Mwanamke Anaweza Kwenda Hijjah Bila Ya Mume Ikiwa Mumewe Haswali Na Analewa
Mwanamke Anaweza Kwenda Hijjah Bila Ya Mume Ikiwa Mumewe Haswali Na Analewa
Swali:
Asalaam Alaykum Warahmaturullah Taala Wabarakatuh.
Mimi nina mme. mme huyo anakunywa pombe na haswali. Nimejaribu kumlingania kwa hilo bila mafanikio. Mimi Maa Shaa Allaah naswali. Swali langu ni je! naweza kwenda hajj nikijaaliwa? Allaah awajaarie kheri kwa kuunda chombo hiki na kutuelimisha. In Shaa Allaah amiin.
Jibu:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Nabiy, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’aalaa) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Nabiy. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu.
Mwanamke hawezi kwenda Hajj pasi na maharimu wake. Maharimu wake ni yule ambaye kisheria hawezi kumuoa kama baba, ndugu yake wa kiume, ami yake, mjombake au mtoto wake wa kiume ambaye tayari amebaleghe.
Ikiwa hutapata maharimu wa kwenda naye basi Hajj haijakupasa wewe na In shaa Allaah Atakufanyia sahali na wepesi upate wa kwenda naye.
Soma katika viungo vifuatavyo upate ufafanuzi kwa upana:
Mwanamke Asiye Na Mahram Hawajibiki Kufanya Hajj
Hijja Yake Imekubaliwa Ikiwa Amekwenda Bila Mahram?
Mwanamke Kumfanyia Hijja Mtu bila Mahram Haifai
Kulingana na maelezo yako ni kuwa wewe uko katika matatizo makubwa ambayo yanafaa yapatiwe ufumbuzi. Shida uliyo nayo ni ile ya unyumba na ikiwa hutachukuwa tahadhari za Kidini basi huenda na Imani yako ikafifia. Hukutueleza kama mumeo alikuwa akifanya hayo kabla ya kukuoa au vipi. Kwa hali yoyote inatakiwa uchukue hatua za haraka na dharura ili upate ufumbuzi.
Umetuelezea kuwa umejaribu kiasi cha uwezo wako bila mafanikio yoyote. Kwa ajili unatakiwa ufanye yafuatayo:
- Itisha kikao baina yako, mumeo, wawakilishi wa mumeo na wako kwa ajili ya kukaa pamoja ili kutafuta ufumbuzi. Ajenda iwe ni tabia za mumeo wala usifiche. Ikiwa hakutakuwa na muafaka wowote basi,
- Nenda kwa Qaadhi au muhusika yeyote mkubwa wa dini kama Shaykh ambaye ni muadilifu kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo. Ikiwa atajirekebisha utaendelea kukaa naye kama mumeo, na lau hatajirekebisha basi Qaadhi huyo atoe uamuzi wa kukuachisha.
Muislamu hafai kukaa na mume ambaye haswali, kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Baina ya mtu na ushirikina na ukafiri ni kuacha Swalah" [Muslim] na baya zaidi kwa mume huyo wako ni kazidisha madhambi zaidi kwa kunywa na pombe.
Tunakutakia kila la kheri na tawfiki katika mambo yako yote mawili.
Na Allaah Anajua zaidi