْ: ((فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا ۚ لَا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّـهِ))
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba alikuwa akisema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema; ((Hakuna kizazi kinachozaliwa (mtoto mchanga) isipokuwa anazaliwa katika 'fitwrah' kisha wazazi wake (humbadilisha na) humuingiza katika dini ya Uyahudi, au Unaswaara au Umajusi, kama mfano mnyama mwenye pembe anavyomzaa mnyama mwenye pembe kama yeye, je, mtahisi kuwa hana pembe? Kisha Abuu Hurayrah akasema: Someni mkipenda: (kauli ya Allaah): ((Umbile la asili la kumpwekesha Allaah Aliyowaumbia watu. Hakuna mabadiliko katika uumbaji wa Allaah)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Ili roho zibakie katika Fitwrah, Allaah (‘Azza wa Jalla) Akatuma Manabii na Rusuli pamoja na Vitabu ili tuwe tunakumbushwa kubakia katika hali hiyo ya asili. Akatuma mwongozo kama Anavyosema:
فَإِمَّا يَأْتِيَنَّكُم مِّنِّي هُدًى فَمَنِ اتَّبَعَ هُدَايَ فَلَا يَضِلُّ وَلَا يَشْقَىٰ ﴿١٢٣﴾
Kisha utakapokufikieni kutoka Kwangu Mwongozo, basi atakayefuata Mwongozo Wangu, hatopotea na wala hatopata mashaka.” [Twaahaa: 123]
Kufuata mwongozo huo vile ni mtihani kwa wana Aadam ili ibainike nani mwenye ‘amali nzuri kabisa. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿١﴾
Amebarikika Ambaye Mkononi Mwake umo ufalme Naye juu ya kila kitu ni Muweza.
الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْغَفُورُ﴿٢﴾
Ambaye Ameumba mauti na uhai ili Akujaribuni ni nani kati yenu mwenye ‘amali nzuri zaidi. Naye ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa kughufuria. [Al-Mulk: 1-2]
Kisha ni khiari ya mtu kuufuata mwongozo au kupotoka kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنسَانِ حِينٌ مِّنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُن شَيْئًا مَّذْكُورًا﴿١﴾
Je haikumfikia insani kipindi fulani katika dahari, hakuwa kitu kinachotajwa?
إِنَّا خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن نُّطْفَةٍ أَمْشَاجٍ نَّبْتَلِيهِ فَجَعَلْنَاهُ سَمِيعًا بَصِيرًا﴿٢﴾
Hakika Sisi Tumemuumba insani kutokana na tone la manii iliyochanganyika ili Tumjaribu; Tukamjaalia mwenye kusikia na kuona.
إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا﴿٣﴾
Hakika Sisi Tumemuongoza njia; ima (awe) ni mwenye kushukuru au mwenye kukufuru. [Al-Insaan: 1-3]
Kuumbwa kwa bin Aadam pamoja na roho yake ni pale mwanamke anaposhika mimba ikatimia miezi minne pindi Allaah (‘Azza wa Jalla) Anapomtuma Malaika Wake kupuliza roho ya huyo kiumbe, na kumwandikia mambo manne kuhusu uhai wake kama ilivyothibiti katika Hadiyth:
عَنْ أَبِي عَبْدِ الرَّحْمَنِ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ رضي الله عنه قَالَ: حَدَّثَنَا رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم -وَهُوَ الصَّادِقُ الْمَصْدُوقُ: ((إِنَّ أَحَدَكُمْ يُجْمَعُ خَلْقُهُ فِي بَطْنِ أُمِّهِ أَرْبَعِينَ يَوْمًا نُطْفَةً، ثُمَّ يَكُونُ عَلَقَةً مِثْلَ ذَلِكَ، ثُمَّ يَكُونُ مُضْغَةً مِثْلَ ذَلِكَ، ثُمَّ يُرْسَلُ إلَيْهِ الْمَلَكُ فَيَنْفُخُ فِيهِ الرُّوحَ، وَيُؤْمَرُ بِأَرْبَعِ كَلِمَاتٍ: بِكَتْبِ رِزْقِهِ، وَأَجَلِهِ، وَعَمَلِهِ، وَشَقِيٍّ أَمْ سَعِيدٍ؛ فَوَاَللَّهِ الَّذِي لَا إلَهَ غَيْرُهُ إنَّ أَحَدَكُمْ لَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ الْجَنَّةِ حَتَّى مَا يَكُونُ بَيْنَهُ وَبَيْنَهَا إلَّا ذِرَاعٌ فَيَسْبِقُ عَلَيْهِ الْكِتَابُ فَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ النَّارِ فَيَدْخُلُهَا. وَإِنَّ أَحَدَكُمْ لَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ النَّارِ حَتَّى مَا يَكُونُ بَيْنَهُ وَبَيْنَهَا إلَّا ذِرَاعٌ فَيَسْبِقُ عَلَيْهِ الْكِتَابُ فَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ الْجَنَّةِ فَيَدْخُلُهَا)) رواه البخاري ومسلم
Amesimulia Abuu 'Abdir-Rahmaan 'Abdillaah bin Mas‘uwd (رضي الله عنه): Ametusimulia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ambaye ni mkweli mwenye kuaminiwa: “Hakika kila mmoja wenu hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arubaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu (za uzazi za mama na baba), kisha arubaini zifuatazo huwa ni donge la damu, kisha arubaini zijazo huwa pande la nyama, kisha Allaah Humtuma Malaika kwake na kumpulizia roho (yake). Na (Malaika huyo) anaamrishwa maneno manne; Kuandika rizki yake, ajali yake (umri atakaoishi duniani), amali zake, mtu muovu au mwema. Wa-Allaahi naapa kwa Yule Ambaye hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, hakika mmoja wenu huenda afanye amali za watu wa Jannah hadi ikawa baina yake na Jannah ni dhiraa na kile kilichoandikwa kikathibiti, akafanya amali ya watu wa motoni akaingia motoni. Na hakika mmoja wenu huenda afanye amali za watu wa motoni hadi ikawa baina yake na moto ni dhiraa na hapo kile kilichoandikwa kikathibiti, akafanya amali ya watu wa Jannah akaingia Jannah.” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Hapo tena itakuwa ni vitu viwili vimeunganika; mwili na roho, na ndio maana mtu anapokufa inasemwa: “Fulani amefariki.” Kwa maana roho yake imetoka na imetengana na mwili wake.