Mahitajio Ya Nafsi: Kuomba Maghfirah Na Kutubia Kwa Allaah (سبحانه وتعالى)

 

Mahitajio Ya Nafsi: Kuomba Maghfirah Na Kutubia Kwa Allaah (سبحانه وتعالى)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Mahitajio ya miili yetu  (chakula) hutoka ardhini ambako ndio asili ya kuumbwa huu mwili. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ مَهْدًا وَسَلَكَ لَكُمْ فِيهَا سُبُلًا وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجْنَا بِهِ أَزْوَاجًا مِّن نَّبَاتٍ شَتَّىٰ ﴿٥٣﴾

 “Ambaye Amekufanyieni ardhi kuwa tandiko, na Akakupitishieni humo njia, na Akateremsha kutoka mbinguni maji.” Na kwayo Tukatoa aina za mimea mbali mbali.

 

كُلُوا وَارْعَوْا أَنْعَامَكُمْ ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّأُولِي النُّهَىٰ ﴿٥٤﴾

Kuleni na lisheni wanyama wenu. Hakika katika hayo bila shaka ni Aayaat (ishara, dalili, zingatio) kwa wenye umaizi.

 

 

مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ ﴿٥٥﴾

Kutokana nayo (ardhi) Tumekuumbeni, na humo Tutakurudisheni, na kutoka humo Tutakutoeni mara nyingine.    [Twaahaa: 53-55

 

Nafsi hali kadhalika mahitajio yake yanotakana na asili yake ambayo ni kutoka juu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

Kwa hiyo, vitu viwili hivi visipopata mahitajio yake utaona kuwa vinadhoofika.   Mwili usipopata chakula basi hudhoofika na mtu akawa amekonda na hata kuumwa. Na nafsi ikikosa mahitaji yake ambayo ni kuwasiliana na kuambatana na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwa kila aina ya ‘ibaadah na kumdhukuru Allaah, basi nayo hudhoofika. Ndipo utamuona mtu ametumbukia katika maasi kwa sababu nafsi yake iko mbali na Muumba wake. Au mtu awe katika dhiki na kukosa furaha kwa sababu nafsi haijamtambua Muumba wake katika mitihani, akatawakali Kwake.     

 

Miongoni mwa ya yanayopelekea kuambatana na Allaah ('Azza wa Jalla) ni kuomba maghfirah na kutubia Kwake.   

 

Bin Aadamu anahitaji kuomba maghfirah kila siku kwa vile hakuna mwana Aadam asiyeingia kosani kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

((كل بني آدم خطاء، و خير الخطائين التوابون)) حسن الألباني صحيح الجامع

((Kila Bin Aadam ni mkosa na mkosa mbora kabisa ni yule anayeomba tawbah)).  [Ameipa daraja ya Hasan Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami']   

 

 

Kwa Rahma ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), bina Aadam hata awe ana makosa mengi, Allaah Anasema kuwa Anaghufuria madhambi hayo:  

 

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾

Sema: Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: “Msikate tamaa na rahmah ya Allaah; hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote; hakika Yeye Ndiye Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu.” [Az-Zumar: 53]

 

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)      Ametuamrisha tumuombe maghfirah na tutubie Kwake katika Aayah nyingi za Qur-aan. Miongoni mwa Aayah hizo ni:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّـهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا عَسَىٰ رَبُّكُمْ أَن يُكَفِّرَ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ  

Enyi walioamini! Tubieni kwa Allaah tawbah ya nasuha (kwelikweli); asaa Rabb   wenu Akakufutieni maovu yenu. [At-Tahriym: 8]

 

Na Anasema pia Allaah ('Azza wa Jalla):

 

وَأَنِ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ يُمَتِّعْكُم مَّتَاعًا حَسَنًا إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى وَيُؤْتِ كُلَّ ذِي فَضْلٍ فَضْلَهُ ۖ وَإِن تَوَلَّوْا فَإِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ كَبِيرٍ﴿٣﴾

Na kwamba: “Mwombeni Rabb wenu maghfirah kisha tubuni Kwake, Atakustarehesheni starehe nzuri mpaka muda maalumu uliokadiriwa; na Atampa kila mwenye fadhila, fadhila Zake. Na mkikengeuka, basi hakika mimi nakukhofieni adhabu ya Siku kubwa.” [Huwd: 3]

