Kila Nafsi Itaonja Mauti Na Hakuna Atakayebakia Isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى)
Kila Nafsi Itaonja Mauti na Hakuna Atakayebakia Isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى)
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ۗ وَإِنَّمَا تُوَفَّوْنَ أُجُورَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۖ فَمَن زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَأُدْخِلَ الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ ۗ وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا مَتَاعُ الْغُرُورِ ﴿١٨٥﴾
Kila nafsi itaonja mauti. Na hakika mtalipwa kikamilifu ujira wenu Siku ya Qiyaamah. Basi atakayewekwa mbali na moto na akaingizwa Jannah kwa yakini amefuzu. Na uhai wa dunia si lolote ila ni starehe ya udanganyifu. [Al-Imraan: 185]
Tokea kuumbwa kwa Nabiu Aadam (‘Alayhis-salaam) hadi leo na mpaka siku ya Qiyaamah hakuna kiumbe kitakachobakia isipokuwa Mwenyewe Rabb Muumba wa kila kitu kama Anavyosema:
كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ
Kila kitu ni chenye kuhiliki isipokuwa Wajihi Wake. [Al-Qaswasw: 88]
Vile vile Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ ﴿٢٦﴾ وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ ﴿٢٧﴾
Kila aliyekuwa juu yake (ardhi) ni mwenye kutoweka. Na utabakia Wajihi wa Rabb wako Mwenye Ujalali na Taadhima. [Ar-Rahmaan: 26 - 27]
Baada ya kupulizwa Asw-Swuwr (baragumu) siku ya Qiyaamah, viumbe vyote vitakufa kwa mpangilio Anaoutaka Mwenyewe Allaah (‘Azza wa Jalla). Kisha mwisho atabakia Malakul-Mawt (Malaika mtoaji roho) na Allaah (‘Azza wa Jalla). Kisha Allaah (‘Azza wa Jalla) Atamuamrisha Malakul-Mawt ajitoe roho yake mwenyewe. Atakapokufa Malakul-Mawt Atabakia Allaah (‘Azza wa Jalla) Pekee Ambaye ni
الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٣﴾
Wa Awali hakuna kitu kabla Yake, na wa Mwisho hakuna kitu baada Yake, na Aliye juu hakuna kitu juu Yake, na Aliye karibu, hakuna kitu kilichokaribu kuliko Yeye, Naye kwa kila kitu ni Mjuzi. [Al-Hadiyd: 3]
Naye ni Al-Hayyul-Qayyuwm (Mwenye uhai wa maisha, Msimamia kila jambo).
Kisha Allaah (‘Azza wa Jalla) Siku hiyo Atazikusanya ardhi na mbingu katika Mikono Yake kama Anavyosema:
وَمَا قَدَرُوا اللَّـهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٦٧﴾
Na hawakumkadiria Allaah kama inavyostahiki kumkadiria; na hali ardhi yote itatekwa Mkononi Mwake Siku ya Qiyaamah; na mbingu zitakunjwa Mkononi Mwake wa kulia. Subhaanahu wa Ta’aalaa (Utakasifu ni wa Allaah na Ametukuka kwa ‘Uluwa) kutokana na yale yote wanayomshirikisha. [Az-Zumar: 67]
Na Hadiyth ya ‘Umar (Radhwiya-Allaahu ‘anhu):
((يطوي السموات والأرض بيده، ثم يقول: أنا الملك، أنا الجبار، أنا المتكبر، أين ملوك الأرض؟ أين الجبارون؟ أين المتكبرون؟)) مسلم
((Allaah Atazikunja mbingu kwa Mikono Yake, kisha Atasema, Mimi ni Mfalme, Mimi ni Al-Jabbaar (Mwenye Kushurutisha), wako wapi wafalme wa dunia? Wako wapi majabbaar (wanaolazimisha), wako wapi wanaotakabari?)) [Muslim]
Hapo tena Atauliza mara tatu:
لِّمَنِ الْمُلْكُ الْيَوْمَ
((Ufalme ni wa nani leo?)) [Ghaafir:16]
Hapatakuwa na kiumbe yeyote yule wa kujibu, kisha Allaah Mwenyewe Atajijibu:
لِلَّهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّار
Ni wa Allaah Pekee Mmoja, Asiyepingika. [Ghaafir: 16]
Na hapo tena ndipo kila mtu atakuta hesabu yake ya matendo aliyoyatenda duniani ikiwa ni mema au mabaya, hakuna atakayedhulumiwa hata chembe, kwani Allaah (‘Azza wa Jalla) Atahukumu kwa uadilifu baina ya viumbe Vyake. Kila jema Atalilipa kwa mara kumi na kila ovu atahesabiwa mja kwa ovu moja. Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla):
الْيَوْمَ تُجْزَى كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ لَا ظُلْمَ الْيَوْمَ إِنَّ اللَّهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ
Leo kila nafsi italipwa kwa iliyochuma. Hapana dhulma leo. Allaah ni Mwepesi wa kuhisabu)) [Ghaafir: 17]
************