Yaliyopita Yameshapita Hayarudi Tena!

 

Yaliyopita Yameshapita Hayarudi Tena!

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

  عَفَا اللَّـهُ عَمَّا سَلَفَ ۚ

Allaah Ameshasamehe yaliyopita. [ Al-Maaidah: 95]

 

Kutafakari yaliyopita nyuma na huzuni zake ni kujitia wahka na wazimu, aina ya ugonjwa unaoharibu uwezekano wa kutatua hali ya maisha ya sasa. Hakika walio na akili wameshayafungilia mbali majalada yao na kusahau matokeo ya nyuma ambayo hayataona tena mwanga, kwa vile wamefunika kiza chao kwa kishubaka cha mawazo. Matukio yaliyopita yamekwisha, huzuni haiwarudii tena, ghamu haiwezi kusawazisha mambo, na unyong'onyevu hauleti tena maisha ya nyuma. Hii ni kwa sababu yaliyopita hayako tena.

 

Usiishi katika ndoto za vitisho za maisha ya nyuma au katika kivuli ulichokosa kutenda. Jiokoe na kivuli cha pepo kilichopita. Je, unadhani utaweza kurudisha jua mahali pake linapochomoza? Au kumrudisha mtoto tumboni mwa mama yake? Au maziwa yaliyomwagika chomboni? Au machozi kurudi machoni? Ikiwa utaendelea kuwaza sana yaliyopita na matokeo yake, basi unajiweka katika hali ya khofu, msiba na wahka wa akili.

 

Kusoma daftari la nyuma sana ni kupoteza wakati wa sasa. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anataja mambo ya Ummah zilizopita kwa kusema:

 

تِلْكَ أُمَّةٌ قَدْ خَلَتْ ۖ 

 

Huo ni ummah uliokwishapita. [Al-Baqarah 2:134, 141]

 

Siku zimeshapita na mambo yake yameshatoweka, hutonufaika kitu kwa kuendelea kubeba uchunguzi wa maiti kwa kurudisha magurudumu ya historia.

 

Anayerudi katika hali ya maisha ya nyuma, ni kama mtu anayekanda unga ambao umeshakandwa mwanzoni na ni kama anayechonga unga wa mbao kwa msumeno. Wamesema watu wa kale: "Usimtoe maiti kaburini".

 

Msiba wetu ni kutokuweza kupambana na wakati tulionao, tukidharau kasri zetu nzuri, tunaomboleza kwa majumba yaliyobomoka. Wangelijumuika watu na majini kurudisha yaliyopita hakika wangelifeli. Watu hawapaswi kuangalia ya nyuma wala kuangaza yaliyowapita, kwa sababu upepo unaelekea mbele na maji yanatiririka mbele, na msafara unaelekea mbele, basi usiende kinyume na desturi ya maisha!    

 

Kutoka katika kitabu cha: Laa Tahzan.

 

 

 

Share