 

Na Anasema pia Allaah ('Azza wa Jalla):

 

وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٣١﴾

Na tubuni kwa Allaah nyote, enyi Waumini mpate kufaulu. [An- Nuwr: 31]

 

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kuomba maghfirah na kutubia kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Hadiyth kadhaa miongoni mwazo ni:

 

((يَا أَيُّهَا النَّاسُ تُوبُوا إِلَى اللَّهِ وَاسْتَغْفِرُوهُ، فَإِنِّي أَتُوبُ إِلَى اللَّهِ، وَأَسْتَغْفِرُهُ فِي كُلِّ يَوْمٍ مِائَةَ مَرَّةٍ)))   مسلم

((Enyi Watu tubieni kwa Allaah na muombe maghfirah kwani mimi natubia kwa Allaah na namuomba maghfirah mara mia kwa siku)) [Muslim]

 

Na pia:

 

عَنْ أَبِي مُوسَى عَبْدِ الله بنِ قَبَسٍ الأَشْعَرِيِّ  (رضي الله عنه) عن النَّبيّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قال: ((إِنَّ اللَّهَ تَعَالَى يَبْسُطُ يَدَهُ بِاللَّيْلِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ النَّهَارِ وَيَبْسُطُ يَدَهُ بِالنَّهَارِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ اللَّيْلِ حَتَّى تَطْلُعَ الشَّمْسُ مِنْ مَغْرِبِهَا)) رواه مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Muwsaa ‘Abdillaah bin Qays Al-Ash‘ariyy (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hakika Allaah Anakunjua Mkono Wake usiku ili Apokee tawbah ya mkoseaji mchana. Na Anakunjua Mkono Wake mchana ili Apokee tawbah ya mkoseaji usiku mpaka jua lichomoze Magharibi [mahali linapokuchwa])) [Muslim]

 

Na du’aa kubwa kabisa ya kuomba tawbah ni iitwayo Sayyidul-Istighfaar kama ilivyothibiti katika Hadiyth:

 

 عن شداد بن أوس رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم أنه قال: ((سيد الاستغفار أن يقول العبد: اللّهـمَّ أَنْتَ رَبِّـي لا إلهَ إلاّ أَنْتَ، خَلَقْتَنـي وَأَنا عَبْـدُك، وَأَنا عَلـى عَهْـدِكَ وَوَعْـدِكَ ما اسْتَـطَعْـت، أَعـوذُبِكَ مِنْ شَـرِّ ما صَنَـعْت، أَبـوءُ لَـكَ بِنِعْـمَتِـكَ عَلَـيَّ وَأَبـوءُ بِذَنْـبي فَاغْفـِرْ لي فَإِنَّـهُ لا يَغْـفِرُ الذُّنـوبَ إِلاّ أَنْتَ))  رواه البخاري في صحيحه

Imetoka kwa Shaddaad Bin 'Aws  (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   kasema: ((Du’aa adhimu kabisa ya kuomba maghfirah  ni kusema:    

 

Allaahumma Anta Rabbiy laa ilaaha illaa Anta Khalaqtaniy wa ana ‘abduka wa anaa ‘alaa ‘ah-dika wawa’-dika mastatwa’-tu, a’uwdhu bika min sharri maa swana’-tu, abuw-u Laka bini’-matika ‘alayya wa abuw-u bidhanbiy, faghfir-liy fainnahu laa yaghfirudh dhunuwba illaa Anta

 

((Ee Allaah, Wewe ni Rabb wangu, hapana muabudiwa wa haki ila Wewe, umeniumba mimi na mimi ni mja Wako, nami niko juu ya  ahadi Yako, na agano Lako, kiasi cha uwezo wangu, najikinga Kwako kutokana na shari ya nilichokifanya, nakiri  Kwako kwa kunineemesha, na nakiri kwa madhambi yangu, basi nakuomba unighufurie  kwani hakuna wa kughufuria  madhambi ila Wewe.)) [Al-Bukhaariy]

 

Kwa faida ziyada bonyeza kiungo kifuatacho:

 

Tawbah: Hukmu Na Fadhila Zake

 

 

 

 

 

 

Share