Dalili Ya Tawhiyd Kwa Wenye Akili Ni Kutafakari Uumbaji Wa Allaah (عزَّ وجل)

 

 

Dalili Ya Tawhiyd Kwa Wenye Akili Ni Kutafakari Uumbaji Wa Allaah ('Azza wa Jalla)   

 

www.alhidaaya.com

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١٩٠﴾ 

Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na mabadiliko ya mfuatano wa usiku na mchana; bila shaka ni Aayaat (ishara, zingatio) kwa wenye akili.

 

 

الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿١٩١﴾ 

Ambao wanamdhukuru Allaah kwa kusimama  na kwa kukaa na kwa kulala ubavuni mwao na wanatafakari katika kuumbwa mbingu na ardhi (wakisema): “Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu ni Wako tukinge na adhabu ya moto.” [Al-'Imraan: 190-191]

 

 

 

 

 

Aayah hizo mbili tukufu ni Aayah ambazo zinaonyesha dalili ya Tawhiyd  kwa watu wanaotafakari uumbaji wa Allaah ('Azza wa Jalla) ambao wanadhihirisha imani zao kwa matendo yao ya kumdhukuru Rabb wao kwa du'aa na adkhaar kila wakati na popote walipo.

 

 

Na hakika mwenye kutafakari uumbaji wa  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), ndio waliokusudiwa kuwa ni  wenye akili.  Nao hukaa na kutafakari  uumbaji wa mbingu jinsi ulivyo ukubwa wake na umbali wake, na uumbaji wa ulimwengu mzima  pamoja na viliomo ndani yake; vikiwemo nyota mbali mbali zinazozunguka angani, bahari, milima, mabonde, chemchemu za maji, mito, majangwa, miti, mimea, maua yenye rangi na harufu mbali mbali, matunda ya kila aina kwa rangi na ladha mbali mbali ambayo yote yanatokana na maji (mvua) hiyo hiyo ya aina moja tu, wanyama wa kila aina wa angani, ardhini na baharini, madini, na mengi mengineyo ambayo hayahesabiki.  Wenye akili hutafakari pia uumbaji wa mwili wao  na hutafakari pia  sababu na lengo la kuumbwa kwao pamoja na uumbaji wa ulimwengu mzima.  

 

 

Juu ya hivyo hutafakari kuhusu mabadiliko ya mfuatano wa mbingu na ardhi na wakati pia; mfano siku za majira ya baridi kuwa fupi na siku za majira ya joto kuwa refu, kugeuka mchana, usiku na kupambazuka kwa Alfajiri, yote hayo ni kwa amri na uwezo wa  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Mwenye Hikma zote na ndio maana Anasema:

 

  لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١٩٠﴾ 

 …bila shaka ni Aayaat (ishara, zingatio) kwa wenye akili.

 

 

Wanaokusudiwa hapo ni Waumini wenye mawazo ya kutafakari sana kuhusu ukweli wa uumbaji wa  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na si wale wasioamini ambao wao ni kama vipofu wasiokuwa na mawazo kabisa ya kufikiri uumbaji wa Rabb wao ambao wanaishi na kunufaika nao.  Uumbjai ambao unaonekana kila mahali walipo, mchana na usiku, na hata kama wanajua kuwa ni uumbaji wa Allaah ('Azza wa Jalla) Ambaye ni Muumba Mwenye Nguvu na Uwezo wote, lakini wanakanusha haki,  bali wanapuuza. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anataja kupuuza kwao katika kauli Zake:

 

 وَكَأَيِّن مِّنْ آيَةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ يَمُرُّونَ عَلَيْهَا وَهُمْ عَنْهَا مُعْرِضُونَ ﴿١٠٥﴾

Na Aayah (ishara, dalili) ngapi katika mbingu na ardhi wanazipitia na huku wao wanazipuuza.

