Al-Jannah (Pepo)

 

Al-Jannah (Pepo)

 

Imekusanywa na Ummu ‘Abdillaah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

بسم الله الرحمن الرحيم

 

 

 

Katika mfululizo wa maisha ya Aakhirah, tutaanza kuelezea Al-Jannah (Pepo) na sifa zake za kheri, kisha tutafuatia na Moto na balaa zake.

 

Tukiingia katika maisha ya Peponi yalivyo kama yalivyotajwa na Qur-aan na Hadiyth, ni muhimu kwanza tuifahamu maana ya neno ‘Jannah’ (Pepo). ‘Jannah’ inayoelezwa katika Qur-aan na Hadiyth kuwa ni Bustani nzuri zilizo na matunda ya kila aina, Yenye kupitiwa na mito ya maji mazuri na matamu kuliko asali na meupe kuliko maziwa na yenye harufu nzuri kuliko miski.

 

Pia ndani ya Bustani hii nzuri isiyo na mfano wake patakuwa na majumba ya ghorofa mazuri yasiyo na mfano na yenye fanicha nzuri zisizohadithika. Maalezo ya Qur-aan na Hadiyth katika kuelezea uzuri wa Pepo ni kama mfano tu kwani vipaji hivi vya ufahamu tulivyonavyo ni vya hapa hapa duniani tu na havina uwezo kabisa kuviingiza katika picha sahihi ya matukio yote ya maisha ya Aakhirah. Katika maisha hayo ya Aakhirah watu watakuwa na maaumbile na vipaji vinavyolingana na maisha hayo na kila mja ataona na kuhisi maisha ya huko kwa uhakika. Hivi ndivyo anavyotufahamisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ifuatayo:

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ عَنْ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((قَالَ اللَّهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى: أَعْدَدْتُ لِعِبَادِي الصَّالِحِينَ مَا لَا عَيْنٌ رَأَتْ وَلَا أُذُنٌ سَمِعَتْ وَلَا خَطَرَ عَلَى قَلْبِ بَشَرٍ)) قَالَ أَبُو هُرَيْرَةَ اقْرَءُوا إِنْ شِئْتُمْ: (( فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَا أُخْفِيَ لَهُمْ مِنْ قُرَّةِ أَعْيُنٍ)) البخاري، مسلم، الترمذي وابن ماجه

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa Amesema: Nimewatayarishia waja Wangu wema kile ambacho jicho lolote halijapata kuona na sikio lolote halijapata kusikia na wala haijapata kupita katika moyo wa binaadamu)) Akasema Abuu Hurayrah: Kwa hivyo, soma ukitaka: Basi nafsi yoyote haijui yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho. Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyatenda)) [As-Sajdah: 32:17] [Al-Bukhaariy, Muslim, At-Tirmidhiy na Ibn Maajah]

 

 

Kwa maana ya ujumla, Neno ‘Al-Jannah’ limetumiwa katika Uislamu kama kielelezo cha mazingira mazuri katika maisha ya Aakhirah ambapo watu wema walioishi hapa duniani kwa wema, kwa kufuata barabara kanuni za maisha ya siku kama zilivyowekwa na Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa), Waishi milele kwa furaha na amani. Hali ya mazingira ya maisha ya wenyeji wakazi wa Peponi inafafanuliwa katika Hadiyth zifuatazo:

 

Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) amesimulia kuwa, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: “Hakika wakazi wa Jannah watakula na kunywa lakini hawatakuwa wanatema, Wala hawendi haja ndogo au kubwa, Wala kutokuwa na uchafu puani.”  Waliuliza Maswahaba: “Kitakuwaje chakula?” Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Kitakuwa kitamu kama utamu wa miski na watakuwa wamejazwa na Tasbiyh na Tahmiyd kama walivyojaaliwa kupumua.” [Muslim].

 

Na pia:

عن أبي هريرة رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وآله سلم قال (( أنهار الجنة تفجر تحت تلال أو من تحت جبال المسك ))  إبن أبي حاتم 1:87

Kutoka kwa Abuu Hurayrah kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  ((Mito ya Peponi inachipuka kutoka chini ya vilima au majabali ya misk)) [Ibn Abiy Haatim 1:87]

 

 

Pamoja na Hadiyth hizi, Pia tuangalie na Qur-aan inasemaje juu ya maisha ya Peponi pamoja na wakazi wake na sifa zitakazotuwezesha kuingia katika Jannah.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَنَعِيمٍ ﴿١٧﴾

Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na neema.

