Khitaan (Twahara) Kwa Mwanamke

 

Khitaan (Twahara) Kwa Mwanamke

 

Alhidaaya.com

 

SWALI

 

Assalaam Alaykum,

 

Naomba unifahamishe kama kumfanyia tohara mwanamke ni sahihi au la. Kama ni sahihi je kuna ushahidi wa aayah au hadiyth?

 

Wabillah Tawfiq

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

'Khitaan' (Twahaarah au Tohara) kwa mwanamke ni jambo lisilokatazwa kwenye Uislam, na ni jambo mtu ana khiyari ya kulifanya au kutolifanya lakini si jambo linalokatazwa kama wengi wanavyodhani! Tofauti ya kutahiri huku kunavyofanywa Kiislam na jinsi wanavyofanya baadhi ya makabila na watu wengine, ni tofauti kubwa. Tutazame dalili zifuatazo na maelezo mbalimbali ili tuweze kujua ruhsa ya kufanyika kwake na njia sahihi za kuifanya;

 

Abu Hurayrah amesimulia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Vitu vitano ni katika fitrah, kutahiri, kunyoa nywele za chini, kupunguza masharubu, kukata kucha na kunyofoa nywele za kwapa" [Imepokewa na Al-Bukhaariy, mj. 7, kitabu 72, namba 779]..

 

Baada ya kuona Hadiyth hiyo inayozungumzia 'Twahaarah' kwa ujumla, tuangalie Twahaarah kwa mwanamke katika sheria ya Kiislam:

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema, “Itakapogusa [kitakapokutana] kilichotahiriwa kimoja kugusa kilichotahiriwa kingine, basi yapasa kuoga.” [Al-Bukhaariy].

 

Na amesema tena Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), "Vitakapokutana viwili vilivyotahiriwa, basi ni wajibu kuoga." [Ibn Maajah 611].

 

Na vilivyotahiriwa viwili hapo makusudio ni sehemu ya ngozi inayokatwa katika utupu wa mwanamme na ile ya utupu wa mwanamke. Na ni ushahidi kuwa wanawake walikuwa wakitahiriwa. [Rejea Swahiyh Fiqhus Sunnah mj.1, uk.99].

 

Hadiyth hizo mbili ni sahihi kwa itifaki ya wanachuoni. Na vilevile kuna Hadiyth nyinginezo zenye kuweka wazi zaidi Twahaarah kwa mwanamke kama Hadiyth ya Ummu 'Atwiyah isemayo kwamba yeye alikuwa akitahiri na Nabiy kusikia akasema, "Ukipunguza usimalize kwani ni pendezo kwa uso na tulizo kwa mume."

Na nyingine iliyopokewa na Imam Ahmad kwenye Musnad yake yenye maneno kama hayo, ingawa wametofautiana wanachuoni kuhusu usahihi na udhaifu wa Hadiyth hizo.

 

Baada ya kuona Hadiyth zenye kuthibitisha kuwepo na kuthibiti jambo hilo kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ni vizuri pia tutazame nao Wanachuoni wamefahamu vipi kuhusu suala hilo:

 

Baadhi ya wanachuoni wameona ni wajibu kwa mwanamme na mwanamke pia, na wengine wameona ni 'Mustahab' (lenye kupendeza) kwani hiyo 'Khitaan' kwa mwanamke ni 'Makrumah' (pendezo). Na wanasema kuwa sio wajibu. Na dalili yao ni kuwa 'Khitaan' kwa mwanamme ni jambo la lazima kwa sababu kuna maslaha yanayopatikana katika kutekelezeka masharti ya Swalah ndani yake, nayo ni Twahaarah; kwa maana kama hajatahiriwa, basi mkojo na uchafu ni rahisi kubaki katika ile sehemu ya ngozi ambayo haijakatwa

.

Na kwa upande wa wanawake ni kupunguza matamanio yake ya kijinsia, na ndio faida inayopatikana kwake, na kwa hivyo, kwa kuwa si jambo la kuondosha madhara, inakuwa si wajibu bali ni mapendekezo.

'Khitaan ni wajibu kwa mwanamme na ni Sunnah kwa mwanamke' [Kitabu 'Mukhtasar al-Fiqhil Islaamiy, uk.381]. 'Khitaan kwa mwanamke inazunguka katika hukmu ya wajibu na istihbaab'[Kitabu 'Swahiyh Fiqhus Sunnah' Mj.1, uk.100].