 

 

 

وَمَا يُؤْمِنُ أَكْثَرُهُم بِاللَّـهِ إِلَّا وَهُم مُّشْرِكُونَ ﴿١٠٦﴾

Na wengi kati yao hawamwamini Allaah isipokuwa wao ni wenye kufanya shirki.  [Yuwsuf: 105-106]

 

 

 

 

 

 

Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Kawaelezea Waumini wanaotafakari, kuwa wao wanamdhukuru Rabb wao kila wakati, popote walipo na vyovyote walivyo na wanashuhudia Utukufu Wake na Uwezo Wake na Rahma zake. Kisha  humtukuza Rabb wao na kutambua kwa kukiri kuwa hakika Allaah ('Azza wa Jalla) Hakuviumba vyote hivyo bila ya sababu bali Kaviumba kwa haki ili awalipe wanaotenda maovu adhabu wanazostahiki na Awalipe wanaofanya mema mazuri  wanayostahiki.  Kisha wanamalizia kumuomba Rabb wao Awaepushe na adhabu ya moto: 

 

 

الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿١٩١﴾ 

Ambao wanamdhukuru Allaah kwa kusimama  na kwa kukaa na kwa kulala ubavuni mwao na wanatafakari katika kuumbwa mbingu na ardhi (wakisema): “Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu ni Wako tukinge na adhabu ya moto.” [Al-'Imraan:191]

 

 

 

 

Hali ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ilivyokuwa wakati zimeteremshwa Aayah hizi ni kama ilivyoelezewa katika Hadiyth:

 

 

 

 روي أن عائشة أم المؤمنين رضي الله عنها سئلت عن أعجب ما رأته من رسول الله صلى الله عليه وسلم فبكت ثم قالت: كان كل أمره عجباً، أتاني في ليلتي التي يكون فيها عندي، فاضطجع بجنبي حتى مس جلدي جلده، ثم قال: ((ياعائشة ألا تأذنين لي أن أتعبد ربي عز وجل؟)) فقلت: يارسول الله: والله إني لأحب قربك وأحب هواك- أي أحب ألاّ تفارقني وأحب مايسرك مما تهواه- قالت: فقام إلى قربة من ماء في البيت فتوضأ ولم يكثر صب الماء، ثم قام يصلي ويتهجد فبكى في صلاته حتى بل لحيته، ثم سجد فبكى حتى بلّ الأرض، ثم اضطجع على جنبه فبكى، حتى إذا أتى بلال يؤذنه بصلاة الفجر، رآه يبكي فقال يارسول الله: مايبكيك وقد غفر الله لك ماتقدم من ذنبك وماتأخر؟ فقال له: ((ويحك يابلال، ومايمنعني أن أبكي وقد أنزل الله عليّ في هذه الليلة هذه الآيات : (إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاخْتِلاَفِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لآيَاتٍ لِّأُوْلِي الألْبَابِ... )    ثم قال: ((ويل لمن قرأها ولم يتفكر فيها)).

 

Imesimuliwa kwamba Mama wa Waumini 'Aishah  (Radhwiya Allaahu 'anhaa) aliulizwa kuhusu jambo la ajabu alilolishuhudia kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Alilia kwanza kisha akasema: "Mambo yake yote yalikuwa ya ajabu. Usiku mmoja alikuja karibu na mimi mpaka ngozi yake ikagusa ngozi yangu na akasema, ((Huniaachi nimuabudu Rabb wangu?)) Nikasema: "Ee Rasuli wa Allaah, Wa-Allaahi, hakika mimi napenda ukaribu wako kwangu (uwe karibu yangu), na pia napenda mahaba yako, kwamba napenda usiwe mbali na mimi, na napenda yale yanayokufurahisha". Akasema ('Aishah):  Akainuka na kutumia kiroba cha maji na akafanya wudhuu wala hakutumia maji mengi. Kisha akasimama akaswali  akalia mpaka ndevu zake zikawa zimerowa. Kisha akasujudu na kulia mpaka akaifanya ardhi  irowe. Kisha akalala kwa upande wa kulia mpaka akaja Bilaal kumjulisha Adhaan ya Alfajiri, akamuuliza:  Ee Rasuli wa Allaah! Jambo gani linakuliza na hali Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amekwishakufutia madhambi yako yaliyotangulia na yanayokuja?" Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Ee Bilaal, na nini kinizuie mimi kulia wakati usiku huu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameniteremshia Aayah hizi?"