 

 

فَاكِهِينَ بِمَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ وَوَقَاهُمْ رَبُّهُمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ ﴿١٨﴾

Wakifurahia kwa ambayo Amewapa Rabb wao, na Akawaokoa na adhabu ya moto uwakao vikali mno.

 

كُلُوا وَاشْرَبُوا هَنِيئًا بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿١٩﴾

 “Kuleni na kunyweni kwa raha kwa sababu ya mliyokuwa mnatenda.”

 

مُتَّكِئِينَ عَلَىٰ سُرُرٍ مَّصْفُوفَةٍ ۖ وَزَوَّجْنَاهُم بِحُورٍ عِينٍ ﴿٢٠﴾

Wakiegemea juu ya makochi ya fakhari yaliyopangwa safusafu, na Tutawaozesha huwr ‘ayn, wanawake weupe wazuri wa Jannah wenye macho makubwa ya kupendeza.

 

 

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَاتَّبَعَتْهُمْ ذُرِّيَّتُهُم بِإِيمَانٍ أَلْحَقْنَا بِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَمَا أَلَتْنَاهُم مِّنْ عَمَلِهِم مِّن شَيْءٍ ۚ كُلُّ امْرِئٍ بِمَا كَسَبَ رَهِينٌ ﴿٢١﴾

Na wale walioamini na wakafuatwa na dhuriya wao kwa iymaan, Tutawakutanisha nao dhuriya wao na Hatutawapunguzia katika ‘amali zao kitu chochote. Kila mtu atawekewa rehani kwa yale aliyoyachuma.

 

 

وَأَمْدَدْنَاهُم بِفَاكِهَةٍ وَلَحْمٍ مِّمَّا يَشْتَهُونَ ﴿٢٢﴾

Na Tutawapa matunda na nyama katika ambavyo wanatamani.

 

 

يَتَنَازَعُونَ فِيهَا كَأْسًا لَّا لَغْوٌ فِيهَا وَلَا تَأْثِيمٌ ﴿٢٣﴾

Watabadilishana humo gilasi za mvinyo usiosababisha maneno ya upuuzi na wala ya dhambi.

 

 

وَيَطُوفُ عَلَيْهِمْ غِلْمَانٌ لَّهُمْ كَأَنَّهُمْ لُؤْلُؤٌ مَّكْنُونٌ ﴿٢٤﴾

Na watawazungukia watumishi vijana kwa ajili yao kama kwamba ni lulu zilizohifadhiwa.

 

 

وَأَقْبَلَ بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ يَتَسَاءَلُونَ ﴿٢٥﴾

Na watakabiliana baadhi yao kwa wengineo wakiulizana.

 

 

قَالُوا إِنَّا كُنَّا قَبْلُ فِي أَهْلِنَا مُشْفِقِينَ ﴿٢٦﴾

Watasema: “Hakika sisi tulikuwa kabla kwenye ahli zetu wenye kuogopa.

 

فَمَنَّ اللَّـهُ عَلَيْنَا وَوَقَانَا عَذَابَ السَّمُومِ ﴿٢٧﴾

Basi Allaah Akatufadhilisha, na Akatuokoa na adhabu ya moto unaobabua.

 

 

إِنَّا كُنَّا مِن قَبْلُ نَدْعُوهُ ۖ إِنَّهُ هُوَ الْبَرُّ الرَّحِيمُ ﴿٢٨﴾

Hakika sisi tulikuwa kabla Tunamuomba Yeye Pekee, hakika yeye Ndiye Mwingi huruma na fadhila, Mwenye kurehemu.” [Atw-Tuwr: 17-28]

 

 

 

Na Anasema pia Allaah ('Azza wa Jalla)

 

إِنَّ أَصْحَابَ الْجَنَّةِ الْيَوْمَ فِي شُغُلٍ فَاكِهُونَ ﴿٥٥﴾

Hakika watu wa Jannah leo wamo katika kushughulika wakifurahi.

 

 

هُمْ وَأَزْوَاجُهُمْ فِي ظِلَالٍ عَلَى الْأَرَائِكِ مُتَّكِئُونَ ﴿٥٦﴾

Wao na wake zao, wakiwa katika vivuli, juu ya makochi ya fakhari wakiegemea.