 

Naye mwanachuoni maarufu wa Fiqh, Dr. Wahbah Az-Zuhayliy katika kitabu chake cha Al-Fiqhul Islaamiy wa Adillatuh, anasema katika Juzuu ya 1, ukurasa wa 460, ''Khitaan ni kukata kigozi kilichozidi hadi kichwa kitokeze kwa mwanamme na kwa mwanamke ni kukata kipande kidogo cha juu kwenye kisimi 'clitoris' .

Ama Imamu wanne maarufu wao wana miono ifuatayo:

 

Imam Abu Haniyfah na Imaam Maalik wanasema ni Sunnah kwa wanaume na ni pendezo kwa wanawake.

 

Imaam ash-Shaafi'iy na Imaam Hanbal wao wanasema ni wajibu kwa wanaume na ni wajib vilevile kwa wanawake.

 

Pia katika kauli nyingine ya Imaam Hanbal ni 'Makrumah' kwa Hadiyth ya Nabiy aliposema, "...kata kipande kidogo na wala usimalize", na Hadiyth "Khitaan ni Sunnah kwa wanaume na Pendezo kwa wanawake." [Hadiyth hizi tumeeleza juu hukmu zake].

 

Kuna baadhi ya watu wakiwemo Waislam, na jumuiya za haki za binaadam, haki za wanawake, Umoja wa Mataifa na Nchi za Magharibi wanaopinga kitendo hiki na kukilaani pamoja na kutafuta njia za kila namna za kuzuia na kuharamisha moja kwa moja kwa kigezo kuwa ni 'UKATILI' na kuwa unakiuka haki za wanawake.

Lakini wao ima wanachanganya tohara ya Kiislam na tohara ya kimila na kikabila inayofanywa na wengineo, au wanafanya makusudi kutaka kuzipinga na kuzikosoa sheria zinazohusiana na Uislam kama wafanyavyo katika suala la Mirathi na Adhabu za kukatwa mkono kwa mwizi na zinginezo.

 

Ni jambo ambalo si SAHIHI kulinganisha au kupinga tohara hii ya Kiislam kwa kuwa kuna wanaofanya tohara vibaya na kimakosa.

 

Kwani wao kigezo chao kikubwa ni baadhi ya nchi zifanyazo 'TOHARA' kimila na si Kiislam, tunasema kimila na si Kiislam, kwa sababu,  nchi nyingi haswa za Afrika kaskazini na mashariki, kama vile Somalia, Chad, Sudan, Misr, Tanzania n.k, hizi wao wanachofanya ni KUFYEKA kabisa na sio kupunguza, nako kunaitwa 'UKEKETAJI'!!! Na matokeo yake kumepatikana madhara mengi kama wanawake kupata saratani, kupata taabu wakati wa uzazi, kukosa raha ya tendo la ndoa na hata wengine kufariki kutokana na kupoteza damu nyingi wakati wa kutahiri.

 

Wao wanaondosha kisimi 'clitoris' (clitorectomy) chote pamoja na sehemu ya 'labia minora', ambacho kinashonwa chote na kubakiza uwazi.  Au kuondosha kisimi 'clitoris' chote, 'labia minora' na sehemu ya kati ya 'labia majora', pamoja na sehemu yote ya kiungo cha mwanamke kushonwa na kubakizwa tundu dogo tu. Na utaratibu huu unahitaji kumfunga miguu mtoto kwa kiasi cha wiki tatu. Na hii ndio wengine wakaita kuwa ni tendo au ada ya Ki-Firauni.

 

Na hivyo wafanyavyo, ni kinyume kabisa na ilivyo Kiislam, na wala Uislam haukubaliana na njia hizo zifanywazo na wafanyao hata kama ni WAISLAM!! Kwani si taratibu zilizofundishwa na Mtukufu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Hivyo, kama tulivyoona, ni jambo lenye kupendezwa na si jambo la lazima. Mwenye kutaka kufanya ni bora, na asiyetaka ni khiyari yake, lakini asilaumu wala kuponda kwani ni jambo ambalo lililopo na limethibiti katika Dini.

 

 

Na Allaah Anajua Zaidi

 

Share