Yuko Katika Dhiki Kwa Sababu Posa Zake Zinavunjika, Wadogo Zake Wameolewa Yeye Bado,
Yuko Katika Dhiki Kwa Sababu Posa Zake Zinavunjika,
Wadogo Zake Wameolewa Yeye Bado
SWALI:
Assalam ALeikum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Naomba sheikh nisaidie kwa kunipa dua au mawaidha itakayoburudisha roho yangu mimi nahisi dhiki na huku nakuandikia mimi machozi yananitoka kwa uchungu hata sina la kufanya zaidi ya kumsujudia mola wangu subhana wataala na kumuomba. Mimi ni msichana wa miaka 30 roho yangu inaniuma kuona wenzangu wanaolewa mimi nipo nikisubiri mdogo wangu kishaolewa ana mtoto na inshallah kuna mwingine posa yake mashallah imesimama.
Mimi najiuliza nimekosa nini ila nakubali ni mitihani ya mola wangu subhana wa taala, na zaida kinachoniumiza mimi posa zangu zilizotangilia zikusimamiwa kama za wenzangu na hii ndio inanifanya nilie kila siku. Lakini inshallah mungu yupo hamtupi mja wake kuna siku na saa atanipa. Naomba nijibu kwa kutumia email yangu hapo juu. Shukran na jazakallah kher.
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Hakika ni kuwa dunia hii tunayoishi ni sehemu na mahali pa mitihani. Na kila mwanadamu anapata mitihani aina yake. Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuarifu kuwa:
"Allaah Akiipenda kaumu basi huitia katika mitihani".
Na juu ya mitihani tofauti Allaah Aliyetukuka Anatuarifu:
وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ ۗ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ ﴿١٥٥﴾الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ﴿١٥٦﴾
Na bila shaka Tutakujaribuni kwa kitu katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao. Na wabashirie wenye kusubiri.Wale ambao unapowafika msiba husema: Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea. [Al-Baqarah: 155 – 156).
Na huu ndio mwendo na Sunnah ya Allaah Aliyetukuka katika maisha ya hapa duniani pale Aliposema:
سُنَّةَ اللَّـهِ فِي الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلُ ۖ وَلَن تَجِدَ لِسُنَّةِ اللَّـهِ تَبْدِيلًا ﴿٦٢﴾
Ni desturi ya Allaah kwa wale waliopita kabla. Na wala hutopata mabadiliko katika desturi ya Allaah. [Al-Ahzaab: 62].
Kwa hivyo, mwanadamu ni lazima apitiwe na majaribio katika maisha yake hapa duniani. Na mara nyingi sisi huwa tunalolitaka huwa hatufikirii hatima yake bali kila tulitakalo huliona kuwa ni jema. Lakini sikiliza Anayosema Allaah kuhusu mambo ya hapa, kwa tunayotaka na tusiyoyataka. Anasema Aliyetukuka:
..وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٢١٦﴾
Na asaa mkachukia jambo na hali lenyewe ni khayr kwenu. Na asaa mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui. [Al-Baqarah: 216].
Hivyo basi amini Qadhwaa na Qadar: (Yaliyohukumiwa na Yaliyokadiriwa) na Allaah, ili upate kukinaika na majaaliwa hayo
Hebu sasa turudi katika yanayokukumba katika maisha. Unapata mume wa kukuposa lakini harusi inavunjika, kuvunjika kwake kunaonekana si jambo zuri lakini sisi hatufahamu wala hatujui mazuri yetu. Mwenye kujua yote hayo ni Allaah Aliyetukuka. Kutofanikiwa harusi hizo ni kuwa hazina kheri nawe kwa namna moja au nyingine. Inatakiwa uwe na subira, uzidi kumuomba Allaah Aliyetukuka Akupe mume wa kheri ambaye ataweza kukusaidia na kusaidiana katika unyumba. Wala usidhanie kuwa kukosa mume kuwa una kasoro bali ni aina ya mtihani uliokufikia. Jambo linalotakiwa kwa kila Muislamu ni,
وَاسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلَّا عَلَى الْخَاشِعِينَ ﴿٤٥﴾
Na tafuteni msaada kupitia subira na Swalaah; na hakika hilo ni kubwa isipokuwa kwa wanyenyekevu. [Al-Baqarah: 45].
Zidi kumuomba Allaah Aliyetukuka Akupe mume wa kheri, mwema, mcha wa Allaah na maadili mazuri. Hasa muombe katika nyakati ambamo du’aa hukubaliwa kama saa za usiku unapoinuka kwa ajili ya Tahajjud, unapofunga, na hasa wakati wa kufungua, baina ya adhana na iqaamah, unapokuwa safarini. Bila shaka Allaah Aliyetukuka Atakusaidia wala usifunjike moyo kabisa katika hilo.
Ingia katika kiungo kifuatacho chenye makala nzuri kabisa zilizojaa maliwazo upate kuburudika moyo wako:
Na Allaah Anajua zaidi