011-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Swalah Kulielekea Kaburi, Nia, Takbiyr, Kunyanyua Mikono Na Kufunga Mikono Wa Kulia Juu Ya Kushoto

 

 

 

SWALAH KULIELEKEA KABURI

 

Alikuwa akikataza kuswali kwa kuyaelekea makaburi akisema:

((Msiswali kuelekea makaburi na msiyakalie)).[1]

 

 

 

NIA[2]

 

Na alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema:

((Vitendo vinategemea (vinalipwa kwa) nia na kila mtu atapata kwa mujibu wa kile alichokusudia)).[3]

 

 

TAKBIYR

 

Kisha Yeye (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akianza Swalah kwa kusema:

‘Allaahu Akbar’.[4]

 

Alimuamrisha 'mtu aliyeswali vibaya' afanye kama ilivyotajwa na akamwambia: ((Hakika Swalah ya mtu haikamiliki hadi awe ametawadha kwa wudhuu uliyokamilisha viungo vya mwili kisha akasema Allaahu Akbar)).[5]

 

Pia alikuwa akisema:

((Ufunguo wa Swalah ni Twahara, inaharamishwa (inaanzwa) na Takbiyr na inahalalishwa (inamalizikia) na Tasliym)).[6]

 

Pia "alikuwa akipandisha sauti yake kutamka Takbiyr hadi walio nyuma yake walimsikia"[7]. Lakini "anapoumwa, Abu Bakr alikuwa akipandisha sauti yake kutamka Takbiyr kwa niaba ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم).[8 ]

 

Alikuwa akisema pia:

((Imamu anaposema: Allaahu Akbar, basi sema: Allaahu Akbar)).[9]

 

 

KUNYANYUA MIKONO

 

Alikuwa mara nyingine akinyanyua mikono pamoja na Takbiyr.[10] Mara nyingine baada ya Takbiyr[11] na mara nyingine kabla yake.[12]

 

Alikuwa akiinyanyua kwa kuvinyosha vidole vyake (sio kwa kuvitawanya wala kuvibana pamoja)[13] na "alikuwa akiiweka (mikono) sambamba na mabega yake"[14] ingawa kwa nadra, "alikuwa akiinyanyua hadi ifikie sawa na (ncha ya juu ya) masikio yake".[15]

 

 

KUWEKA (KUFUNGA) MKONO WA KULIA JUU YA MKONO WA KUSHOTO NA KUAMRISHWA KWAKE

 

"Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akiweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto"[16] na alikuwa akisema:

((Sisi, Mitume, tumeamrishwa kukimbilia kufungulia Swawm, kuchelewa (kula) daku na kuweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto katika Swalah)).[17]

 

Vile vile: "alimpitia mtu aliyekuwa akiswali aliyeweka mkono wake wa kushoto juu ya mkono wa kulia, akamvuta kuondosha kisha akauweka wa kulia juu ya kushoto"[18]

 

 

 



[1] Muslim, Abu Daawuud na Ibn Khuzaymah.

[2] An-Nawawiy amesema katika Radhwah Atw-Twaalibiyn (1/224 iliyochapishwa na Maktab Al-Islaamiy): "Nia ni kusudio, kwa hiyo mtu anayetaka kuswali, hutia akilini tayari hiyo Swalah pamoja na yanayohusika nayo ya sifa zake, mfano kama ni Swalah ya kipindi kipi, je, ni Swalah ya faradhi n.k. ndipo huleta hivi vyote katika nia yake pamoja na Takbiyr ya mwanzo".

[3] Al-Bukhaariy na Muslim na wengineo. Imetolewa pia katika Al-Irwaa (Namba: 22).

[4] Muslim na Ibn Maajah. Hadiyth inaashiria kwamba hakuwa akianza (Swalah) kwa maneno ya baadhi ya watu: "Nawaytu Uswalliy… n.k" ambayo imekubalika kuwa ni bid'ah (uzushi). Bali wamekhitilafiana kama ni bid'ah njema au mbaya ambayo tunasema: Hakika bid'ah zote katika ibada ni upotofu, kutokana na kauli (صلى الله عليه وآله وسلم) ((…na kila bid'ah ni upotofu na kila upotofu ni motoni)). Lakini hapa sipo mahali pa maelezo marefu ya mas-ala haya.

[5] Atw-Twabaraaniy ikiwa na isnadi Swahiyh.

[6] Abu Daawuud, At-Tirmidhiy na Al-Haakim ambao wamekiri usahihi wake na Adh-Dhahaabiy amekubali. Imetolewa katika Al-Irwaa (Namba: 301). Maana hasa ya 'inaharamishwa na Takbiyr', ni vitendo vyote ambayo Allaah Ameviharamisha wakati huo. 'na inahalalishwa na Tasliym' ni yote yaliyoruhusiwa nje ya Swalah. Kama vile Hadiyth ilivyothibitsha kuwa mlango wa Swalah umefungwa, hakuna mwenye kuabudu anaweza kufungua isipokuwa kwa Twahara, imethibitisha pia kuwa Swalah haiwezi kufunguliwa (kuanzishwa) isipokuwa kwa Takbiyr na haiwezi kumalizika bila ya Tasliym. Hii ni rai iliyokubalika kwa wengi wa Maulamaa.

[7] Ahmad, Al-Haakim ambao wamekiri kuwa ni Swahiyh na Adh-Dhahabiy amekubaliana.

[8] Muslim na An-Nasaaiy.

[9] Ahmad na al-Bayhaqiy ikiwa na isnaad Swahiyh.

[10] Al-Bukhaariy na An-Nasaaiy.

[11] Al-Bukhaariy na An-Nasaaiy.

[12] Al-Bukhaariy na Abu Daawuud.

[13] Abu Daawuud, Ibn Khuzaymah (1/62/2, 64/1), Tammaam Na Al-Haakim ambao wamekiri ni Swahiyh na Adh-Dhahaabiy amekubaliana.

[14] Al-Bukhaary na An-Nasaaiy.

[15] Al-Bukhaariy na Abu Daawuud.

[16] Muslim Na Abu Daawuud, pia imetolewa katika Al-Irwaa (352).

[17] Ibn Hibbaan na Adh-Dwiyaa ikiwa na isnaad Swahiyh.

[18] Ahmad Na Abu Daawuud ikiwa na isnaad Swahiyh.

 

Share