 

 إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١٩٠﴾ 

Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na mabadiliko ya mfuatano wa usiku na mchana; bila shaka ni Aayaat (ishara, zingatio) kwa wenye akili.

 

 

الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿١٩١﴾ 

Ambao wanamdhukuru Allaah kwa kusimama  na kwa kukaa na kwa kulala ubavuni mwao na wanatafakari katika kuumbwa mbingu na ardhi (wakisema): “Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu ni Wako tukinge na adhabu ya moto.”

 

 

رَبَّنَا إِنَّكَ مَن تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ ﴿١٩٢﴾

 “Rabb wetu, hakika Umuingizaye motoni, kwa yakini Umemhizi. Na madhalimu hawana yeyote mwenye kuwanusuru.”

 

 

رَّبَّنَا إِنَّنَا سَمِعْنَا مُنَادِيًا يُنَادِي لِلْإِيمَانِ أَنْ آمِنُوا بِرَبِّكُمْ فَآمَنَّا ۚ رَبَّنَا فَاغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَكَفِّرْ عَنَّا سَيِّئَاتِنَا وَتَوَفَّنَا مَعَ الْأَبْرَارِ ﴿١٩٣﴾

 “Rabb wetu, hakika sisi tumemsikia mwitaji anaita kwenye iymaan kwamba ‘mwaminini Rabb wenu’ basi tukaamini.  Rabb wetu, Tughufurie madhambi yetu na Tufutie makosa yetu na Tufishe pamoja na Waumini wema.”

 

 

 رَبَّنَا وَآتِنَا مَا وَعَدتَّنَا عَلَىٰ رُسُلِكَ وَلَا تُخْزِنَا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ إِنَّكَ لَا تُخْلِفُ الْمِيعَادَ ﴿١٩٤﴾

 “Rabb wetu na Tupe Uliyotuahidi kupitia Rusuli Wako, wala Usituhizi Siku ya Qiyaamah; hakika Wewe Huendi kinyume na miadi.”

 

 

فَاسْتَجَابَ لَهُمْ رَبُّهُمْ أَنِّي لَا أُضِيعُ عَمَلَ عَامِلٍ مِّنكُم مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ ۖ بَعْضُكُم مِّن بَعْضٍ ۖ فَالَّذِينَ هَاجَرُوا وَأُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِمْ وَأُوذُوا فِي سَبِيلِي وَقَاتَلُوا وَقُتِلُوا لَأُكَفِّرَنَّ عَنْهُمْ سَيِّئَاتِهِمْ وَلَأُدْخِلَنَّهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ثَوَابًا مِّنْ عِندِ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ عِندَهُ حُسْنُ الثَّوَابِ ﴿١٩٥﴾

Basi Rabb wao Akawaitikia  “Hakika Mimi Sipotezi ‘amali za mtendaji yeyote yule miongoni mwenu akiwa mwanamume au mwanamke, nyinyi kwa nyinyi. Basi wale waliohajiri na wakatolewa majumbani mwao na wakaudhiwa katika njia Yangu, wakapigana na wakauliwa; bila shaka Nitawafutia makosa yao na bila shaka Nitawaingiza Jannaat zipitazo chini yake mito, ni thawabu kutoka kwa Allaah.  Na kwa Allaah kuna thawabu nzuri kabisa.”

 

 

 لَا يَغُرَّنَّكَ تَقَلُّبُ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي الْبِلَادِ ﴿١٩٦﴾

Isikudanganye kabisa kutangatanga kwa wale waliokufuru katika nchi.

 

مَتَاعٌ قَلِيلٌ ثُمَّ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۚ وَبِئْسَ الْمِهَادُ ﴿١٩٧﴾ 

Ni starehe ndogo, kisha makazi yao ni Jahannam. Na ni mahala pabaya mno pa kupumzikia.

