Kurudisha Ubikra Haifai Na Ni Udanganyifu
Kurudisha Ubikra Haifai Na Ni Udanganyifu
SWALI:
Nimesoma nakala yenu, nimevutiwa sana na ushauri wenu. lakini kama ilivyo kwa wanaume zipo dawa za kienyeji za kuongeza uume ambazo hazina madhara. Sasa naomba kuuliza hakuna dawa za kienyeji za kuweza kurudisha bikira ambazo hazina madhara? Tafadhali naomba unijibu kwenye email yangu. asanteni sana.
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakika ni kuwa zipo dawa za kienyeji za kurudisha ubikira bandia. Hapa lakini tunataka kuuliza kwa nini mwanamke wa Kiislamu anataka kurudisha ubikira? Hii ni njia ya udanganyifu inayotumiwa na wasichana wanaoolewa hasa kwa siku hizi . Kwa nini wanafanya hivyo? Wao wanafanya hivyo ili kuwadanganya ma-bwana harusi kwa ule usiku wa mwanzo kuwa wao bado ni watahirifu na wamejihifadhi kutokana na zinaa. Wenye kufanya hayo aghalabu huwa wamezunguka na wanaume wengine kabla ya ndoa katika kitendo cha zinaa. Mume anadhania kwa usiku huo wa mwanzo kuwa mkewe ni bikira naye ni wa mwanzo kufungua kizibo ilhali si hivyo.
Ikiwa tayari umeolewa na unaishi na mumeo unatakia nini tena ubikira kwani ubikira ni kama ujana unapopita haurudi tena baada ya kukutana na mumeo.
Tutahadharini hayo kwani Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
" Mwenye kutughushi sisi (kutudanganya) si katika sisi" [Muslim].
Na tufahamu kuwa udanganyifu ni alama moja ya unafiki.
Na Allaah Anajua zaidi