 

 

لَهُمْ فِيهَا فَاكِهَةٌ وَلَهُم مَّا يَدَّعُونَ ﴿٥٧﴾

Watapata humo kila aina ya matunda, na watapata wanavyoomba.

 

 

سَلَامٌ قَوْلًا مِّن رَّبٍّ رَّحِيمٍ ﴿٥٨﴾

 “Salaamun!” Kauli kutoka kwa Rabb Mwenye kurehemu.     [Yaasiyn: 55-58]

 

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 قُلْ أَؤُنَبِّئُكُم بِخَيْرٍ مِّن ذَٰلِكُمْ ۚ لِلَّذِينَ اتَّقَوْا عِندَ رَبِّهِمْ جَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا وَأَزْوَاجٌ مُّطَهَّرَةٌ وَرِضْوَانٌ مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ بَصِيرٌ بِالْعِبَادِ ﴿١٥﴾

Sema: “Je, nikujulisheni yaliyo bora kuliko hayo? Kwa wale waliokuwa na taqwa kwa Rabb wao watapata Jannaat zipitazo chini yake mito, ni wenye kudumu humo na wake waliotakasika na radhi kutoka kwa Allaah. Na Allaah ni Mwenye kuwaona waja.”

 

 

الَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا إِنَّنَا آمَنَّا فَاغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ﴿١٦﴾ 

Wale wasemao: “Rabb wetu, hakika sisi tumeamini, basi Tughufurie madhambi yetu na Tukinge na adhabu ya moto.”

 

 الصَّابِرِينَ وَالصَّادِقِينَ وَالْقَانِتِينَ وَالْمُنفِقِينَ وَالْمُسْتَغْفِرِينَ بِالْأَسْحَارِ﴿١٧﴾

Wenye kusubiri na wasemao kweli, na watiifu, na watoaji mali katika njia ya Allaah na waombao maghfirah kabla ya Alfajiri.  [Al-‘Imraan: 15-17] 

 

Hebu tuangalie ni furaha ilioje kwa Mume na Mke watakapokutana katika Jannah ya Allaah ('Azza wa Jalla)  na kuyaendeleza Maisha yao kwa raha kamili ambayo haina mfano? Ni raha ilioje hiyo jamani? Pia Ni raha ilioje kukutana na watoto wako katika Al-Jannah na kujumuika pamoja? Na pia kukutana na ndugu na Jamaa huko ni raha ilioje? Sharti la kukutana nao huko Peponi ni wao kubakia katika iymaan na utiifu wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama Anavyosema:

 

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَاتَّبَعَتْهُمْ ذُرِّيَّتُهُم بِإِيمَانٍ أَلْحَقْنَا بِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَمَا أَلَتْنَاهُم مِّنْ عَمَلِهِم مِّن شَيْءٍ ۚ كُلُّ امْرِئٍ بِمَا كَسَبَ رَهِينٌ ﴿٢١﴾

  Na wale walioamini na wakafuatwa na dhuriya wao kwa iymaan, Tutawakutanisha nao dhuriya wao na Hatutawapunguzia katika ‘amali zao kitu chochote. Kila mtu atawekewa rehani kwa yale aliyoyachuma. [Atw-Tuwr: 21]

 

 

Ndug zangu, tujitahidi katika kuitafuta Al-Jannah (Pepo) na si kuihangaikia hii dunia isiyokuwa na manufaa kwetu.

 

Enyi waja wa Allaah! Tushikamane na ‘Ibaadah ili tuweze kufaulu kuipata Jannah ya Allaah ('Azza wa Jalla)  kama Alivyotuahidi Mwenyewe, Tusihadaishwe na mapito ya dunia kwani hakika Mola Wetu Ametuandalia maisha ya milele yasiyo na mfano kwa mwenye kufaulu kwa kumcha Yeye Pekee bila ya kumshirikisha. Kwa hiyo tushikamane na ‘Ibaadah ya kumwabudu Allaah na kufuata yote Aliyokuja nayo Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Na kuacha aliyotukataza.

 

Tunamuomba Allaah Atuongoze na Atujaalie tuwe ni wenye kuipata Al-Jannah, Aamiyn.

 

 

Share