 

 

 لَـٰكِنِ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ لَهُمْ جَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا نُزُلًا مِّنْ عِندِ اللَّـهِ ۗ وَمَا عِندَ اللَّـهِ خَيْرٌ لِّلْأَبْرَارِ ﴿١٩٨﴾

Lakini wale waliomcha Rabb wao watapata Jannaat zipitazo chini yake mito, ni wenye kudumu humo, mapokezi kutoka kwa Allaah. Na vilioko kwa Allaah ni khayr kabisa kwa ajili ya wema watiifu.

 

 

وَإِنَّ مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ لَمَن يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَمَا أُنزِلَ إِلَيْكُمْ وَمَا أُنزِلَ إِلَيْهِمْ خَاشِعِينَ لِلَّـهِ لَا يَشْتَرُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ ثَمَنًا قَلِيلًا ۗ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ أَجْرُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ ﴿١٩٩﴾

Na miongoni mwa Ahlil-Kitaabi wamo wanaomwamini Allaah na yaliyoteremshwa kwenu, na yaliyoteremshwa kwao, wananyenyekea kwa Allaah hawabadilishi Aayaat za Allaah kwa thamani ndogo. Hao watapata ujira wao kwa Rabb wao. Hakika Allaah ni Mwepesi wa kuhesabu.

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٢٠٠﴾

Enyi walioamini! Subirini na zidini kuvuta subira na bakieni imara na mcheni Allaah ili mpate kufaulu. [Aal-‘Imraan: 190-200]

 

 

 

 

Kisha akasema: ((Ole wake,  yule anayezisoma lakini hatafakari kwayo))

 

Unapoamka usiku kwa ajili ya kuswali,  ni Sunnah kuzisoma Aayah hizo kwani ilikuwa ni ada ya Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuzisoma Aayah hizi anapoamka usiku kuswali.  Na sisi tunapaswa tufuate Sunnah hii tukufu.

 

 

Ndugu Waislamu, hizo ndizo Aayah ambazo zilimliza Nabiy  wetu mpenzi (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa aalihi wa sallam) akawa hakuweza kulala usiku huo akawa anazisoma na huku analia tu. Hakika ni Aayah tukufu mno zinazosisimua mwili na kushitua nyoyo za wenye akili. Basi tujiulize:

 

Je, tutakuwa katika wale wanaomdhukuru  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kila wakati na popote tulipo? 

 

Je, tutafikiria Uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  wa kuumba vitu vyote vilivyo ulimwenguni na katika uumbaji wa nafsi zetu pia na kufikiria Ufalme na Utukufu wake? Lau kama tutatafakari tunaposoma au kusikia Aayah hizi basi na sisi tutalia kwa khofu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), lakini labda nyoyo zetu zimekuwa ngumu, kwa hivyo inatupasa tumuombe Allaah ('Azza wa Jalla)  Atuajaalie Nuru ya Qur-aan katika nyoyo zetu itujaze imani na khofu ya Rabb wetu.  Aamiyn.

 

 

 

اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ قَلْبٍ لاَ يَخْشَعُ وَمِنْ دُعَاءٍ لاَ يُسْمَعُ وَمِنْ نَفْسٍ لاَ تَشْبَعُ وَمِنْ عِلْمٍ لاَ يَنْفَعُ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَؤُلآءِ الأَرْبَعِ

 

Allaahumma inniy a’uwdhu bika min-qalbin-laa yakh-sha’u, wamin du’aain-laa yasma’u, wamin nafsin-laa tashba’u, wamin ilmin-laa yanfa’u, a’uwdhu bika min haaulail-arba’i

 

Ee Allaah, hakika mimi najikinga moyo usionyenyekea na du’aa isiyosikizwa na nafsi isiyoshiba na elimu isiyonufaisha, najikinga Kwako dhidi ya haya manne.

 

[Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, Swahiyh An-Nasaaiy, Swahiyh Al-Jaami’ (1297)]

 

 Aamiyn

 

 

 

 

Share